
Matendo 9:26-31; Zaburi 22; 1 Yohana 3:18-24; Yohana 15: 1-8
Bila ya Kristo Hatuwezi
Wapendwa, leo ni Jumapili ya tano ya Pasaka. Tunazo wiki chache zaidi katika kipindi hiki ambacho ni kilele cha vipinfi vitano ya mwaka wa liturujia wa Kanisa. Kufikia sasa tayari tunajua mengi kuhusu ufufuo kutokana na masoma ya Jumapili na siku za wiki. Somo la kwanza, linasimulia kuhusu mtihani mgumu ambao Mtakatifu Paulo alilazimika kupitia baada ya uongofu wake, yaani, kutetea wongofu wake. Kama Paulo sisi pia tunakabiliana na mtihani huo mara nyingi. Mtakatifu Yohana anatutia moyo kwamba ikiwa dhamiri yetu ni safi, hatuhitaji kuogopa kuhukumiwa na ulimwengu.
Leo Yesu anajitambulisha kwetu kama mzabibu wa kweli ambao lazima tuendelee kuunganika nao. Baba ndiye mkulima anayeutunza na kuusafisha na kuupogoa. Matawi lazima yaendelee kuwa kuunganika na shina ili kupokea virutubisho na kuzaa matunda. Ikiwa matawi hayazai matunda, basi hayana faida kuwa kuwa juu ya shina.
Kama Wakristo, tunatarajiwa kuzaa matunda ambayo yatawavutia wengine kuunganika na Kristo. Kupitia kwa matawi mti uzaa matunda. Yesu ndiye mti wa matunda, na sisi ndio matawi yake. Sisi ndio tunatakiwa kuzaa matunda ya upendo wake, huruma, na umoja kwa wale wanaotuzunguka. Matawi ya mti wa matunda yanaweza kuwa na afya na kuwa na majani mengi lakini bila kuzaa matunda ni hayafai kitu. Nilipokuwa mtoto, nilijifunza kuhusu maana ya kupogoa mikahawa nyumbani. Nilijiuliza kwa nini wazazi wetu walikuwa wanaharibu mikahawa ambayo ilionekana mizuri sana ikiwa na majani mengi.
Matawi ya mti wa matunda lazima yapunguzwe ili kutoa nafasi kwa matunda kutokea na kupata mwanga wa kutosha na hewa ili kukomaa na kupata utamu. Ikiwa matawi yatabaki na majani mengi, yatazaa matunda machache sana ambayo hayawezi kuiva, au kuwa na utamu. Matawi lazima yaachie majani yao mazuri ili kuzaa matunda. Sadaka ni jambo la msingi katika maisha yetu ya kila siku. Kuna vitu ambavyo lazima tuviachie au kupoteza ili tuweze kuzaa matunda mazuri ikiwa ni pamoja na kiburi cha kujiona bora kuliko wengine, majivuno, na kuwahukumu wengine. Mambo haya yote na mengine kama hayo yanatufanya tujihisi vizuri lakini yanatuzuia kuzaa matunda mazuri. Kila tawi linazaa matunda kadiri ya uwezo wake. Hata hivyo, lililo muhimu ni kuzaa matunda mazuri.
Wapendwa, mwaliko huu wa Yesu kwa kila mmoja wetu hauwezi kuwa wazi zaidi. Tunaweza kuwa wanafunzi wake tu ikiwa tutafuata mfano wake na kuzaa matunda. Katika barua yake Mtakatifu Yohana analiweka vizuri, “Watoto wangu wadogo, tusipende kwa maneno tu, bali kwa kazi na ukweli.” Matendo husema zaidi kuliko maneno. Bila vitendo vya kweli, sisi ni kama matawi yenye majani mengi bila matunda. Watu wanaweza kuvutiwa kwetu lakini wanapotukaribia, watagundua kwamba hatuna kitu cha kuwapa. Wanasema, “Debe tupu hupiga kelele kubwa,” na watu wanaosubiri, hufanya hivyo kufidia upungufu wa uaminifu ndani yao.
Wakati Sauli alipoona mwanga njiani kwenda Damasko na kuamini katika Bwana mfufuka, wanafunzi wengine ambao walimjua awali kama mtesaji walikuwa na hofu ya kumkaribisha kati yao. Ililazimu Barnaba ambaye alikuwa ameona matunda ya Injili ndani yake, kuingilia kati ili kuwashawishi kwamba sasa alikuwa mwanafunzi. Ushuhuda wa wale wanaoonja matunda yetu ni muhimu kutushuhudia. Mti hauwezi kujua mwenyewe ikiwa matunda yake ni matamu au machungu. Ni wale wanaoyaonja ndio wanaweza kusema.
Mara nyingine tunatumia jitihada nyingi kufanya watu waamini kwamba sisi ni hivi au vile. Wengine hutumia jitihada sawa na hizo kufanya wengine waonekane wabaya kwa sababu ya wivu. Methali ya inatukumbusha kwamba “chema chajiuza kibaya chajitembeza” inamaanisha, pia nyingine usema “Uongo una maisha mafupi, lakini ukweli ni wa milele”. Shutuma za uongo haziwezi kuufanya mti mzuri uwe mbaya, lakini kumbuka mti wenye matunda matamu ndio hutupwa mawe. Watu wanapokutupia mawe, jua kwamba hawakushambulii ila wanapiga matunda yalioko juu yako ili wapate kula. Ukweli daima una njia ya kujidhihirisha, haijalishi utachukua muda gani. Usijali wale wanaosambaza uongo dhidi yako, wakati ukweli utakapodhihirika, wataishifa kujificha.
Kuzaa matunda ina maana kuwa waaminifu katika wito na utume wetu. Mengine ni siasa na maneno matupu. Ikiwa wewe ni kiongozi, ongoza kwa mfano na si kupitia kipaza sauti au ilani. Ikiwa wewe ni mwanafunzi, muige mwalimu wako, mwisho wa hadithi. Yesu anatupa mfano wa kiongozi wa kweli anayeongoza kwa mfano.
Wapendwa, ikiwa tutabaki tumeshikamana na Kristo matunda yetu yatakuwa matamu kwa wale walio karibu nasi, lakini ikiwa tumejitenga naye, tunaweza kuongeza viungo vyote vitamu tunavyoweza kupata lakini matunda yetu yatakuwa daima machungu. Hatuwezi kusemea utamu wa matunda yetu wenyewe, wale wanaoyaonja ndio wanaoweza kusema.
Uwe na Jumapili njema.
Pd. Lawrence Muthee, SVD
