Masomo ya Dominika kwa Ufupi: Dominika ya 19 ya Mwaka C


Hekima 18:6-9; Zaburi 32(33); Waebrania 11:1-2, 8-19; Luka 12:32-48

Ukweli Usioonekana


Wapendwa, leo ni Dominika ya kumi na tisa ya mwaka wa kawaida. Masomo ya leo yanatualika kutafakari juu ya uhakika wa mambo tunayoyaamini. Jumapili iliyopita tulitafakari jinsi ubinafsi ulivyoingia katika jamii yetu, na ni wachache sana wanaojitoa kwa ajili ya manufaa ya wote bila kutarajia malipo ya ziada mbali na iliyo halali yao. Kabla ya watu kukubali jukumu fulani, siku hizi wauliza watafaidi nini. Kabla ya kutoa zabuni, huuliza asilimia yao itakuwa kiasi gani. Vivyo hivyo, nimewasikia watu wakijiuliza watafaidi nini wakienda Kanisani. Swali ni Je, unadhani nini faida ya kwa kwenda Kanisani?

Imani inajengwa juu ya uhakika kwamba Mungu anatimiza ahadi zake kwa  watu wake. Kuhusu imani, hakuna kitu tofauti cha kushikilia isipokuwa tumaini la ahadi zilizotolewa katika Kristu Yesu. Katika somo la kwanza, watu walishikilia ahadi zilizotolewa kwa mababu zao, na hili liliwafanya wavumilie mateso yote. Mara nyingi sana, Mungu aliwaokoa Waisraeli kutoka kwa maadui zao kwa msingi wa ahadi alizowapa mababu zao. Kuja kwa Kristo kulikuwa kilele cha utimilifu wa ahadi aliyowapa wana wa Israeli. Kama waamini, rejea ya imani yetu ni matukio ya Pasaka yaliyotokea zaidi ya miaka 2000 iliyopita.

Katika somo la pili, waraka kwa Waebrania unamtaja Abrahamu ambaye, kwa sababu ya imani yake kubwa kwa Mungu, alifanyika baba wa wote wanaoamini hadi leo hii. Katika Abrahamu tunapata mfano wa muumini wa kweli. Aliamini ahadi zisizoonekana na akaweka maisha yake mikononi mwa matarajio ambao wakati huo yalikuwa ahadi tu. Siku hizi, watu wanataka kuona miujiza kabla ya kuamini. Hii inapinga kabisa maana halisi ya imani: kuwa na hakika ya mambo yasioonekana kwa macho au kutambulika kwa hisia za kimwili. Hata sayansi yenyewe imethibitisha kwamba mambo tunayoweza kushuhudia kwa macho ni machache sana ukilinganishwa na yale tusioyaona.

Kwa imani, Abrahamu aliacha nchi ya mababu zake kwenda katika nchi asiyoijua? Kwa nini Sara aliweza kupata mtoto katika uzee wake? Jibu ni kwa imani. Abrahamu alikuwa tayari kumtoa dhabihu mwanae wa pekee ambaye ndiye alikuwa alishikilia ahadi ya Mungu ya kuwa taifa kubwa. Ingawa Abrahamu alijua hatapata kuishi hadi kuona ahadi zote za Mungu zikitimia, alikuwa na imani ya kutosha kuanza safari. Swali ni je, ni kwa kiasi gani wewe na mimi tuko tayari kuwekeza katika imani? Mungu hakutani nasi ana kwa ana bali kupitia alama na ishara. Si macho ya kimwili yanayomshuhudia Mungu, bali ni imani yetu. Macho ya kimwili yaliyoona tunda lililokatazwa kuwa ni zuri kwa chakula (Mwa 3:6) yalipoteza heshima na uwezo wa kumshuhudia Mungu. Ni kwa imani tu tunaweza kumwona Mungu. Acha kupoteza muda na fedha ukifuata miujiza na sarakasi, kwa kuwa hata hao wasingiziao kuwa na nguvu za kutenda miujiza hawawezi kumwona Mungu.

Katika Injili, Yesu anafichua hali wa kibinadamu inayotuandama: “Mahali ambapo hazina ya mtu ipo, ndipo moyo wake ulipo.” Wapo wengi wasioheshimu siku za ibada kwa sababu wana shughuli za kutafuta pesa. Ukiwa mkweli, utakubali kwamba masaa machache unazokosa kwenda Kanisani huenda hufanyi chochote cha faida. Kuwa na imani ni kutumaini na kutamani zaidi ya yaliyo katika dunia hii. Tamaa ya mambo haya ndiyo inayochochea mwenendo wetu. Imani huwafanya watu kutenda haki, hudumisha mshikamano wa kijamii, huleta amani (hofu ya Mungu), huongoza utawala bora, huhakikisha haki na uadilifu katika huduma za umma, na huimarisha usalama miongoni mwa mambo mengine.

Yesu anatukumbusha kwamba hakuna ajuaye siku wala saa. Tungalijua siku ya kufa, maisha yangejaa vurugu. Mungu ameficha makusudi hili ambalo linatusawasisha wote, wenye nguvu na wanyonge, matajiri na maskini. Hivyo, tunapaswa kuwa macho tusije tukafumaniwa na siku hiyo. Wengi watafumaniwa na kupigwa viboko vingi kama anavyosema yesu katika Injili ya leo. Yeyote aliyepewa vingi, kwake vingi vitatakwa.

Wapendwa, tafakari kuhusu majukumu na nafasi uliyopewa. Je, unatumika ipasavyo? Je, majitoleo yako yanalingana na uwezo ambao Mungu amekupa? Je, mchango wako unalingana na matumizi yako?

Jumapili Njema
Padri Lawrence Muthee, SVD

Leave a comment