Yeremia 23:1-6; Zaburi 23; Waefeso 2:13-18; Marko 6:30-34
Kuponya Majeraha
Wapendwa, tunapozama zaidi katika Kipindi cha Kawaida cha kalenda ya liturujia ya Kanisa, lazima tuwe tumeanza kutambua kwamba masomo ya kila Jumapili yanabeba mada maalum. Jumapili iliyopita Yesu aliwatuma wanafunzi wake kwenda kuhubiri kama jaribio la kile walichokuwa wamejifunza kutoka kwake. Kwa ubatizo, tulifanywa kuwa washirika katika utume waw a Kristo wa kuhubiri Injili. Nabii Amosi alitumwa na Mungu kuwaonya makuhani wa hekalu waliokuwa wameshindwa kutekeleza wajibu wao na na kwanyanyasa na kuwahumiza maskini na wanyonge. Yesu alikuja kuponya majeraha ya ulimwengu. Anatutuma sisi sote pia ulimwenguni kuendeleza utume huu wa uponyaji.
Katika Injili ya leo, wanafunzi walirudi kwa Yesu na taarifa ya yale walichofanya. Ali akitambua kwamba walikuwa wamechoka, Yesu alipendekeza waende mahali pa faragha kupumzika. Hata hivyo, umati mkubwa ulikuwa unawafuata kutoka nyuma. Umati huo labda ulitaka kusikia zaidi kuhusu hii habari njema mpya na ya kutia moyo kuhusu Ufalme wa Mungu ambayo ilizungumzia majeraha yao. Kwa kuwafuata wanafunzi, umati ulifika mahali alipokuwa Bwan. Kwa kuwaonea huruma, Yeasu alianza kuwahubiria kwa kuwa walikuwa kama kondoo waliojeruhiwa na bila mchungaji.Vivyo hivyo, kila mbatizwa hufanyika mwanafunzi wa Yesu.
Mwanafunzi hufanya kile alichojifunza kutoka kwa mwalimu wake. Katika Injili ya Yohana 1, tunasoma kwamba baada ya kuona mahali Yesu alipoishi, Filipo alikwenda na kumleta ndugu yake Nathanaeli kwa Yesu. Katika Yohana 4, baada ya kumtambua Yesu kama Masihi ambaye alipaswa kuja, mwanamke Msamaria alirudi kijijini kwake na kuwaleta watu wake kwa Yesu. Na wewe na mimi, je, tumeleta nani kwa Yesu hadi sasa?
Kinyume cha heri ni ole. Nabii Yeremia anatamka ole kwa wachungaji ambao badala ya kukusanya watu kwa Mungu waliwauumiza na kuwatawanya. Utume wa viongozi wa dini ni kuwaleta watu kwa Mungu ili wapate kuponywa na majeraha yao na si kuwavuta kwao wenyewe. Tunachokiona leo ni wahubiri na manabii wanaojitahidi kadiri ya uwezo wao kuwavuta watu wengi kwao wenyewe. Badala ya kuponya majeraha ya watu yaliyosababishwa na uvunjikaji wa familia, dhuluma za kijamii, kisiasa na kiuchumi, aina mbalimbali za unyanyasaji na wivu, wanawatawanya kwa usaliti na upotoshaji. Swali kwako na kwangu ni je, watu wangapi tumeumiza kwa maneno yetu, umbea, na vitendo vyetu?
Mungu anaahidi kumwinua mchungaji kutoka kwenye uzao wa Daudi, masihi, ambaye atawakusanya watu wote kutoka walipotawanyika na kuwaponya. Katika Zaburi 23, Daudi alitabiri ujio wa mchungaji huyu ambaye ataleta faraja kwa kondoo wake. Mtakatifu Paulo anatuambia kwamba ndani ya Kristo tuna mchungaji huyu mkuu ambaye anawatunza kondoo wake vizuri. Ndani yake na kupitia kifo na ufufuo wake, majeraha yote ya watu yanaponywa, na kinachobaki ni kundi moja chini ya mchungaji mmoja. Kwa bahati mbaya, si hivyo tunavyoona katika wachungaji wa siku hizi. Kuongezeka kwa madhehebu ya dini kunaendelea kusababisha majeraha zaidi na mgawanyiko badala ya uponyaji duniani. Watu wanachukiana kwa sababu wanatofautiana katika jinsi za kumwabudu Mungu. Kadhalika wanatetea chuki hiyo kwa kutumia jina la Mungu. Nisionekane kuwalenga wachungaji bila sababu. Mimi ningali mmojawapo, natambua kwamba kondoo mara nyingi huwa hawana tatizo, bali tatizo ni wachungaji ambao badala ya kuhubiri umoja wanasisitiza utofauti.
Imani yetu ya Kikristo ina vipimo viwili vinavyoungana na kutegemeana. Hivi ni vipimo vya wima na mlalo. Kipimo cha wima ni uhusiano wetu na Mungu na kipimo cha mlalo ni uhusiano wetu na wengine. Uhusiano wetu na Mungu unategemea uhusiano wetu na Jirani zetu, nao uhusiano wetu na Jirani zetu unategemea neema inayotokana na uhusiano wetu na Mungu. Mtu hawezi kudai kuwa na uhusiano mzuri na Mungu ikiwa anamchukia mwanadamu mwenzake.
Kipimo cha Mkristo mzuri sio mahudhurio mara nyingi au kwa kiasi cha sadaka na zaka anazotoa kanisani. Sadaka zote na ibada hazina maana iwapo hatujali wengine. Katika Mathayo 12:7 Yesu aliwaomba Mafarisayo wajifunze maana ya maneno ya Nabii Hosea 6:6, “Natamani rehema wala siyo dhabihu”. Hatuwezi kununua neema ya Mungu, anatoa bure kwa wale tu wanaoishi kulingana na mapenzi yake. Wale wanaoshika amri ya upendo kwa Mungu na jirani.
Mkutano wa hivi karibuni wa Baraza Kuu la Shirika la Wamisionari wa Neno la Mungu (SVD) kule Roma, ambacho nilikuwa mjumbe, ilijikita kwenye wito wa kuwa waponyaji wa majeraha ya watu nay a uumbaji na siyo chanzo cha majeraha. Mada ya sura hiyo ilikuwa, “…Kuwa Wanafunzi Waminifu na wabunifu katika Ulimwengu Uliojeruhiwa”. Hapa muhtasari wangu wa maazimio ya mkutano huo katika sentensi tano fupi:• Kutambua majeraha ya watu na uumbaji popote tulipo.• Kuhakikisha kwamba malezi ya wamisionari yanaelekezwa katika kukabiliana na majeraha ya ulimwengu.• Tukiimizwa na Neno la Mungu, kubuni njia za kukabiliana na majeraha duniani.• Kuwashirikisha vema walei katika utume wetu wa kimisionari.• kuweka mikakati ya kujitegemeza ili tuweze kudumu katika utume.
Kama wanadamu na zaidi kama wanafunzi wa Kristo, wito wetu ni kuufanya ulimwengu kuwa bora kwa wote kwa kutumia vipaji na fursa ambazo Mungu ametupa. Maswali ya kutafakari leo ni: Ni majeraha gani nimesababisha kwa wengine na kwa uumbaji? Je, nanafakari juu ya matokeo ya maneno na matendo yangu kwa wengine? Naweza kufanya nini ili kuponya majeraha niliyoyasababisha mimi na wengine? Je, nina majeraha yangu mwenyewe yanayohitaji kuponywa? Je, nimejaribu kuwasamehe wale walionijeruhi?
Jumapili yenye baraka.
Fr. Lawrence Muthee, SVD
