Masomo ya Jumapili kwa Kifupi, Pentekoste B

Matendo 2:1-11; Zaburi 104; Wagalatia 5:16-25; Yohana 15:16-27, 16:12-15

Roho Mtakatifu ni Nani?

oplus_2

Wapendwa, leo ni Sikukuu ya Pentekoste. “Pentekoste” ni neno la Kigiriki linalomaanisha “hamsini.” Kwa hiyo, Pentekoste ni siku ya hamsini na ya mwisho ya Kipindi cha Pasaka. Katika sikukuu hii, Wakristo huadhimisha Ujio wa Roho Mtakatifu juu ya wanafunzi wa Yesu na kwetu wote tuliobatizwa. Sherehe hii inalingana na sikukuu ya Kiyahudi ya Shavuot ambayo inaashiria siku walifanyika taifa takatifu la Mungu kwa kukubali sheria kupitia Musa. Siku hii pia ni sikukuu ya kuzaliwa kwa Kanisa. Wanafunzi, wakiwa wamejawa Roho Mtakatifu, walipata ujasiri na kujitokeza hadharani kwa mara ya kwanza tangu kifo cha Yesu. Ujumbe wao ulikuwa kwamba mtu aliyeitwa Yesu ambaye Wayahudi walimfitinisha kwa Warumi ili asulubiwe, ndiye Masiha na tena yuko hai. Roho Mtakatifu aliwajaza uelewa wa mambo ambayo Yesu alifanya na kuwafundisha.

Sasa, Roho Mtakatifu ni nani? Katika Kanuni ya Imani ya Nicea-Konstantinopoli, tunasema, “Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana, mleta wa uzima, atokaye kwa Baba na Mwana, ambaye pamoja na Baba na Mwana anaabudiwa na kutukuzwa, ambaye amenena kwa manabii.” Kwa hiyo, Roho Mtakatifu ni nafsi ya tatu ya Mungu au Utatu Mtakatifu. Mungu mmoja, nafsi tatu, Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu walioungana kwa upendo.

Mungu Baba hujidhihirisha kama muumba na Baba huisha na kutunza uumbaji wake. Mungu Mwana hujidhihirisha kama mwokozi aliyekuja kurejesha uhusiano wetu uliovunjika na Baba. Mungu Roho Mtakatifu hujidhihirisha kama nguvu ya Mungu inayotosaidia kuamini katika Baba na Mwana. Yeye ndiye anayetuongoza kufanya mapenzi ya Mungu au kama Mtakatifu Paulo anavyosema kumwita Mungu “ABBA.” Yeye ndiye aliyewapa wanafunzi wa Yesu na sisi maarifa na uelewa wa Bwana mfufuka na ujasiri wa kumtangaza kwa watu wote.

Katika Agano la Kale, tunasikia jinsi Mungu Baba alivyoumba na kudumisha uumbaji wake. Mungu anaahidi watu wake ukombozi kupitia mkombozi atakayekuja. Katika Agano Jipya, tunakutana na Mungu Mwana, Yesu Kristo, ambaye tunaamini kuwa ni Mwana wa Mungu na Masiha aliyetabiriwa. Alishuka kutoka kwa Baba kuleta ufalme wa Mungu duniani. Alipokuwa akimaliza kazi yake, aliwaahidi wafuasi wake msaidizi ambaye ni Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu ndiye ambaye, tangu siku ya Pentekoste, amekuwa akihuisha utume  wa Kikristo wa kuleta Ufalme wa Mungu duniani hadi leo.

Wakati wa Roho Mtakatifu ni wakati wa Kanisa. Anafanya kazi katika Kanisa kututakasa na kuendelea kutufundisha njia ya wokovu. Roho Mtakatifu anatuhamasisha kuishi katika jamii zilizounganishwa kwa upendo na kusudi moja. Hii ni imani yetu na inatufanya tuwe wafuasi wa Kristo.

Katika sakramenti ya ubatizo, tunapokea Roho wa Mungu ambaye anatujalia kuwa watoto wake, anatuosha dhambi yetu ya asili (dhambi ya kibinadamu tunayorithi kutoka kwa wazazi wetu), na kutufanya warithi wa Ufalme wa Mungu. Roho anatufanya tujazwe na matunda ya upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na Kiasi. Katika Sakramenti ya Kipaimara, tunapokea mapaji ya Roho Mtakatifu yanayotufanya kuwa watu wazima katika imani na kutupa ujasiri wa kutetea imani yetu. Haya ni hekima, akili, shauri, nguvu, elimu, ibada, na uchaji wa Mungu. Wale waliofundishwa vizuri katika imani kupitia katekesi sahihi hawatapata shida kuelewa mambo haya. Hata hivyo, kutokana na mara nyingi mafundisho yasiokidhi na ukosefu wa malezi endelevu ya kiimani, Wakristo wengi hukwama na mara nyingi huchanganyikiwa na kupotoshwa kuhusu Roho Mtakatifu na nafasi yake katika maisha ya Mkristo. Roho Mtakatifu anaweza kutuhamasisha tu ikiwa tutampa nafasi na ushirikiano. Yeye si roboti au mashine ya ATM. Kupitia vipawa na matunda yake, tunaweza kukabiliana na hali zozote za maisha.

Wengine wameaminishwa kuwa Roho Mtakatifu ni chombo cha kufanyia miujiza ili kujipatia umaarufu na kuvutia umati kwa faida binafsi. Wengine wamemgeuza kuwa kama Mashine ya kuwapa kila kitu wanachotaka, hasa utajiri. Bado wengine wamemfanya kuwa silaha ya kulipiza kisasi dhidi ya maadui zao. Wengine wanataka afanye kazi zote kwa niaba yao wao wapumzike na kufurahia maisha. Hii inajidhihirisha katika jinsi tunavyomchukulia Roho Mtakatifu katika ibada zetu.

Watu wanakwenda mbali na kutumia gharama nyingi ili waweze kufanikiwa maishani. Wengine wanatumia njia zozote kuonyesha watu kwamba wanaye roho mwenye nguvu. Roho inayotafutwa zaidi ni ile ya utajiri na miujiza ya uponyaji. Badala ya roho kuwaunganisha watu, kuna mgawanyiko zaidi katika makanisa. Roho inayosababisha mgawanyiko na ushindani mbaya haiwezi kuwa Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu aliwajalia wanafunzi kuzungumza kwa njia ambayo kila mtu aliyekuwepo aliweza kusikia na kuelewa hivyo kuleta umoja badala ya mgawanyiko.

Roho Mtakatifu hawezi kununuliwa kwa pesa, kuuzwa, kununuliwa, au kumiminwa juu ya mtu maombi yaliyopambwa na maigizo. anawaangazia awapendao yeye na kwa wakati aliouchagua yeye mwenyewe. Roho Mtakatifu ni Mungu mwenye upendo ambaye kila mara anataka kutuhamasisha kuishi maisha yenye matunda. Hawezi kutumika kuleta madhara au kudhalilisha wengine. Hajilazimishi juu yetu bali anahitaji ushirikiano wetu.

Ubatizo pekee hautufanyi tuwe Wakristo wakomavu. Wale ambao hawajafundishwa vizuri katika imani wanafananishwa na askari anayeyaacha kambi bila kumaliza mafunzo yake. Anaweza kuwa hatari sana kwa kikosi chake katika uwanja wa vita. Maarifa kidogo hasa katika mambo ya imani ni hatari sana katika jumuiya zetu za imani. Tuna watu wengi wanaodai wameona maono yaliyo wasukuma kuanza kuhubiri. Hawa huishia kuchanganyikiwa na kuwachanganya waumini wasioelewa kuwafuata. Wale wanaohisi wameitwa kuwa viongozi wa kiroho wanahitaji kupitia mafunzo na uchunguzi wa kina kabla ya kuruhusiwa kufundisha. Wale ambao wamefundishwa wanahitaji mafunzo ya mara kwa mara ili kusoma alama za nyakati na kujikumbusha kazi za Roho.

Ndugu wapendwa, tujiulize, ni roho yuo anayefanya kazi ndani yetu tunapofikiria, kutenda, na kuzungumza. Tumwombe Roho Mtakatifu wa Mungu akae ndani yetu na kutuangazia kuwa watu wema zaidi.

Uwe na Pentekoste yenye baraka.

Fr. Lawrence Muthee, SVD

Leave a comment