Tatizo Lililofichika na Fr. Lawrence Muthee, SVD

Je, umewahi kughadhabika au kukatishwa tamaa na huduma katika ofisi za umma? Hili linaweza kuwa kutokana na ucheleweshaji usioelezeka, mifumo taratibu au inayokwama mara kwa mara, maafisa kutokuwepo, au nyaraka kupotea, miongoni mwa mambo mengine. Katika baadhi ya ofisi, watu husubiri kwa saa nyingi, na hata siku kadhaa, ili kuwasilisha nyaraka za maombi tu. Baada ya kuwasilisha, husubiri tena kwa siku au miezi kadhaa kabla ya kupata majibu. Mchakato rahisi unaohitaji sahihi tu huwa mgumu, wa gharama kubwa, na unaotumia muda mwingi. Mchakato kama huo unaweza kuchukua dakika chache au masaa machache tu kama maafisa husika wangekuwepo na kufanya kazi yao. Ni kama vile imekuwa kawaida kwamba huduma za umma lazima zicheleweshwe ili zionekane kuwa muhimu. Chukulia mfano wa kupata hati miliki ya ardhi. Hata kama una taarifa na nyaraka zote zinazohitajika, inaweza kuchukua miezi kadhaa kuipata.

Miaka michache iliyopita, nilikutana na mzee mmoja katika ofisi za Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), na tulipokuwa tukipanda ngazi kwenda ghorofa la nne (kwa sababu lifti zilikuwa hazifanyi kazi), tukaanza kuzungumza. Mzee huyo aliniambia kwamba lifti ziliharibika miezi tisa iliyopita. Nilipouliza alijuaje hilo, alisema kwamba amekuwa akitembelea ofisi hiyo kudai mafao yake ya uzeeni kwa miaka mitatu bila mafanikio. Hilo lilinishangaza sana. Aliongeza kuwa kila anapokuja, kuna kitu ambacho kinakosekana au hakifanyi kazi. Aliniambia kwamba anamfahamu mtu aliyekufa akifuatilia mafao yake. Swali ni: nini hasa husababisha ucheleweshaji katika ofisi za umma?

Jibu la haraka kwa swali hilo ni RUSHWA. Rushwa ina sura nyingi. Ile ya kawaida ni pale afisa anapohitaji hongo ili kuharakisha mchakato. Hata hivyo, aina nyingine za rushwa hazionekani moja kwa moja na huenda hata zisionekane kama rushwa. Mojawapo ni posho za safari (per diem), yaani posho zinazotolewa kwa wafanyakazi wanapofanya kazi nje ya vituo vyao vya kazi ili kufidia gharama za usafiri na kazi. Katika hali nyingi nilizoshuhudia, viwango vya posho hizi ni vikubwa mno kuliko gharama halisi za safari. Kumbuka, mara nyingine, usafiri na chakula hutolewa na ofisi mbali na posho za safari. Hapo ndipo tatizo linapoanza.

Katika taasisi nyingi za serikali na mashirika yasio ya kiserikali, posho za safari za kila mwezi huenda zikazidi mshahara wa kawaida wa mfanyakazi. Katika sekta binafsi, hili ni nadra sana kwa sababu zilizo wazi. Mmiliki huhakikisha kwamba anapata thamani ya pesa kutoka kwa kila mfanyakazi. Ndiyo maana, watu wengi waliowahi kufanya kazi katika sekta ya umma huwawia vigumu sana kufanya kazi katika sekta binafsi. Kwa tamaa ya posho za safari, maafisa wengi wa umma hutumia muda mwingi katika vikao, ziara za mafunzo, kutembelea miradi, na mikutano ya bodi katika hoteli za kifahari. Katika vituo vyao vya kazi, foleni za wanaosubiri huduma zinaongezeka kila siku. Cha kusikitisha zaidi, hakuna taarifa ambo hutolewa iwapo maafisa wapo ofisini au la. Watu husubiri hadi ofisi zinafungwa.

Aina nyingine ya rushwa ni utoro kazini. Hii ni pale ambapo maafisa wanakosa kuripoti kazini au wanakuja kwa muda mfupi kisha wanatoweka ofisini. Hii inajitokeza sana katika sekta kama afya, uhandisi, upimaji wa ardhi, n.k., kwa sababu maafisa wengi wana ofisi binafsi ambako hutumia muda wao mwingi. Baadhi ya wakuu huacha ofisi zao wazi na makoti yao yakiwa juu ya viti. Watu wanaosubiri kuhudumiwa hudhani kwamba afisa yuko karibu. Mwishoni mwa mwezi, maafisa hawa hupokea mishahara yao huku wakipata faida kupitia biashara zao binafsi. Idara nyingi za serikali na mashirika yasio ya kiserikali hupoteza fedha nyingi ambazo zingetumika katika miradi kwa kulipa posho za safari. Hivi karibuni, mkanganyiko na USAID ulienea kwenye vyombo vya habari. Ilidaiwa kwamba sehemu kubwa ya fedha inaelekezwa katika kulipia posho za safari na maisha ya kifahari ya maafisa nje ya nchi, na kiasi kidogo sana hufika kwenye miradi iliyokusudiwa.

Aina nyingine ya rushwa ni uhepukaji wa wajibu kwa madai ya stahiki zisizo za haki (false entitlement). Hii ni pale mfanyakazi anapoamini kwamba anastahili haki, zawadi, au manufaa ambayo kisheria, kimkataba, au kwa makubaliano ya kikazi, hastahili. Hili linaweza kusababishwa na mambo mbalimbali, ikiwemo muda mrefu kazini, ongezeko la mahitaji ya kifedha binafsi au ya kifamilia, ongezeko la masomo au mafunzo, au uhusiano na mwajiri au msimamizi wake. Dhana hii ya kujihisi kustahili inaweza kuathiri vibaya kazi za timu na mahusiano kazini. Wale wanaojiona kudhulumiwa ugeuka kuwa wazembe, sumu kwa wengine, au hata kuacha kazi.

Katika maonyesho ya vitabu katika mji mmoja barani Ulaya, nilikutana na mfanyakazi wa shirika moja linalofanya kazi katika mojawapo ya mitaa mikubwa zaidi ya mabanda barani Afrika. Tulipokuwa tukizungumza, niligundua kwamba shirika lake lilikuwa likifanya kazi katika mtaa huo kwa miaka 30. Nilipomuuliza kama aliona mabadiliko yaliyofanyika katika maisha ya watu kutpitia shirika lake katika miaka hiyo, aliniambia kwa uwazi kwamba, kwa bahati mbaya, kufanya mabadiliko katika maisha ya watu si kipaumbele cha mashirika mengi kama lake. Kipaumbele ni kukusanya fedha kwa miradi isiyoisha ili kudumisha ajira za maafisa wa shirika. Hivyo ndivyo hali ilivyofikia kuwa mbaya.

Kulingana na FAO Statistical Yearbook 2024, dunia huzalisha chakula cha kutosha kumlisha kila mtu. Tatizo ni usambazaji, ukosefu wa usawa, na upotevu. Kulingana na WFP (wfp.org), asilimia 18% ya chakula duniani hupotezwa huku karibu bilioni moja wakikabiliwa na lishe duni (SOFI report, who.int). Serikali nyingi za nchi za kusini mwa dunia haziwezi kuhakikisha chakula kwa raia wote kwa sababu ya usimamizi mbaya wa rasilimali unaosababishwa na rushwa iliyokithiri.

Kuna ukosefu mkubwa wa uzalendo miongoni mwa maafisa wa serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali. Tamaa ya kujilinda, upendeleo, na uvivu vimeenea katika sekta zote. Kwa upande mmoja, sekta binafsi inaendeshwa kwa misingi ya ubepari kupita kiasi na kwa upande wa pili hakuna mifumo ya ukaguzi na uwajibishaji katika taasisi za umma. Wakati kila mtu ana “mikono michafu,” hakuna mtu anayeweza kumsimamia mwingine. Ingawa hazikosi changamoto zake, baadhi ya dini kuu kama Kanisa Katoliki zimeweza kubadilisha jamii kutokana na nidhamu, wito wa utume, ukaguzi, na usimamizi wa karibu. Hata hivyo, ili jamii ifurahie maendeleo ya kuaminika na endelevu, sekta zote lazima zishirikiane.

Aina nyingine ya rushwa na maarufu zaidi ni hongo. Kutoa na kupokea hongo ni sababu kuu ya kukiukwa kwa haki za msingi za binadamu. Katika utume wangu, tuna kesi nyingi sana za unyanyasaji wa watoto katika mfumo wa ndoa za utotoni. Wahalifu wakuu ni wazazi, hasa kinababa, wanaowaoza binti zao ili kupata ng’ombe. Baadhi yao huolewa na wanaume wa umri wa babu zao. Kama utume wa parokia, tumetengeneza mahali salama ambapo wasichana katika hali hii wanaweza kukimbilia. Hata hivyo, hatuna uwezo wa kuwaokoa wote bila ushirikiano wa mamlaka za kisheria na viongozi wa jamii. Katika majaribio mengi tuliyofanya kuwaokoa wasichana hawa, kiungo dhaifu kila wakati kimekuwa ni viongozi wa jamii na maafisa watendaji wanaopaswa kusimamia sheria.  Wahalifu hulipa hongo kubwa, na wasichana huishia kuolewa kwa lazima. Viwango vya kukiuka sheria katika jamii yetu ni vya kutisha. Hivyo, wanyonge wanaendelea kuteseka. Sio mpango na mapenzi ya Mungu kwamba baadhi ya wanadamu kuishi maisha ya kifalme na wengine kuishi utumwa. Haya ni mambo ya mila na desturi za kibinadamu ambao kama vile yaliwekwa yanaweza pia kubadilishwa.

Hali hii ya Rushwa iliyosheheni jamii yetu inaanzia katika familia na jamii tunazokulia. Kuna uhitaji mkubwa wa mazungumzo ya pamoja, kati ya sekta mbalimbali kuhusu rushwa, na kutafakari upya jinsi tunavyoweza kurekebisha misingi ya maadili katika jamii yetu. Je, wewe ni mwathirika au ni mhusika katika kutoa na kupokea rushwa katika sekta yako? Na Je, unadhani njia ya kutoka katika giza hili ni ipi?

Leave a comment