Kumbukumbu la Torati 4:32-34, 39-40; Zaburi 33; Warumi 8:14-17; Mathayo 28:16-20
Udhihirisho wa Utatu Mtakatifu

Wapendwa, leo ni Sikukuu ya Utatu Mtakatifu, ambayo hufanyika Jumapili baada ya Pentekoste. Jumapili ijayo itakuwa sikukuu ya Corpus Christi (Mwili na Damu ya Kristo). Neno Utatu kutoka kwa Kilatini “Trinitas” linamaanisha tatu. Kama Wakristo, kupitia ufunuo katika Maandiko Matakatifu, tunamwona Mungu katika madhihirisho matatu, Mungu Baba, Mungu Mwana, na Mungu Roho Mtakatifu. Fumbo la Utatu Mtakatifu ni la kwanza kati ya mafumbo manne makuu yanayounda msingi wa imani ya Kikatoliki. Mengine ni Fumbo la Umwilisho (Noeli), Fumbo la Pasaka, na Fumbo la Ekaristi Takatifu. Fumbo linaeleweka katika imani ya Kikatoliki kama ukweli wa wokovu ambao hauwezi kueleweka kikamilifu kwa akili ya mwanadamu.
Katika somo la kwanza la leo, katika maneno yake ya kuaga, Musa anakumbusha watu wa Israeli jinsi Mungu alivyojidhihirisha kwao kwa njia ambazo hazijasikika katika taifa lingine lolote. Kwamba Mungu amesema na watu wake na walinusurika ili kusimulia (iliaminika kwamba mtu akinena au kumwona Mungu angekufa mara ile ile). Kwamba Mungu amejichagulia taifa kwa ajili yake na kuishi miongoni mwao akifanya maajabu na kupigana kwa niaba yao. Anawasisitiza pia kwamba Bwana Mungu ni mmoja tu na njia ya kupata neema yake ni kwa kuzishika amri zake.
Mtume Paulo anamrejelea Roho Mtakatifu kama yule anayetuongoza kuwa wana wa Mungu. Anatuwezesha kuamini na kukiri imani yetu kwa Mungu na Kristo wake, ambaye kwa njia yake tunakuwa warithi kwa kufanywa wana. Roho Mtakatifu “anaabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana”. Yeye si chombo cha miujiza au laana kama wanavyofikiri manabii wa siku hizi. Wanachotumia ni “roho mtakakitu” na si Roho Mtakatifu.
Katika Injili, tunakutana na Bwana aliyefufuka ambaye, baada ya kufungua akili za wanafunzi wake kuelewa maandiko, anawatuma kwenda kuwabatiza watu kwa jina la Utatu Mtakatifu, yaani, Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu.
Katika imani yetu, tunakiri kile ambacho Mungu ametufunulia kuhusu yeye mwenyewe. Kwamba “Nasadiki kwa Mungu mmoja, Baba mwenyezi, muumba wa mbingu na dunia, na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana”. Kupitia Agano la Kale, Mungu anajifunua kama Muumba na mtegemezi wa vitu alivyoviumba. Yeye ni baba kwa watu wake waliochaguliwa, akiwa msaada wao na, kupitia manabii na watu wengine waliotiwa mafuta, akiwapa maagizo ya haki.
“Nasadiki kwa Bwana mmoja Yesu Kristo, Mwana pekee wa Mungu, aliyezaliwa na Baba tangu milele yote, Mungu kutoka kwa Mungu, Mwanga kwa Mwanga, Mungu wa kweli kwa Mungu kweli, aliezaliwa, bila kuumbwa, mwenye umoja na Baba; kwa njia yake vitu vyote viliumbwa. Alishuka kutoka mbinguni, kwa ajili yetu wanadamu na kwa ajili ya wokovu wetu, …”. Kristo ni udhihirisho wa Mungu asiyeonekana aliyekuja kuishi nasi ili kuleta Utatu Mtakatifu karibu nasi. Yeye ni sakramenti ya Baba, yaani, ishara inayoonekana ya neema/ukweli usioonekana. Pia, baada lituachia Mwili na Damu yake ili tule na kunywa ili tuweze kupata kuonya moja kwa moja upendo na msaada wa Mungu katika safari yetu ya kurudi kwa Mungu.
“Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana, mleta uzima, atokaye kwa Baba na Mwana, ambaye anaabudiwa na kutukuzwa, pamoja na Baba na Mwana, aliyenena kwa vinywa manabii”. Roho Mtakatifu ni nafsi ya tatu ya Utatu Mtakatifu. Yeye ndiye anayetuwezesha kuhusiana na Mungu. Mtume Paulo anatufundisha kwamba ni kwa nguvu za Roho Mtakatifu tunaweza kumwita Mungu Abba-Baba. Bila Roho Mtakatifu hatuwezi kumwita wala kumsikiliza Mungu, na yule mwovu anachukua fursa hiyo kuzungumza nasi akiwa amejinafiki kuwa sauti ya Mungu.
Kila wakati Mungu anatenda, anatenda kama umoja kwa sababu yeye ni umoja usiogawanyika. Hata hivyo, tunampata kwa njia hii ya fumbo la Utatu Mtakatifu. Hapo mwanzo, Mungu alisema, “Na tufanye mtu kwa mfano wetu na sura yetu” (Mwa 1:26). Pia tunasoma kwamba Roho wa Mungu alikuwa akienea juu ya uso wa maji kabla ya kitu chochote kuumbwa. Mungu pia aliumba mbingu na dunia kwa Neno lake, Mungu Mwana. Katika Mt. 3:16-17, wakati wa ubatizo wa Yesu, Roho wa Mungu alishuka juu yake kwa umbo la hua na sauti ya Baba ilithibitisha kwamba yeye ni Mwana mpendwa wa Mungu. Wakati wa Kanisa ni wakati wa Roho Mtakatifu ambaye anaendeza kazi ya wokovu kwa kuwahamasisha Wakristo kumwiga Kristo katika maisha yao na kuleta upendo na wokovu duniani.
Baada ya maelezo kuhusu Utatu Mtakatifu, tunajiuliza, Mungu anamaanisha nini kwa kujifunua kwetu kama Utatu Mtakatifu? Ninaamini kwamba Mungu alikusudia tushiriki katika upendo wake wa kipekee. Ni upendo wa nguvu sana ambao humwezesha kujidhihirisha kwa njia tatu lakini kubaki mmoja. Tunaweza kufupisha hili katika kauli moja, “Umoja katika utofauti bila kuchanganyikiwa.”
Mungu aliumba jinsia mbili za binadamu na kuwajalia uwezo wa kuzaa na kuleta watoto duniani kama matunda ya upendo na umoja kati yao. Mungu angeweza kuumba jinsia moja yenye uwezo wa kuzaa peke yake kama mimea mingi ifanyavyo. Hata hivyo, alitaka wanadamu walioumbwa kwa sura na mfano wake wapate kushiriki upendo wake. Upendo hauwezi kuwa wa ndan kwa ndani tu bali asili yake ni kutoka nje na kuenea. Upendo hujidhihirisha kwa kufurika nje ya chanzo chake na katika mchakato huo usababisha uhai.
Upendo huu unapaswa kujidhihirisha katika familia zetu, sehemu zetu za kazi, taasisi zetu za umma na binafsi, na jamii zetu. Mtume Paulo anafupisha sifa za upendo wa kweli kuwa uvumilivu na wema. Hauwi na tamaa, husuda, au kutenda vibaya. Upendo hautafuti faida kwa ajili yake na hauchukii au kuwa na hasira. Upendo hausingizii uovu wala kufurahia uovu bali unafurahia ukweli na maendeleo ya jirani. Upendo daima hukumbatia bila kujali ni nani.
Wapendwa, tunapotafakari juu ya fumbo la Utatu Mtakatifu leo, tujifunze umoja katika utofauti na tujenge familia na jamii zinazofurika na upendo na nguvu chanya.
Sikukuu njema.
Fr. Lawrence Muthee, SVD
