JUMAPILI YA 14 MWAKA C na Fr. Lawrence Muthee, SVD

downloadjesus-sends

‘go’

 

 

Tumsifu Yesu Kristu. Leo ni Jumapili ya 14 ya Mwaka C. Masomo ya leo yanatuhimiza kuweka imani na matumaini yetu kwa Mungu kama msingi wa maisha mema.

Katika Somo la Kwanza, nabii Isaya anawapa moyo Waisraeli kwamba Mungu angewarejesha katika hali ya ufanisi waliokuwa nayo kabla ya uhamisho Babeli. Anamlinganisha Mungu na mama anayemtunza mwanawe.

Mji mkuu wa Israeli – Yerusalemu ulikuwa umesalia majibu tu baada ya kuharibiwa mwaka wa 586 KK na Wababilonia chini ya mfalme Nebukadineza. Isaya anawaambia Waisraeli kwamba Mungu hajawaacha hata kama ilionekana hivyo katika taabu zao.

Taabu na matatizo ya Waisraeli yalitokana na kuasi sheria ya Bwana Mungu. Hata hivyo Mungu hajawaacha waangamie kabisa. Ana mpango wa kuwaokoa.

Sisi pia mara kwa mara huwa tunajikuta katika hali mbaya na matatizo kwa sababu ya kumsahau Mungu. Ujumbe wa leo ni kwamba tusione haibu kumrudia Mungu na kumwomba msamaha wa dhambi zetu. Yeye ni baba ambaye aachi kutupenda hata tunapomkana kwa tabia na matendo yetu maovu. Miungu mingine haina uwezo mzuri.

Katika somo la pili, Paulo anaendelea kutetea Imani yake katika Kristu na kwamba utakatifu mbele za Mungu unakuja tu kwa njia ya Yesu Kristu wala sio kwa njia ya sheria. Kwake Paulo, imani sio wazo au dhana tu isioyokuwa na mashiko bali ni mtazamo wa maisha unaomfanya mtu kumtegemea Yesu kama mkombozi wa maisha yake.

Paulo anapingana na wale walioshikilia mawazo kwamba sheria ya Kiyahudi ilikuwa muhimu kuliko imani katika Kristu. Yeyé mwenyewe alikuwa na msimamo huo kabla hajakutana na Yesu njiani na kumbadilisha mawazo. Tangu wakati huo, msalaba wa Yesu ulichukuwa nafasi kubwa katika imani ya Paulo.

Alama ya msalaba ni dhihirisho ya sadaka aliyotoa Yesu kwa kutupenda sisi, ili atuokoea kotokana na utumwa dhambi na mauti ya milele, ambayo yalikuwa matokeo wa dhambi.

Wakati mwingine sisi pia tunasahau mambo muhimu ya imani yetu kama vile huruma, msaada kwa wanyonge, utu wema, nk, na kung’ang’ania sheria ndogo ndogo tulizopokezana wenyewe ambazo sio muhimu. Hii inatufanya tuonekane na watu kuwa wenye imani kuu lakini kwa ndani hatuna moyo wa upendo kwa wengine.

Msalaba ndio kitambulisho chetu kama Wakristu na hususan Wakatoliki. Imani yetu katika wokovu wa msalaba inatufanya tuishi tofauti na malimwengu. Hii ina maana kwamba lazima kuepuka mambo ambayo ulimwengu unaona mazuri lakini kinyume cha Ukristu. Hili sio jambo rahisi kwani tunaishi kati ya watu ambao hawaamini kama sisi.

Changamoto za maisha ndizo msalaba wetu. Tunaweza kuweka msalaba wetu chini na kukubali kushindwa. Katika kituo cha pili cha njia ya msalaba kuna sala inayoorodhesha misalaba katika maisha, kama vile, kazi, mme, mke, watoto, joto, baridi, nk. Hii inatufundisha kwamba msalaba sio kitu kibaya ambacho tunapaswa kukiogopa au kuuepuka bali ni chombo muhimu cha wokovu katika Yesu Kristu.

Msalaba ni njia ambayo Yesu alitumia kutuokoa. Vile vile, sisi pia tunapaswa kukubali misalaba yetu kama njia ya wokovu. Kuna sehemu zingine za kuabudu ambapo waamini wanaahidiwa kuondolewa misalaba yote. Bila msalaba hamna wokovu.

Kama Mtume Paulo, inatupasa pia kujilinganisha na Kristu msulubiwa. Wakati tunapambana kuishi imani yetu kwa kuvumilia changamoto za ndoa, watoto, kazi, magonjwa, kutengwa, uongozi, nk, ina maana kwamba tunatembea nyuma ya Yesu tukibeba misalaba yetu kwa imani kuu.

Wanaofikiria kuwa kumfuata Kristu ni maisha ya kifahari, anajindanganya. Kuna tofauti ya maisha ya kifahari na maisha mema. Maisha mema yana furaha ya kudumu tofauti na maisha ya kifahari yanayotegemea mali zisizodumu.

Katika somo la Injili Yesu anawapa maagizo wanafunzi wake kabla hajawatuma kufanya utume kadiri walivyosoma kutoka kwake. Hiki ni kikundi kikubwa cha watu 72 ambacho kinaashilia utume mkubwa kwa mataifa yote.

Yesu anawaonya kwamba watakumbana na upinzani. Hilo lisiwe ajabu kwao watakapokataliwa na kisimangwa na watu wasiopenda kubadili mienendo yao mibaya. Leo pia upinzani huu bado upo. Kutakuwa na mbwa mwitu wengi ambao lengo lao ni kuwashambulia na kuwaangamiza kondoo. Hii haikuwa kuwaweka hufu bali kuwaonya kwamba utume hautakuwa rahisi.

Hawakupaswa kubeba vitu vingi, maana yake ni kwamba wamtegemee Mungu katika utume wao. Anawaambia “wasimsalimie mtu njiani” maana yake ni kwamba utume wao sio wa kufanya marafiki binafsi bali kumwakilisha Yesu na kufanya kazi aliyowapa kwa kwa dharura sana.

Anawatuma kupeleka amani katika miji na nyumba za watu. Amani ni hali ya kuwa na uhusiano mwema na Mungu. Mtu ambaye hana uhusiano mwema na Mungu hawezi kuishi kwa amani. Yesu anawaambia wabaki katika nyumba watakapokaribishwa ili wasiwe wanahangaika kutafuta hifadhi nzuri na kusahau kazi yao.

Pia anawaagiza watangaze habari njema ya ufalme wa Mungu na kuwaponya walio wagonjwa. Watakaowakubali watafaidi neema ya Mungu.

Ujumbe mkuu hapa ni kwamba utume wetu ni utume wa Yesu, na ili kuufanya vizuri lazima tutambue Yesu kama kiongozi wa utume huu. Tukiubadilisha kuwa nafasi ya kutafuta umarufu binafsi tutashindwa kwa sababu Yesu atajitenga nao.

Wanafunzi waliporudi walimsimulia Yesu jinsi hata pepo wachafu walivyowatii kwa jina lake. Hii ina maana kwamba utume wa mitume ulikuwa na nguvu za kushinda maovu yaliyoletwa na Shetani. Hii ndiyo maana ya ujio wa ufalme wa Mungu. Pia Yesu anawahakikishia kwamba mradi wafanye kazi yake, hakuna kitu kitakachowadhuru.

Lakini pia Yesu anawaonya mitume dhidi ya kufurahi kwa sababu pepo waliwatii bali kwamba wamekwisha kuhesabiwa uzima wa milele mbinguni katika yeye. Utume ni njia ya wokovu kwake aliyetumwa. Sisi pia tunapaswa kumshukuru Mungu kwa kutujalia kuwa wafanyakazi katika shamba lake wala sio kiburi mbele ya wengine. Ufalme wa Mungu unadai unyenyekevu katika yote. Tumwombe Mungu atujalie neema hii. Amina.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Blog at WordPress.com.

Up ↑

%d bloggers like this: