Faith Matters/Imani

Know your faith

Mafundisho ya Sakramenti

MTIHANI WA UBATIZO

Ishara ya Msalaba

Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu Amina

SALA NI NINI?

Sala ni kusungumza na Mungu au kuinua mioyo yetu na kutazama mbinguni kunapotoka msaada wetu (KKK 2559). Wakati tunaposali tunaingia katika uhusiano, mawasiliano hai na ya kipekee na Mungu. Sala ni sehemu muhimu sana katika imani. Yule anayesali haishi tena kivyake, mpweke au kwa nguvu zake. Anajua kwamba kuna Mungu ambaye anaweza kusungumza naye. Yule anayeomba ujikabidhi kwa Mungu kwa vyote na kwa yote.

Uwepo wa Mungu: Sala sio njia ya kusungumza na Mungu tu, bali pia ni njia ya kutambua uwepo wa Mungu katika maisha yetu. Kila tusalipo tunakiri kwamba Mungu yupo na anatusikiliza. Mtu anayesali mara kwa mara huwa haanguki katika dhambi kirahisi kwa sababu ndani yake anatambua kuwa Mungu yupo pamoja naye na anakuwa na hofu takatifu mbele za Mungu.

KANUNI YA IMANI

Nasadiki kwa Mungu Mmoja/ Baba mwenyezi/ muumba wa mbingu na dunia/ na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana/

Nasadiki kwa Bwana mmoja Yesu Kristo/ Mwana pekee wa Mungu/ aliyezaliwa kwa Baba tangu milele yote/ Mungu aliyetoka kwa Mungu/ mwanga kwa mwanga/ Mungu kweli kwa Mungu kweli/ aliyezaliwa bila kuumbwa/ mwenye umungu mmoja na Baba/ Ambaye vitu vyote vemeumbwa naye/

Alishuka kutoka Mbiguni/ kwa ajili yetu sisi wanadamu/ na kwa ajili ya wokovu wetu/ Akapata mwili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu/ kwake yeye Bikira Maria/ akawa mwanadamu/

Akasulibiwa kwa ajili yetu sisi/ kwa mamlaka ya Ponsyo Pilato/ Akateswa/ akafa/ akazikwa/ siku ya tatu akafufuka/ kadiri ya Maandiko/ akapaa Mbinguni/ ameketi kuume kwa Baba/ Atakuja tena kwa utukufu/ kuwahukumu Wazima na wafu/ na ufalme wake hautakuwa na mwisho/

Nasadiki kwa Roho Mtakatifu/ Bwana mleta uzima/ atokaye kwa Baba na Mwana/ Anayeabudiwa na kutukuzwa/ pamoja na  Babana Mwana/ aliyenena kwa vinywa vya manabii/

Nasadiki kwa Kanisa moja/ takatifu/ Katoliki la Mitume/ Naungama ubatizo moja/ kwa maondoleo ya dhambi/ Nangojea na ufufuko wa wafu/ na uzima wa milele ijayo/ Amina.

BABA YETU

Baba yetu uliye mbinguni/ jina lako litukuzwe/ ufalme wako ufike/ utakalo lifanyike duniani kama mbinguni/ utupe leo mkate wetu wa kila siku/ utusamehe makosa yetu/ kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea/ usitutie katika kishawishi/ lakini utuopoe maovuni.

SALAMU MARIA

Salamu Maria/ umejaa neema/ Bwana yu nawe/ umebarikiwa kuliko wanawake wote/ na Yesu mzao wa tumbo lako amebarikiwa/ Maria mtakatifu mama wa Mungu/ utuombee sisi wakosefu/ sasa na saa ya kufa kwetu/ Amina.

ATUKUZWE

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu/ kama mwanzo na sasa na siku zote na milele/ Amina.

AMRI ZA MUNGU

1. Ndimi Bwana Mungu wako/ usiabudu miungu mingine/

2. Usitaje bure jina la Mungu wako/

3. Shika kitakatifu siku ya Mungu/

4. Waheshimu baba na mama/ upate miaka mingi na heri duniani/

5. Usiue/

6. Usizini/

7. Usiibe/

8. Usiseme uongo/

9. Usitamani mwanamke asiye mke wako/

10. Usitamani mali ya mtu mwingine/

AMRI ZA KANISA

1. Hudhuria Misa takatifu Dominika na Sikukuu zilizoamriwa/

2. Funga siku ya Jumatano ya Majivu na usile nyama Ijumaa Kuu/

3. Ungama dhambi zako walau mara moja kila mwaka/

4. Pokea Ekaristi Takatifu hasa wakati wa pasaka/

5. Saidia kanisa katoliki kwa zaka/

6. Shika sheria katoliki za ndoa/

SALA YA IMANI

Mungu wangu/ nasadiki maneno yote linayosadiki/ linayofundisha kanisa katoliki la Roma/ kwani ndiwe uliyetufumbulia hayo/ wala hudanganyiki/ wala hudanganyi/ Amina.

SALA  YA MATUMAINI

Mungu wangu/ natumaini kwako nitapewa kwa njia ya Yesu Kristu/ neema zako duniani na utukufu mbinguni/ kwani ndiwe uliyeagana hayo nasi/ nawe mwaminifu/ Amina.

SALA YA MAPENDO

Mungu wangu/ nakupenda zaidi ya chochote/ kwani ndiwe mwema/ ndiwe mwenye kupendeza/ nampenda na jirani yangu kama nafsi yangu kwa ajili yako/ Amina.

SALA YA KUTUBU

Mungu wangu/ nimetubu sana dhambi zangu/ kwani ndiwe mwema/ ndiwe mwenye kupendeza/ wachukizwa na dhambi/ Basi sitaki kukosa tena/ nitafanya kitubio/ naomba neema yako nipate kurudi kwako/ Amina.

SALA YA MALAIKA MLINZI

Malaika mlinzi wangu/ unilinde katika hatari zote za roho na mwili/ Amina.

MALAIKA WA BWANA

Malaika wa Bwana alimpasha habari Maria/ naye akapata mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu/

Salamu Maria…

Ndimi mtumishi wa Bwana—nitendewe ulivyonena

Salamu Maria…

Neno la Mungu akatwaa mwili—akakaa kwetu

Salamu Maria….

Utuombee mzazi mtakatifu wa Mungu—tujaliwe ahadi za Kristu/ Salamu maria…

Tuombe: Tunakuomba Ee Bwana utie neema yako mioyoni mwetu/ ili sisi tuliojua kwa maelezo ya malaika kwamba/ mwanao amejifanya mtu / kwa mateso na msalaba wake/ tufikishwe kwenye utukufu na ufufuko/ Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu/ Amina.

MALKIA WA MBINGU

Malkia wa mbingu furahi—Aleluya

Kwani uliyestahili kumchukua—Aleluya

Amefufuka alivyosema—Aleluya

Utuombee kwa Mungu—Aleluya

Furahi/ shangilia/ ee Bikira Maria—Aleluya

Kwani hakika Bwana amefufuka—Aleluya

Tuombe: Ee Mungu uliyependa kuifurahisha dunia/ kwa kufufuka kwake Bwana wetu Yesu Kristu mwanao/ Fanyiza twakuomba/ kwa ajili ya Bikira Maria/ tupate nasi furaha za uzima wa milele/ Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu/ Amina.

UJE ROHO MTAKATIFU

Uje Roho Mtakatifu/ uzienee nyoyo za waumini wako/ peleka roho wako/ vitaumbwa vipya na nchi zitageuka.

Tuombe: Ee Mungu uliyefundisha nyoyo za waumini wako/ kwa kuwaletea mwanga wa Roho Mtakatifu/ tunakuomba utuongoze na yule Roho/ tupende yalio mema/ na tupate daima faraja  zake/ Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu. Amina

SALA YA NAMUUNGAMIA

Namuungamia Mungu Mwenyezi. Nanyi ndugu zangu. Kwani nimekosa mno. Kwa mawazo, kwa maneno, kwa vitendo na kwa kutotimiza wajibu. Nimekosa mimi, nimekosa mimi, nimekosa sana. Ndio maana nakuomba Maria mwenye heri, Bikira daima, Malaika na watakatifu wote. Nanyi ndugu zangu, mniombeeni kwa Bwana Mungu wetu. Amina.

SALA KABLA YA CHAKULA

Ee Mungu wangu, nakuomba unibariki mimi na hiki chakula ulichonijalia, ili nipate nguvu za kukutumikia vyema. Amina.

Tunapaswa kusali lini?

Tunapaswa kusali kila wakati bila kukata tamaa.

Amri ipi ina ahadi?

Amri ya nne, inayosema “Waheshimu baba na mama upate heri na miaka mingi duniani.

Mungu ni nani? Mungu anaishi wapi?

Mungu ni Baba yetu wa Mbinguni aliyeumba vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Mungu huishi Mbinguni.

Kwa nini Mungu alituumba?

Mungu alituumba ili tumjue, tumpende, tumuheshimu, tumuabudu, tumtumikie na baada ya maisha aliyotupa hapa duniani, turudi kuishi naye milele mbinguni.

Mungu ni wangapi?

Mungu ni mmoja anayejidhihirisha katika nafsi tatu yaani Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu.

Utatu mtakatifu ni nani?

Ni nafsi tatu za Mungu yaani Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.

Yesu Kristu ni nani?

Ni Mungu Mwana au nafsi ya pili ya Mungu ambaye ndiye Mkombozi wa wanadamu.

Roho Mtakatifu ni nani?

Ni nafsi ya Tatu ya Mungu ambaye anatoka kwa Baba na Mwana na ndiye anayetusaidia kumjua na kumwamini Mungu.

Bikira Maria ni Nani?

Ni Mama wa Yesu Mungu Mwana na hivyo anaitwa Mama wa Mungu au kwa Kigiriki Theotokos.

Mt. Yosefu ni Nani?

Ni baba mlezi wa Yesu aliyeteuliwa na Mungu kabla ya kuzaliwa kwa Yesu.

Malaika ni nani?

Malaika ni viumbe vya Mungu vyenye roho, akili na utashi lakini bila mwili.

Mtu ni nani?

Mtu ni kiumbe chenye mwili na roho kilichoumbwa kwa sura na mfano wa Mungu tofauti na wanyama wengine.

Sala ni nini?

Sala ni njia ambayo mwanadamu anazungumza na kumsikiliza Mungu.

Yesu alifundisha sala ipi? Inapatikana wapi katika Biblia?

Yesu alitufundisha sala ya Baba Yetu inayopatikana Mt. 6:9-13

Nani anapaswa kusali?

Watu wote wanapaswa kusali wema na wabaya

Kwa nini tunaenda Kanisani?

Ni jukumu letu kama wakristu waliokombolewa kwa mateso, kifo na ufufuko wake Yesu Kristu kuadhimisha siku ya Mungu kwa ibada na sadaka kama alivyoagiza Mungu katika amri ya tatu.

Jumuiya Ndogondogo ni nini?

Ni watu wanaoishi pamoja na kushirikishana imani yao kwa maneno, sala na matendo ya kiinjili.

Kanisa ni nini?

Kanisa ni watu wa Mungu, familia ya Mungu, Hekalu la Roho Mtakatifu ambalo Kichwa chake ni Kristu mwenyewe. Kanisa pia ni njia ya wokovu wa wanadamu.

Parokia ni nini?

Parokia ni Kanisa mahalia ambapo Sakramenti na ibada zote za Kanisa uadhimishwa. Parokia inaongozwa na Paroko kwa niaba ya Askofu. Katika kanisa kuu la parokia kuna tabernakulo inayomhifadhi Yesu wa Ekaristi.

Jimbo ni nini?

Jimbo ni Kanisa Mahalia lililokamilika na linaloongozwa na ya Askofu

Jimbo kuu ni nini?

Ni Kanisa mahalia lililokamilika na linaloongozwa na Askofu Mkuu.

Sakramenti ni nini?

Ni ishara wazi inayoonekana kwa macho ya neema ya Mungu isiyoonekana kwa macho ila imani tu. Sakramenti zilifanyizwa kwanza na Yesu aliye mwenyewe Sakramenti ya Mungu Baba ili zilete neema au kuzindisha neema mioyoni mwetu. Sakramenti pia ni milango ya neema ya Mungu.

Sakramenti ni ngapi? Taja

Sakramenti ni saba yaani: Ubatizo, Ekaristi, Kipaimara, Kitubio, Mpako wa Wagonjwa, Daraja Takatifu na Ndoa

* Katika Ubatizo wanadamu wanasamehewa dhambi na kufanyika wana wa Mungu.

* Katika Kipaimara wanyonge upata nguvu, wanakuwa Wakristu imara na waliojitolea.

* Katika Ekaristi walio na njaa ya kiroho ushibishwa na kupata nguvu ya kiroho.

* Katika Kitubio wenye dhambi usamehewa na kupatanishwa na Mungu na jirani.

* Katika Upako wa Wagonjwa wanaokata tamaa ufanywa wajasiri wa kuvumilia mateso.

* Katika Upadrisho na Ndoa ubinafsi unaondolewa na kuwafanya wale wanaozipokea watumishi wa upendo.

Sakramenti za wafu ni zipi?

Hizi ni Ubatizo na Kitubio ambazo umuondolea mwanadamu dhambi ya asili au dhambi baada ya ubatizo. Roho yenye dhambi ni imekufa au ipo karibu na kifo.

Sakramenti za walio hai ni zipi?

Hizi ni Ekaristi Takatifu, Kipaimara, Mpako wa Wagonjwa, Daraja Takatifu na Ndoa ambazo upokewa na wale tu walio hai baada ya kujitakaza dhambi zao.

Sakramenti ya ubatizo ni nini?

Ni Sakramenti inayomuondolea mwanadamu dhambi ya asili na dhambi zingine zote kumfanya mtoto wa Mungu na wa Kanisa yaani Familia ya Mungu.

Nani anayeweza kubatizwa?

Yeyote aliyeonyesha imani kwa Mungu na mafundisho ya Kristu na kuandaliwa vizuri.

Sakramenti ya ubatizo inatuondolea nini?

Inatuondolea dhambi ya asili na dhambi zingine zote.

Sakramenti ya ubatizo inatufanya tuwe nini?

Inatufanya viumbe vifya na watoto wa Mungu.

Mtu aliyebatizwa ana sifa zipi?

Sifa kama zake Yesu Kristu mwana wa Mungu: Unyenyekevu, upole, huruma, mkweli, mtiifu, mwema.

Ishara ya Sakramenti ya Ubatizo ni nini?

Ishara kuu ni maji, zingine ni Mafuta ya wakatekumeni, mafuta ya Krisma Takatifu, Kitambaa cheupe, Mshumaa, na Efatha.

Kuna ubatizo wa aina ngapi?

Aina tatu: Ubatizo wa Tamaa—Mtu anayefariki akiwa na shauku la kubatizwa; Ubatizo wa Damu—Mtu anayefariki akiwa katika maandalizi ya Ubatizo; na Ubatizo wa Maji—ambao ndio wa kawaida.

Watoto wadogo wanabatizwa kwa imani ya nani?

Watoto wadogo wanabatizwa kwa imani ya wazazi wao hai na kumilika kisakramenti na kuonyesha nia ya kuwalea watoto wao kama ilivyo sharia ya Kristu na Kanisa lake.

Dhambi ni nini?

Dhambi ni tendo la Mtu kuvunja Amri za Mungu kwa makusudi.

Dhambi ya wazazi wa kwanza ilikuwa nini?

Wazazi wa kwanza Adamu na Hawa walitenda dhambi ya kutotii maagizo ya Mungu wakala tunda la mti waliokatazwa.

Wanaotenda dhambi wataenda wapi?

Wanaotenda dhambi watakosa kumwona Mungu na kuhukumiwa adhabu ya milele jehanamu.

MTIHANI WA KUMUNYO TAKATIFU

Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ni nini?

Ni Sakramenti ya mwili na damu ya Kristu aliye kweli katika maumbo ya mkate na divai.

Lini tunapaswa kupokea Sakramenti ya Ekaristi Takatifu?

Kila tunaposhiriki Misa Takatifu na tukiwa tumejiandaa kwa kutubu dhambi zetu.

Ishara ya Sakramenti ya Ekaristi ni nini?

Ni maumbo ya mkate na divai yanayogeuka kuwa mwili na damu ya Kristu.

Misa ni nini?

Ni sadaka safi ya Wakristu kwa Mungu, ndiyo sadaka ya agano jipya ambamo Kristu kwa njia ya padre, anamtolea Mungu Baba mwili na damu yake katika maumbo ya mkate na divai, kama alivyojitolea mwenyewe juu ya msalaba.

Sakramenti ya Kitubio ni nini?

Ni sakramenti inayomwondolea Mkristu dhambi alizotenda baada ya ubatizo na kumptanisha tena na Mugu na wenzake.

Jinsi gani ya kuungama dhambi?

Namuungamia Mungu mwenyezi, nawe Padre wangu, kwani nimetenda dhambi. Sijaungama tangu… (taja ni lini uliungama mwisho, au ni mara ya kwanza).

Dhambi zangu ndizo hizi … (taja zote unzokumbuka bila kuacha).

Basi Padre wangu, dhambi zangu ni hizi. Naungama na zingine nilizozisahau. Naomba maondoleo na kitubio kama nastahili. Ee Yesu Mwana wa Mungu unihurumie.

Lini tunapaswa kupokea Sakramenti ya Kitubio?

Kila tunapotenda dhambi na kujuta.

Ni Sakramenti zipi zinazotolewa mara moja katika maisha ya mwanadamu?

Ni sakramenti ya Ubatizo, Kipaimara na Daraja Takatifu hizi zinaacha alama isiyofutika.

Msalaba  ni nini?

Ni ishara ya wokovu wetu inayotukumbusha jinsi Yesu Kristu alijitoa auawe kwa ajili ya ukombozi wetu wanadamu.

Kwa nini Yesu akafa msalabani?

Yesu alikufa msalabani ili kwa njia ya sadaka hii Mungu aweze kufuta adhabu aliyostahili mwanadamu kwa sababu ya dhambi ya asili na dhambi zingine.

Yesu alifufuka siku gani?

Yesu alifufuka siku ya kwanza ya Juma ambayo sasa ni Jumapili.

Liturjia ni nini?

Neno liturjia linamaana ya Kazi za watu kwa Mungu. Liturjia ni mpangilio wa ibada za wazi ambazo wakristu wanamtolea Mungu wanapokutana pamoja kama Kanisa.

Shemasi ni nani?

Ni mklero aliyepewa daraja ya tatu ambaye kazi yake kubwa ni kuhubiri Neno la Mungu na kuwahudumia maskini.

Padre ni nani?

Ni kuhani anayeshiriki ukuhani wa kitume wa Kristu ambaye kazi yake ni kuwahudumia watu, kuhubiri Neno la Mungu, kufundisha imani na kuadhimisha Sakramenti.

Askofu ni nani?

Ni kuhani ambaye anashiriki ukamilifu wa ukuhani wa Kristu kama mitume wa Yesu ndiye mwalimu mkuu wa imani.

Baba Mtakatifu au Papa ni nani?

Papa maana yake Baba, ni Askofu wa Roma, na kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani. Yeye ni mwakilishi wa Yesu duniani au Vika.

Walei ni nani?

Ni waamini wote ambao hawajapewa daraja za uklero.

Vipindi vya mwaka wa kanisa ni vingapi? Taja.

Vitano (5): Maajilio—kipindi cha kuandaa kuzaliwa kwa Yesu Kristu

Noeli—Kipindi cha kuzaliwa kwa Bwana wetu Yesu Kristu.

Kwaresma—Kipindi cha Mateso na Kifo cha Bwana wetu Yesu Kristu.

Pasaka—Kipindi cha ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristu.

Kipindi cha Mwaka—Kipindi cha Mafundisho ya Bwana wetu Yesu Kristu

Tunatumia rangi zipi katika mwaka wa liturgia?

Maajilio, Kwaresma, maziko—Zambarau

Noeli, Pasaka, Sherehe—Nyeupe

Jumapili ya Matawi, Ijumaa kuu, Kipaimara, Kumbukumbu ya mashaidi– Nyekundu.

Bikira Maria—Bluu

Maombolezo—Nyeusi

Utaratibu wa kushiriki misa takatifu?

Maandamano kuingia, ibada ya toba, ibada ya neno, kanuni ya imani, sala za waumini, matoleo, mageuzo, ibada ya komunyo, shukrani, maandamano ya kutoka.

Watu wazuri wakifa uenda wapi?

Watarudi mbinguni kwa Mungu na kuishi naye milele.

MTIHANI WA KIPAIMARA

Mitume wa Yesu walikuwa wangapi?

Kumi na wawili:  Petro, Andrea, Yakobo, Yohane, Filipo, Bartholomew, Mathayo, Tomasi, Yakobo mwana wa Alifeo, Simoni aitwaye Zealot, Yuda pia aitwaye Thadayo,  na Yuda Isikariote ,

Sakramenti ya Upako Mtakatifu ni nini?

Ni Sakramenti ya wagonjwa inayowapa nguvu za roho na za mwili, ili kuvumilia mateso na maumivu yao na pia kuwapa matumaini katika uwezo wa Mungu wa kuponya.

Nani anayeweza kupewa Sakramenti ya Upako Mtakatifu?

Muumini yeyote mkatoliki aliyejiandaa kwa kutubu dhambi zake.

Sakramenti ya Kipaimara ni nini?

Ni sakramenti inayompa Mkatoliki Roho Mtakatifu na ukamilifu wa mapaji yake saba, kumfanya Mkristu nkamilifu na kumwandika askari hodari wa Yesu Kristu mpaka kufa.

Ishara ya Sakramenti ya Kipaimara ni nini?

Ni Sala ya Kuwekewa Mikono na kupakwa mafuta Krisma Takatifu.

Taja matunda tisa ya Roho Mtakatifu

1) upendo, 2) furaha, 3) amani, 4)uvumilivu, 5) utu wema, 6) fadhili, 7)uaminifu, 8) upole, 9) kiasi

Taja mapaji saba ya Roho Mtakatifu

1. Hekima 2. Akili 3. Shauuri 4. Nguvu 5. Elimu 6. Ibada 7. Uchaji wa Mungu

Sakramenti ya Daraja Takatifu nini?

Ni Sakramenti inayopewa mkatoliki mwanamme aliyeteuliwa na kuandaliwa ili kushiriki utume wa Kristu kuhani ndani ya Kanisa.

Nani anayetoa Sakramenti ya Daraja      Takatifu?

Askofu au Askofu Mkuu

Sakramenti ya Ndoa Takatifu ni nini?

Ni Sakramenti inayowaunganisha wakristu wawili mwanamme na mwanamke kwa upendo na hiari, na kuwapa neema ya kuishi pamoja kama mme na mke, kuza na kulea watoto kama familia.

Sakramenti ya Ndoa ni Kati ya nani na nani?

Mwanamme mmoja na mwanamke mmoja

Kwani nini ndoa ya Kikristu haina talaka?

Kwa sababu ni agano la milele lililounganishwa na Mungu.

Toharani ni nini?

Ni mahali ambapo roho za waumini ambao walikuwa na deni ya dhambi utakaswa kabla ya kuingia katika uzima wa milele.

Biblia ni nini?

Ni mkusanyiko wa vitabu mbalimbali vinavyosimulia historia ya wokovu wa mwanadamu

Nani aliyeandika Biblia?

Biblia iliandikwa na watu mbalimbali walioangaziwa na roho wa Mungu.

Rosari Takatifu ni nini?

Ni sala maalumu iliyotolewa na Bikira Maria kwa Kanisa kupitia Mt. Dominiko Karne ya 13, na inayoadhimisha matendo 20 ya maisha, utume, mateso na ufufukowa Bwana wetu Yesu Kristu.

UJE ROHO MTAKATIFU

Uje Roho Mtakatifu/ uzienee nyoyo za waumini wako/ peleka roho wako/ vitaumbwa vipya na nchi zitageuka.

Tuombe: Ee Mungu uliyefundisha nyoyo za waumini wako/ kwa kuwaletea mwanga wa Roho Mtakatifu/ tunakuomba utuongoze na yule Roho/ tupende yalio mema/ na tupate daima faraja  zake/ Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu. Amina

TUNAUKIMBILIA

Tunaukimbilia ulinzi wako mzazi Mtakatifu wa Mungu/ usitunyime tukiomba katika shida zetu/ utuokoe kila tuingiapo hatarini/ Ee Bikira Mtukufu mwenya baraka/ Amina.

Get in touch

Diane is always available for side collaborations and talks worldwide. If you want to chat about design, books, wine, or anything else, don’t hesitate in reaching out.

Writing

Lessons from remote interviewing
April 2020

What design mentees need
December 2019

How to foster collaboration
November 2019

Blog at WordPress.com.

Up ↑

%d bloggers like this: