Masomo ya Jumapili kwa ufupi Pasaka 6 B

Matendo ya Mitume 10:25-48; Zaburi 98; 1 Yohana 4:7-10; Yohana 15:9-17

Lugha Ambayo Kila Mtu Uelewa ni Upendo

Wapendwa, leo ni Jumapili ya sita ya Pasaka na Jumapili ijayo itakuwa sherehe ya Kupaa kwa Bwana wetu. Hivi karibuni kipindi cha Pasaka kitamalizika. Natumaini kwamba umepata faida ya kutosha kutoka kwa kipindi hiki cha liturujia. Katika wiki mbili zilizopita, tumekuwa tukisoma masomo kuhusu upendo, haswa kutoka kwa Injili na barua za Mtakatifu Yohane. Yesu ameelezea kwa kina kwamba hakuna njia nyingine ya kushikamana naye isipokuwa ile ya kumpenda Mungu na Jirani.

Upendo ni kitu cha thamani sana ambacho kila mtu angependa kuwa kiasi kikubwa iwezekanavyo. Changamoto tuliyo nayo sote ni kwamba tunasingizia mambo mengi kuwa ni upendo. Yesu hataki tuwe na mkanganyiko kuhusu upendo anaouzungumzia. Anatupa mfano wa upendo ambao Baba anao kwake na ule ambao yeye mwenyewe anao kwetu. Aina ya upendo ambao unajitolea kila kitu kwa ajili mpendwa. Kwa bahati mbaya, watu wengi wamejikuta katika mateso mengi kwa kusingiziwa upendo. Mfano mzuri ni wa wanandoa wengi ambao walidhani kwamba baina yao ilikuwa upendo uliowapeleka hata kufunga ndoa. Lakini sasa maisha wanayoishi hayana hata chembe ndogo ya upendo, bali dhiki tupu na utumwa. Vijana wengi wamechanganya hisia za mahusiano ya kimapenzi ambayo ni ya kawaida katika umri wao kuwa ni upendo. Baada ya msichana kupata ujauzito, mvulana anamuacha na kwenda kutafuta mwingine. Ndoto za yule msichana zinavurugika na ujauzito usiokusudiwa. Hawana mtu wa kutembea nao na kuwashauri wakati huu muhimu katika ukuaji wao.

Mtakatifu Petro katika somo la kwanza anakiri kugundua, kwamba upendo wa Mungu haubagui mtu, au kwa maneno mengine, Habari Njema ya upendo ambao Yesu alileta kwetu haina mipaka yoyote. Anasema, “Nimegundua kweli kwamba Mungu hana upendeleo, lakini yeyote wa taifa lolote anayemcha Mungu na kutenda yaliyo mema anakubaliwa naye” (Matendo 10:34-35). Wayahudi waliamini kwamba Masiha alikuwa wao pekee. Hii ndiyo sababu walichukizwa na kumkataa Yesu kama Masiha kwa sababu alishirikiana na watu wa mataifa (wasio Wayahudi).

Katika siku za mwanzo mwazo za upadri wangu, niliwahi kubahatika kufanya kazi katika shule moja ya sekondari ya wasichana (A-Level) kama mshauri wa Kiroho. Kwanza, nilianza na Wanafunzi Wakatoliki tu lakini baadae wanafunzi kutoka madhehebu mengine ya Kikristo na hata dini zingine walianza kuhudhuria. Baadaye Utawala wa Shule uliniomba niwe mshauri wa wasichana wote. Nilikuwa na vikao pamoja kwa wote siku ya Jumatano na vikao binafsi siku ya Ijumaa. Jumapili, nilikuwa na Misa kwa wanafunzi Wakatoliki, lakini wanafunzi wengine pia walihudhuria. Hii ilinilazimu kuwa makini sana kutofanya au kunena lolote ambalo lingemfanya hata mmoja wao ajisikie kubaguliwa. Nilifurahia sana Jumuiya hii ya wote tuliyoiunda katika roho moja na upendo mmoja. Nilijifunza kwamba Injili ambayo Yesu alituwachia sio ya Wakristo peke yao bali ni ujumbe ambao lazima uwakusanye wanadamu wote kwa Baba mmoja wala si kuwagawanywa. Leo wengi wao ni wadada waliokomaa katika fadhila wanaofanya wanaochangia mazuri katika jamii. Baadhi yao wanasoma tafakari hii, na nina hakika wanatabasamu kusoma ushuhuda huu.

Ninaweza kukiri kwamba nafasi hii iliangazia sana uelewa wangu wa Injili kwa njia ambayo sikupata kukutana nayo katika miaka yangu kumi na miwili seminari. Kusikiliza historia zao, mapambano, na hofu zao, niligundua kwamba changamoto nyingi ambazo watu hupitia hasa vijana, zimefungamana sana na historia yao, kwa maana ya jamii na mazingira walikolelewa na imani walizozirithi kwa wazazi au walezi wao. Kama hili halijaeleweka kwanza, ushauri wowote, uwe ni wa kisaikolojia au kiroho hautakuwa na msaada kwao. Elimu hii ilinifanya nirudi kufanya utafiti kuhusu madhehebu mengine ya Kikristo pamoja na dini zingine. Kwa ufupi, niligundua kwamba nilikuwa na msaada zaidi kwa wasichana nilipoweza kuhusiana vizuri na historia zao za kiimani na makuzi yao bila kuwahukumu. Bila shaka, wengi wao hawakuwa wamechagua kuwa wa dhehebu au dini hii au ile, ilikuwa ni kitu walichorithi kutoka familia walikozaliwa na kulelewa.

Vita kati ya dini na madhehebu yao tofauti vimekuwa vikiendelea kwa muda mrefu sasa sehemu nyingi duniani. Hata ndani ya Makanisa ya Kikristo, kuna ushindani mbaya sana kuhusu ibada au liturujia ipi ni bora kuliko nyingine. Mara nyingi baadhi ya wahubiri ututumia muda na nguvu nyingi kusuta na kudharau madhehebu mengine badala ya kuhubiri upendo wa Mungu. Hii ndio tunaweza kusema ni “ubatili wa kiroho” na unasababisha kutoelewana kati ya watu wa dini na madhehebu tofauti. Imani ya mwanadamu kwa maoni yangu inadhibiti zaidi ya theluthi tatu ya jinsi mtu anavyoelewa ulimwengu – mtazamo wake wa ulimwengu na mtazamo wake kwa wengine. Imani ni zaidi ya kuwa mwanachama wa dhehebu hili au lile. Imani ni sehemu ya utamaduni wa msingi sana wa binadamu. Imani yangu uchangia jinsi ninavyotafsiri maisha, mazingira, na watu wanaonizunguka. Lakini, kama Mtakatifu Yosefu Freinademetz alivyosema, “lugha pekee ambayo kila mtu uelewa ni upendo”. Ujumbe wa Kikristo unaweza kufupishwa kama upendo kwa Mungu na jirani licha ya kile jirani anachoamini

Ndugu zangu, tuna mengi ya kujifunza kuhusu upendo ambao Yesu anatuomba tupendane. Upendo ambao unajumuisha vipengele vyote vya maisha yetu. Upendo kwa Mungu na jirani haumtengi au kumfungia nje mtu yeyote au kikundi chochote cha watu kwa sababu ya imani zao au wanakotoka. Ni kupenda kama Mungu anavyotupenda kupitia Yesu Kristo. Sisi sote, weupe, weusi, Wakristo, Waislamu, nk., tuna damu ya rangi moja tu katika mishipa yetu. Mtakatifu Yohane anatuambia kwamba “Upendo unatoka kwa Mungu na kila mtu anayependa amezaliwa na Mungu na hakika anamjua Mungu” (1 Yoh 4:7-10). Je, umewahi kuwa na hisia za kibagusi au kauli hasi dhidi ya watu wa dini au dhehebu lingine?

Wapendwa, mwaliko wangu leo ni kutathmini jinsi tunavyowatendea wengine na kuona kama tunambagua mtu yeyote. Ikiwa ndiyo basi upendo wetu si wa Mungu, ni upendo wetu tu tuliouchonga wenyewe kwa masilahi yetu. Ikiwa tunataka upendo wetu uwe na maana kama ule wa Mungu katika Kristo Yesu, basi lazima tupende kama Mungu anavyopenda.

Jumapili njema.

Padre Lawrence Muthee, SVD

Leave a comment