Masomo ya Jumapili kwa Kifupi: Maajilio 1 A

Masomo ya Jumapili kwa Kifupi: Maajilio 1 A

Isaya 63:16-17.19. 64: 2-7; Zaburi 80; 1 Wakorintho 1:3-9; Marko 13:33-37

Maandalizi na Ujio

Wapendwa, leo tunaanza mwaka mpya katika kalenda ya liturujia ya Kanisa ambayo itakuwa na vipindi vitano au nyakati tano ukipenda. Hizi nyakati tano ni alama za matukio matano muhimu zaidi katika historia ya wokovu wetu. Kila mwaka tunakumbuka matukio haya na hii hutufanya tuelewe zaidi imani yetu. Kwa kifupi, kipindi cha Majilio ni wakati wa kuandaa kuzaliwa kwa Masiha. Kipindi cha Krismasi ni wakati tunasherehekea kuzaliwa kwake Masiha. Kipindi cha Kwaresima ni wakati wa kutubu na kuishi upya matukio yaliyopelekea wokovu wetu kupitia Masiha. Pasaka ni wakati wa furaha kwa sababu wokovu wetu umetimia kupitia kufufuka kwa Masiha, na Wakati wa Kawaida ni wakati wa kuelewa zaidi Ufalme wa Mungu mwalimu wetu akiwa Masiha mwenyewe. Sasa unajua.

Leo tunaanza kipindi cha Majilio ambacho kina wiki nne. Majilio maana yake ni “ujio” au “kuwasili” kwa kile kilichosubiriwa. Ni kungojea kwa shauku kuzaliwa kwa Masiha mioyoni mwetu. Kila mwaka tunakumbuka kwa shauku hii na utayari zaidi kumkaribisha Masiha upya katika maisha yetu. Ni wakati wa kusafisha na kurekebisha njia zetu ili Masiha aweze kupata furaha kukaa nasi. Labda katika mwaka mzima tumechafua maisha yetu kiasi kwamba tunahofia hata kumkaribisha. Kushindwa kupenda Mungu na Jirani, vilevile kushindwa kutekeleza majukumu yetu kwa uaminifu, vinaharibu maisha yetu na kutuweka mbali Mungu. Basi, sasa ndio wakati wa kusafisha machafuko hayo. Tutagundua kwamba Bwana wetu daima ni mwenye huruma kwa moyo wenye toba.

Katika somo la kwanza, tunasikia jinsi waisraeli walivyodhoofika kwa sababu mambo hayakuwa mazuri kwao, na msaada waliokuwa wakipata kutoka kwa Mungu haukuonekana kuja kwao. Manabii wanakumbusha jinsi mambo yalivyokuwa wakati Bwana alikuwa mfalme wao. Sasa watu wameachana naye na kumwabudu miungu ya kigeni, mambo yamekuwa mabaya kila siku. Hali hii ni sawa na maisha yetu leo. Tunakabiliana na hali ya hewa kali kwa sababu ya vitendo vyetu vya uharibifu dhidi ya mazingira. Kwa hakika, wengine wamefanya uharibifu zaidi kuliko wengine, lakini sote tunalipa gharama. Wale wanaoacha njia ya haki kujaribu njia za ulimwengu huu, hatimaye wanajikuta kwenye matatizo. Inahitaji neema ya Mungu na unyenyekevu mkubwa kugundua kuwa hali yetu ya sasa ni matunda ya jinsi tunavyoishi maisha yetu. Tunapenda kulaumu kila mtu kwa matatizo yetu isipokuwa sisi wenyewe. Wengi wameacha kuabudu kwa sababu wamekasirika na Mungu. Wanadhani amewaacha. Mungu hatunyang’anyi kitu kwa sababu yeye ndiye mmiliki wa vitu vyote. Badala yake, daima anatupa nafasi ili turudi katika upendo wake. Ikiwa tunamkimbia, tutalazimika kukabiliana na ulimwengu pekee yetu na hatuwezi kumlaumu kwa changamoto tunazokutana nazo huko. Ikiwa tupo karibu naye kwa uaminifu, tunaweza kukutana na changamoto, lakini kamwe hataruhusu tushindwe.

Kusubiri ni jambo la kawaida katika maisha yetu ya kila siku. Foleni ndefu benki, kusubiri katika vituo vya basi na hospitalini, kusubiri rafiki, nk. vinaweza kutufundisha kitu fulani. Kusubiri inaweza kuwa kero sana ikiwa hatujui jinsi ya kusubiri. Nimeona tabia nyingi za watu wanaposubiri. Wengine hukaa wakilalamika kuhusu kucheleweshwa mara tu wanapofika na kupata foleni ndefu na kuwasumbua wengine. Wengine huja na kitabu au gazeti kusoma wanaposubiri, na kuna wale kama mimi ambao huangalia na kuchunguza wengine wanavyosubiri. Leo, tukiwa na simu za kiganjani au rununu, kusubiri kumekuwa tofauti, wakati mwingine unaweza hata kuendelea kufanya kazi ukisubiri. Sote tunajua kwamba kulalamika hakufanyi foleni kwenda haraka zaidi, lakini tukiendelea kushughulika tunaposubiri, hatuhisi hata jinsi muda unavyopita.

Katika Injili ya leo, Yesu anatuasa tukeshe tunaposubiri kurudi kwake. Wengi wamepoteza mali zao vituoni vya mabasi, benki, hospitalini, na mahali pengine wanaposubiri kwa sababu hawakuwa macho. Tunaposubiri Ufalme wa Mungu, Mtume Petro anatuonya, “Basi, iweni waangalifu na kukesha, kwa maana adui yenu Ibilisi, huzunguka-zunguka kama simba angurumaye, akitafuta mtu ammeze” (1 Pt 5:8-9). Tofauti na sisi, Ibilisi ni mwenye subira na na yupo macho sana, akisubiri wakati mwafaka wa kushambulia kama simba anavyofanya. Kama katika mchezo wa ngumi, tunaposhusha ulinzi wetu, tunapigwa ngumi za usoni na yule mwovu. Kusubiri kwetu kama Wakristo lazima kuwe kwa kukesha na kushughulika. Hatujui Bwana atarudi lini, lakini ikiwa tupo macho, siku ya kurudi kwake sio suala kubwa kwetu. Atakaporudi, tutakuwa tayari kila wakati.

Wapendwa, tunapoanza kipindi hiki cha Majilio, nawakaribishani tujitafakari, labda tunateseka kwa sababu tumeghaili mapenzi ya Mungu. Mungu wetu atuletee furaha na uponyaji wakati tunaposubiri kurudi kwake.

Na mwanzo mwema wa Majilio.

Pd. Lawrence Muthee, SVD

2 thoughts on “Masomo ya Jumapili kwa Kifupi: Maajilio 1 A

Leave a reply to Dennis Ombeni Cancel reply