JUMAPILI YA 4 MWAKA C

 

faithgodreachingjpg.jpg

Somo I: Jeremia 1:4-5, 17-19;  Wimbo wa Katikati:   Zaburi 71:1-2, 3-4, 5-6, 15-17; Somo 2: Wakorintho 12:31-13:13 or 13:4-13;  Injili: Luka 4:21-30

Upendo wa Kweli ni upi?

Tumsifu Yesu Kristo. Katika Somo la Kwanza kutoka kitabu cha Nabii Yeremia 1:4-5,17-19, tunasikia jinsi Yeremia aliogopa kupokea kazi ya unabii kwa sababu alijua ugumu wa mioyo ya watu wa wakati wake. Mungu anamwambia kwamba alimuandaa kwa ajili hiyo tangu tumboni mwa mama yake. Atampigania ili asishindwe katika wito wake. Wito wa Yeremia ni mfano wa wito wetu sisi wote tuliobatizwa katika Kristo. Kwanza tumeitwa kama wanadamu viumbe walio juu zaidi ya viumbe wengine wote, na pili kama watoto wa Mungu kwa njia ya Ubatizo.

Kila mwanadamu ameumbwa kwa upendo wa Mungu. Haijalishi mazingira alipozaliwa kwa maana hayo yanategemea hali za kibinadamu. Jambo la muhimu ni kwamba kila mwanadamu ameumbwa na Mungu. Mungu alikuwa na uwezo wa kuumba kila mtu pasipo uwezo wa binadamu, lakini katika hekima yake, aliwaachia wanadamu kazi ya kuujaza ulimwengu. Aliwapa wanadamu uwezo na akili ya kushiriki katika kazi yake ya kuumba.

Somo hili linaangazia jambo muhimu sana katika maisha ya mwanadamu. Kwamba kila mtu aliyetungwa mimba ana kibali cha kuishi kutoka kwa Mungu na pia Mungu ana mpango naye. Haijalishi kama wazazi walikusudia kumzaa au la. Hii ina maana kwamba wazazi wanapaswa kuwampa nafasi wale viumbe kuzaliwa na kuishi ili watimize sababu yao duniani. Hamna mtu aliye na mamlaka ya kuamua kama mwanadamu yeyote, katika hali yeyote anapaswa kuishi au kutoishi.

Hakuna hata mmoja anayezaliwa kwa bahati mbaya. Kila mmoja wetu amekusudiwa na Mungu kwa ajili ya kazi fulani. Hii ndiyo maana sisi wote ni tofauti wala hakuna anayefanan ana mwingine.

Neno hili linatuita kudhamini maisha ya kila mtu katika hali zote, awe mchanga au mzee, awe na afya au mgonjwa, awe na tajiri au maskini, awe mkristo au si mkristo.

Machoni pa Mungu sisi wote ni sawa. Hili ni muhimu liweleweke na lifundishwe kwa watu wote kwamba hatuna sababu yoyote ya kumbagua mtu yeyote. Kile tunapaswa kubagua ni maovu, chuki, vita, mashindano yasio na tija na kiburi mbele ya wengine.

Haya tuyabague kweli kweli. Hamna anayechagua azaliwe wapi. Ni vizuri kutambua neema ya Mungu na kumshukuru kwa kuwa na amani na uhuru wa kuabudu.

Wito wa imani yetu katika Kristo ni kufaana kama ndugu wa baba mmoja na warithi pamoja na Yesu mwenyewe.

Tunaitwa kupendana kwa upendo wa kimungu. Siku hizi upendo una sura nyingi sana tofauti na upendo wa kweli wa kimungu.

Paulo leo katika waraka wake kwa Wakorintho 12: 31; 13:1-13, anatufundisha nini haswa upendo wa kweli ni nini. Kuna mambo mengi tuliyozoea kuita upendo mengine ukiyatafakari yanashangaza kweli kweli.

Walio wengi kwa kusingizia upendo wamejitenga na Mungu na kanisa. Kanisa kwao ni kikwazo cha kupenda. Hili kweli ni la ajabu. Kanisa ni mwili wa Kristo na Ujumbe mkubwa zaidi ambao kanisa linatangaza ni ule wa Upendo wa kweli.

Utasikia wakisema, ananipenda kwa sababu ameninunulia lunch, amenitoa mtoko, ameninunulia simu nzuri, nguo, amenipa hela, nk. Lakini tangu hayo yote yaanze nimeshindwa kwenda kanisani na hata Ekaristi takatifu niliacha kupokea.

Huu hauwezi kuwa upendo jamani, ni mambo yetu tu yanayopita tu ambayo yanapaswa kutambulikana kwa neno lingine mbali na upendo. Ukitaka kujua kama kweli ulikuwa upendo subiri mpaka mmoja apate matatizo. Bahati mbaya ni kwamba wengi wanajikuta mahali pabaya baada ya mambo haya waliodhania kuwa upendo yanapokwisha.

Ebu tutafakari anachokisema Paulo kuhusu UPENDO kama karama iliyo kuu zaidi ya nyingine zote:

Upendo wa kweli unapita ujanja wote wa lugha (mtu anapigwa maneno matamu anachanganyikiwa baadaye anatapeliwa kiroho, kiakili, kihisia, kimwili na kivyote, anabaki maskini wa kutupwa kwa hali zote, kisa na maana amependwa).

Upendo wa kweli unapita unabii wote (wengine utasikia wakiambiana kwamba nimeonyeshwa kwamba wewe ndiwe umeumbwa kwa ajili yangu, Mungu ameniambia kwamba nikuoe, tapeli kwa jina la Mungu).

Upendo wa Kweli unapita ukarimu wa mali (kununuliwa zawadi mbali mbali na kupelekwa kwa mwezi na kwa jua haimanishi mtu anakupenda).

Upendo wa Kweli unapita sadaka za kimwili (watu wapo radhi kufanya mambo yote kupata walichonuia. Hii haimanishi upendo, subiri mpaka apate alichonuia. Utaachwa kwenye mataa.

Kanisani na sehemu za kusali ni mahali pa kutangaza upendo wa Mungu unayesamehe kila kitu sio mahali pa kutapeli watu kwa kutangaza ghadhabu ya Mungu. Mungu ametupa akili uhuru wa kuchagua yaliyo mema tupate baraka. Chaguo ni la kila mtu. Yesu anaposema tuwapende adui zetu, anataka kwa njia ya upendo wetu waweze kubadilika.

Wengine wanawaombea adui zao wapigwe na radi, wengine hata wenzao wa ndoa na watoto wao. Yesu alitufundisha kusamehe hata wakati inaonekana vigumu. Wasamehe kwa sababu hawajui walitendalo (Lk 23:34).

Paulo anasema kwamba upendo wa kweli:

  • Huvumilia – katika hali zote, katika raha na katika shida. Upendo unachukuwa muda kukua na kukomaa. Hauna pupa. Watu wanakutana mjini na baada ya miezi miwili wanaishi pamoja, baada ya miezi mitatu wana mtoto, wengine kabla ya mtoto kuzaliwa wameachana na kuingia katika mahusiano mengine na mengine.
  • Ufadhili – maana yake husaidia. Kama kweli mtu anapenda yupo radhi kumsaidia anayempenda kufikia malengo yake wala sio kummiliki na kumnyima uhuru wake wote.
  • Hauhusudu – maana yake hauoni wivu au kijicho. Mtu anasema anapenda lakini hataki maendeleo ya anayempenda. Tangu apendwe ameacha shule, kazi, nk.
  • Hautakabari wala kujivuna – maana yake hauna kiburi na dharau kwa wengine. Upendo daima unanyenyekea katika yote. Unadhamini anayependwa kuliko nafsi.
  • Una adabu – mtu anasema anapenda lakini haheshimu anayempenda. Haheshimu ndoto zake au utu wake. Anataka tu kumtumia. Huo sio upendo ni ubinafsi.
  • Hautafuti mambo yake – mtu anayependa hatafuti masilahi yake kwanza. Utamsikia mtu akimwambia mwingine wewe usisome njoo ukae kwangu huku moyoni anasema uwe mpishi wangu, dobi wangu, chombo changu cha kujifurahisha na nk.
  • Hauoni uchungu – upendo daima upokea yote kutoka kwa apendwaye wala haukwaziki kwa mapungufu ya anayependwa. Katika ndoa hili ni muhimu sana.
  • Hauhesabu maovu – utamsikia akisema sasa mara ya ngapi nimekuonya. Hii ni mara ya mwisho. Au mwingine anabeba mambo ya miaka na mikaka moyoni na kukumbuka mara kwa mara. Chakula kikiungua au mwenzake akichelewa.
  • Haufurahii udhalimu – daima upendo utafuta haki kwa kila mtu na katika mambo yote. Ausitawi katika unyanyasaji.
  • Haupungui – hili hata linashangaza, ukiwauliza watu wengi wanaoishi pamoja wakumbuke na kulinganisha siku za kwanza walipoanza mahusiano na wanavyoishi sasa, wengi watatokwa na machozi. Wengine watadiriki kusema kwamba wanachokiishi sasa sio upendo ni kuvumiliana tu kwa sababu hamna namna nyingine. Wangekuwa na namna hawangekuwepo pale. Wengine wanafikia mwisho na kutengana au kutamani kufa. Hii ndiyo hali halisi katika jamii yetu.

Nitadhubutu hata kusema kwamba kunao ambao wanaishi unyumba lakini hawajawahi kuonja upendo wa kweli kwa sababu haukuwepo tangu mwanzo. Kilichowaleta pamoja hakikuwa upendo.

Lakini kuna habari njema: Yesu alikuja kwa ajili ya kukarabati udhaifu wetu katika katika upendo. Katika kipindi hiki cha kawaida cha mwaka wa Kanisa, tunasikiliza mambo ambayo Yesu aliyasema na kuyatenda ili kutufundisha kupenda kama Mungu anavyotupenda.

Yesu anakuja kuondoa unafiki na ulagai ambao umekuwa ukisambazwa kwa jina la upendo. Jumapili tulimsikia akitangaza manifestó yake. Kuwahubiri maskini habari njema, wafungwa kufunguliwa, vipofu kuona na uhuru kwa waliosetwa.

Hili liliwapa faraja wale wote waliokuwa wanateswa lakini liliwatia hofu na chuki waliokuwa wanaendeleza udhalimu na utapeli katika jamii ile. Wanakasirika kiasi cha kutaka kumuua kwa kuchomwa roho zao. Wanamtoa nje ili wamtupe kwenye kilima.

Watu kama Yesu wapo wengi duniani. Jana tumesherehekea siku kuu ya kutolewa Yesu Hekaluni ambayo pia ni sherehe ya watawa kote ulimwenguni. Kunao wanajitolea maisha yao yote kuboresha hali ya maskini katika jamii lakini wanakumbana na upinzani mkubwa kiasi hata cha kupoteza maisha.

Neno la Mungu linachoma, tena ni kali kama upanga wenye ncha mbili, unakata huku na huku. Hamna mahali pakuushika na kuubana usikate, unakata kotekote (Wae 4:12). Neno la Mungu halisitiriki au kubanwa. Linaingia na kuchangamotisha kwa lengo la kubadirisha kilicho kinyume na mapenzi ya Mungu. Ni kama mvua ambayo ikianguka hairudi bila kuotesha mimea (Isa 55:10-11).

Ndugu zangu. Sisi tumepokea neema ya kuwa wana wa Ufalme wa Mungu. Tulisikilize neno la Mungu na kulipa nafasi kubadirisha maisha yetu. Tukifanya hivi, hakika tutakuwa na uhai wa kweli hapa duniani na maisha ya milele mbinguni.

Tupendane sisi kwa sisi. Tuwapende wanaotuchukia kwani vita vya chuki havishindwi kwa kurudisha chuki bali kwa kupenda. Chuki na chuki uleta kuvunjika kwa jamii na maafa.

Mungu awabariki.

Fr. Lawrence Muthee, SVD

 

 

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Blog at WordPress.com.

Up ↑

%d bloggers like this: