
Kutoka 20:1-17; Zaburi 18(19); 1 Wakorintho 1:22-25; Yohana 2:13-25
Maneno Kumi ya Uhai
Wapendwa, leo ni Jumapili ya Tatu ya Kwaresima. Tunazo wiki tatu zaidi kumaliza mazingatio ya Kwaresima na kusherehekea Pasaka. Je! Umewahi kutumia mkongojo au fimbo ya kutembelea au kuona mtu akitumia? Mkongojo hutumiwa na wale ambao kwa sababu fulani kwa miguu yao hawawezi kubeba uzito wa miili yao na kutembea vizuri. Fimbo huwasaidia kutumia mikono na mabega yao kuweza kuongeza nguvu ya miguu yao.
Katika somo la kwanza la leo, tunasikia kuhusu Amri Kumi zinazojulikana pia kama Torati. Mungu aliwapa watu wa Israeli maneno haya kumi chini ya mlima Sioni ili kuwasaidia kuishi kulingana na mapenzi yake, hii ni mara ya pili Mungu anawapa wanadamu maagizo. Ya kwanza yalitolewa kwa Adamu na Hawa katika bustani ya Edeni kuhusu mti wa uzima, “Mnaeza kula matunda ya miti yote ya bustani, isipokuwa mti wa ujuzi wa mema na mabaya. msile matunda yake; siku mtakapokula mtakufa hakika” (Mwanzo 2:16-17). Kwa kutozingatia amri za Bwana, dunia ililaaniwa, na maisha ya binadamu yakabadilika daima. Mwanamume na mwanamke hawakuweza tena kutenda mema kwa hiari yao wenyewe. Mungu aliwapa Amri Kumi ili kuonya dhamiri zao ili kuchagua mema na kuepuka mabaya. Amri za Mungu sio mzigo bali ni msaada kwetu katika safari yetu ya haki, ni kama fimbo kwa maisha yetu yaliyovunjika.
Amri Kumi zimegawanywa katika sehemu mbili kuu. Tatu za kwanza hutusaidia kudumisha uhusiano mzuri na Mungu na zingine saba zinatusaidia kuwa na uhusiano mzuri na watu wengine. Zote zinaunganishwa na hatuwezi kuvunja moja bila kuvunja zingine. Amri ya kwanza inazungumzia uwepo wa Mungu mwenyewe. Vitu vyote vinavyotuondolea hofu na utii kwa Mungu vinaweza kuitwa “miungu mingine.” Kila kitu kilicho duniani kimeumbwa na Mungu na hakiwezi kuchukua nafasi ya Mungu. Kutumia jina la Bwana bure ni kutumia jina la Mungu kutetea aina yoyote ya uovu na ubinafsi. Siku kuu ya Mungu ni siku ya kukumbuka kwamba Mungu ndiye muumba na mwanadamu ni kiumbe dhaifu ambaye bila Mungu hawezi kufanya chochote. Ni siku iliyotengwa kumheshimu na kumuabudu muumba wetu na kukumbuka kwamba yote yanatoka kwake. Yote yanayotuzuia kumwabudu Bwana Jumapili huwa sanamu kwetu.
Amri ya nne inaweka wazazi wetu nafasi ya pili baada ya Mungu na ndiyo pekee yenye ahadi kwa wale wanaoishika. Ile ya tano inatukumbusha kwamba kwa sababu sisi sio waumbaji wa uhai, vilevile hatuna mamlaka ya kutoa uamuzi wa kukomesha maisha ya mtu yeyote kwa sababu yoyote ile, ikiwa ni pamoja na wale ambao bado hawajazaliwa ndani ya tumbo la mama. Tamaa binafsi hufanya watu kuchukua maisha ya wengine kwa sababu wana nguvu na uwezo wa kufanya hivyo. Wanasahau kwamba wao pia siku moja watakufa na kusimama mbele ya hukumu. Sio halali kufanya uzinzi na mtu asiye mke au mume wako, usichukue kitu ambacho sio chako, acha kuwa mvivu fanya kazi kujitafutia riziki yako. Acha kusema uwongo kwa sababu unadhuru wengine. Watu wengi wanateseka kwa sababu ya uwongo tunasema au kuambiwa. Uwongo unavunja mahusiano. Wengi wanatumikia hukumu gerezani kwa makosa ambayo hawakufanya. Mungu alituamuru kufanya kazi na sio kuwa wavivu. Usitamani mali ya mtu mwingine ikiwa ni pamoja na mwenzi wake, tafuta yako mwenyewe.
Vema, haya ni rahisi kusemwa kuliko kutekelezwa. Hata hivyo, kwa malezi sahihi ya dhamiri yetu na kiasi cha kutosha cha nidhamu, kushika amri kunaweza kuwa sehemu ya maisha yetu. Hata hivyo, wengi wameongeza amri ya kumi na moja, ambayo tafsiri yake inasema, “Usikamatwe.” Hii tunaishika kwa uaminifu mkubwa. Je! amri za Mungu zina maana gani kwangu?
Mzaburi anatuambia kwamba sheria ya Bwana ni safi na yenye busara. Ikiwa tunafuata sheria ya Bwana, tutapata furaha na maisha mazuri. Maisha mtu aliyejitenga na Mungu yanaweza kuonekana mazuri kutoka nje lakini kwa ndani, hayana furaha ya kweli na ya kudumu.
Kwa vizazi vingi, Mungu alitumia manabii na viongozi kuwasaidia watu kubaki waaminifu katika amri zake. Wakati watu walipotii, kulikuwa na furaha na mafanikio. Walipokaidi, kulikuwa na mateso na kifo. Katika siku hizo, wengi waliteseka kwa sababu ya maamuzi yaliyofanywa na wengine. Watoto waliadhibiwa kwa dhambi za wazazi wao, na raia waliteseka kwa sababu ya maamuzi ya wafalme wao. Hatimaye, Mungu alimtuma Mwanawe Yesu kutuokoa kutoka kwa hali hii. Yesu akawa kilele cha sheria, na sasa tunachotakiwa kufanya ni kumwamini na kuishi kulingana na mafundisho yake. Wayahudi walitaka daima kumfanya Mungu kuonekana kuwa mbali na watu ili kupata kisingizio cha kutotii amri zake. Hii ndiyo wengi wanayopenda leo pia. Ndio maana ilikuwa kikwazo kwao kwamba Mungu alifanyika mwanadamu. Watu wa Mataifa ambao hawakuwa na imani kwa Mungu lakini walitegemea falsafa yao waliichukulia wazo la Mungu kuwa mwanadamu kama lisilofikirika na upumbavu mtupu. Hata hivyo, kwetu sisi ambao tumepata wokovu kupitia Kristo, tunajua kwamba Mungu amefanya makao pamoja nasi. Tunaweza kumkaribia wakati wowote tunapotaka. Lile tunalopaswa kufanya ni kujitahidi kuwa wema kama yeye alivyo mwema.
Leo wengi wa Wakristo hawaendi kanisani kwa sababu tofauti tofauti. Moja ya sababu kubwa ni kwamba hawajui maana ya kwenda kanisani. Baadhi wanafikiri kwamba kwenda kanisani ni jambo tunalofanya ili kuonekana vizuri katika jamii. Hata hivyo, tangu kwenda masokoni, maduka makubwa, na kutangamana na marafiki inatuonekana kuwa jambo la kisasa zaidi, mambo haya yamechukua nafasi ya kwenda kanisani. Wengine wanafikiri kwamba Kanisa ni mahali pa miujiza ya kuwa matajiri na kupata mafanikio ya haraka. Lakini pia, kuna njia nyingine nyingi za kupata utajiri na mafanikio ya haraka, kwa nini kujibkujitesa kwenda kanisani. Wengine wako kanisani leo si kwa sababu ni waumini wazuri bali kwa sababu ni biashara nzuri. usishangae leo tuna makanisa yaliyomilikiwa na watu binafsi. Ndio maana nafasi za uongozi kanisani zimekuwa za kisiasa na kampeni kubwa hufanyika kuzigombania. Baadhi wamekataa kuondoka katika nafasi hizo kwa sababu ikiwa watafanya hivyo, wanaadhirika kibiashara. Kwa nini ninaenda kanisani? Au kwa nini siendi kanisani?
Wapendwa, Yesu aliwafurusha wafanyabiashara kutoka hekaluni kama ishara kwamba nyumba ya Mungu lazima ibaki takatifu. Hekalu kuu la Bwana ni maisha yetu wenyewe, na leo tunaitwa kuyafurusha mambo yasiofaa kutoka katika maisha yetu kama vile vitendo, mawazo na maneno yanayochafua hekalu hili. Je, mwili wangu ni hekalu la Bwana?
Jumapili njema.
Pd. Lawrence Muthee, SVD
