Masomo ya Jumapili kwa kifupi 14 B


Ezekieli 2:2-5; Zaburi 123; 2 Wakorintho 12:7-10; Marko 6:1-6


Kukataliwa
Je, umewahi kukutana na kukataliwa au maishani mwako? Je, umewahi kufika mahali ambapo wakazi hawakukukaribisha? Hisia za kukataliwa zinaweza kuwa mbaya sana, hasa unapokataliwa bila kutarajia. Kuna sababu nyingi zinazowafanya watu kuwakataa wengine. Wakati mwingine tunakataliwa kwa sababu ya tabia au kauli zetu mbaya au tabia na kauli za wale wanaotukataa. Ubaguzi wa rangi, ubepari wa kitamaduni, dhana ya kuwa bora kuliko wengine, msimamo wa kisiasa au maadili, imani, n.k., hufanya watu wawakatae wengine. Hata hivyo, haimaanishi kwamba kila mtu anayekataliwa ni mbaya. Yesu mwenyewe alikataliwa.

Katika somo la kwanza, tunasikia jinsi Mungu alivyomwita na kumtuma nabii Ezekieli kwa watu waliokuwa wamevunja agano lake. Watu wa Israeli walikuwa wamefanya agano na Mungu lakini mara nyingi, walimuonyesha mgongo na hata kuwaua manabii ambao aliwatuma kuwarejesha katika agano (Yer 37:11-16). Mungu anamwagiza Ezekieli azungumze na watu kwa niaba yake akitumaini kwamba watamsikiliza na kubadilisha njia zao. Ikiwa hawatabadilika, wakati wa mahesabu utakapofika, angalau watakuwa wanajua kwamba kulikuwa na nabii kati yao. Wasije wakasema “hatukuambiwa”.

Katika Injili ya leo, Yesu anakutana na kukataliwa sawa sawa na manabii waliomtangulia. Mbaya zaidi watu wa nyumbani kwake wenyewe walimkataa. Watu hawa walifikiri kwamba walimjua Yesu na kwa sababu hii, walimpuuza ingawa maneno na ishara zake zilionyesha wazi kwamba hakuwa mhubiri wa kawaida au kama mafarisayo wa wakati wake. Siku hizo, kazi ya useremala ambayo Yesu alifanya ilikuwa inachukuliwa kama kazi ya tabaka la chini. Familia ya Yesu pia haikuwa miongoni mwa familia zilizoelimika na tajiri za Nazareti. Baba yake Yesu hakuwa mtu maarufu wala nabii bali mtu wa kawaida.

Katika jamii yetu leo, tunashuhudia aina hii ya kukataliwa. Viongozi wazuri wanakataliwa na umma kwa sababu ya asili yao ya unyenyekevu au familia zao zizizokuwa maarufu. Jamii leo ingependa kuwa na viongozi kutoka kwenye familia za kifalme au tajiri hata kama ni mafisadi na hawatendi kazi zao, kuliko watu kutoka tabaka la chini au maskini hata kama ni waaminifu, wenye heshima, na wanaofanya kazi kwa bidii.

Katika Kanisa pia tunakutana na changamoto hizo. Watu uenda mbali wakitafuta miujiza ili kuponywa na magonjwa na shida mbalimbali au kupata utajiri, huku wakiacha nyumbani manabii wa kweli wanaojua chanzo halisi cha matatizo yao. Manabii wa henzi zetu pia uenda umbali mrefu kuuza miujiza kwa watu wasiojua wanaotaka mafanikio bila kutoa jasho. Kila Jumapili, makuhani katika parokia zetu utulisha kwa Neno la Mungu na Ekaristi lakini hatushibi wala kufaidi kwa sababu mara baada ya ibada tunakimbilia sehemu za miujiza.

Mtakatifu Paulo, alikutana na kukataliwa na changamoto nyingine katika utume wake. Hata hivyo, alipata faraja katika neema ya Mungu. Badala ya kulalamika juu ya changamoto za utume, aliziona kama mwiba mwilini mwake uliomsaidia asijisifu juu ya mafanikio yake bali badala yake, kutumaini katika neema ya Mungu. Paulo alitambua kwamba alichohitaji si dhamana ya mafanikio katika utume wake bali hakikisho la neema ya Mungu pamoja naye. Mama Teresa wa Kalkuta aliwahi kumwambia Mwandishi mmoja wa habari, “Mungu hahitaji mafanikio bali uaminifu”.

Wapendwa, hebu tuchunguze kwa makini imani yetu na kuona kama sisi ni wafuasi wa kweli wa Yesu au tumemkataa na kuwakimbilia manabii wanaotuambia kile tunachotaka kusikia. Tena, tujue leo kwamba Mungu hajatuita tutafute ukuu bali tuamini katika neema yake, ambayo inatosha katika hali zetu zote.

Jumapili njema.

Fr. Lawrence Muthee, SVD

Leave a comment