Amosi 7:12-15; Zaburi 85; Waefeso 1:3-14; Marko 6:7-13

Umeitwa, Ukachaguliwa, na Kutumwa
Wapendwa, leo ni Jumapili ya 15 katika kipindi wa kawaida. Baada ya Yesu kukusanya wafuasi kadhaa, aliwachagua baadhi yao kushiriki katika utume wake. Kila Mkristo ameitwa, amechaguliwa, na ametumwa kushiriki katika utume huu popote alipo. Tulipokea wito huu tulipobatizwa, kuoa au kuolewa, katika nadhiri za kitawa, upadrisho, au kuchaguliwa kwa nafasi ya uongozi. Maandiko Matakatifu yanatupa mifano mingi ya watu waliitwa, kuchaguliwa, na kutumwa na Mungu kushiriki katika kazi yake ya kuwaokoa wanadamu. Kwa mfano, Musa, Samweli, Eliya, na Amosi katika Agano la Kale; na Maria, Yosefu, Petro, na Paulo katika Agano Jipya. Kama tunavyosikia katika masomo ya leo, utume wetu ni kufanya mapenzi ya Mungu hata kama kufanya hivyo kunaweza kutuweka katika upinzani na wenye nguvu na matajiri wa dunia au kutuletea chuki na mateso.
Katika somo la kwanza, tunasoma kuhusu Amosi, mtu wa kawaida kutoka ufalme wa kusini wa Yuda ambaye aliitwa na Mungu kuhubiri kwa watu wa ufalme wa kaskazini wa Israeli. Ujumbe wake ulikuwa umeelekezwa kwa matajiri, hasa makuhani wa hekalu ambao walijitajirisha kwa sadaka za maskini bila kuwapa huduma stahiki. Kuhani mkuu Amazia aliposikia mahubiri ya Amosi alikereka. Wakati mwingine tunatenda kama Amazia. Tunakerwa na watu wanaodhihirisha uovu wetu. Tunawachukia watu ambao wana ujasiri wa kutuonyesha makosa yetu. Tunawapenda wanaotuambia kile tunachotaka kusikia hata kama sio kweli. Hii ndiyo sababu wengi wamepita njia ambazo zimewapelekea kupotea. Tumepuuza sauti ya kinabii ya wajumbe wa kweli wa Mungu na badala yake kufuata wale wanaotuliza hisia zetu. Tunataka kuwasikiliza hasa wanapotuambia ni nani maadui zetu na jinsi watakavyotusaidia kupata utajiri wa haraka. Aina hii ya dini inafanya watu wengi kutumia muda mwingi wakikimbizana miujiza badala ya kufanya kazi kujipatia riziki. Je, wewe ni mmoja wa watu kama hao?
Leo pia tunao Amazia wengi ambao wanapigana sana yeyote anayejaribu kufichua utaperi wao. Shida tuliyonayo ni kwamba manabii wa kweli ni nadra kupatikana siku hizi. Tamaa ya mali na madaraka imewafisadi wale waliitwa kuwa wajumbe wa neno la Mungu. Wamefanya maagano na matajiri na wenye mamlaka, ili kupata utajiri na kuwa na ushawishi katika jamii. Paulo anatukumbusha kwamba tumeitwa kuwa watakatifu katika Kristo na tukishiriki katika utume wake kutakatifusha malimwengu.
Katika somo la Injili, Yesu anawatuma wale kumi na wawili aliowachagua kushiriki katika utume kwa mara ya kwanza. Anawaagiza wasichukue mahitaji kwa ajili ya safari bali wamtegemee Mungu. Wasichukue mkoba, mkate, wala pesa bali fimbo na viatu miguuni tu. Walishangaa sana kwa sababu siku zile wasafiri walihitajika kubeba mahitaji ya safari. Lazima walihisi kuwa dhaifu na wanyonge sana. Walipaswa kutegemea mia kwa mia ukarimu wa watu waliowahubiria. Ni pale tu tunapokuwa katika hali ya udhaifu na unyonge ndipo tunapoweza kuzingatia utume ambao Mungu Mungu. Leo, wengi wameacha utume na kutumia muda wao mwingi kukusanya mali na ili kuwa na hakika ya mustakabali wao. Wanawaacha kondoo wakiwa na njaa na kiu ya neno la Mungu kwa sababu wako busy.
Yesu alijua vizuri kwamba wale kumi na wawili wangekutana na changamoto nyingi katika utume wao. Katika sehemu zingine, wangepokelewa vizuri na katika sehemu zingine wangekataliwa. Yesu aliwaagiza kwamba wakikataliwa katika nyumba au mji wasing’ang’anie bali waondoke kwena pengine. Yesu alitaka wanafunzi waelewe kwamba mfumo wa tume wake ulikuwa ni amani. Hawakupaswa kuingia katika mabishano au mapambano bali kuhubiri kwa wale tu waliokuwa tayari kupokea Injili.
Uongofu hauwezi kulazimishwa kwa watu; ni Roho Mtakatifu anayebadili mioyo kwa wakati na njia zake mwenyewe. Msikilizaji anahitaji kuvutiwa na ujumbe na anaposhawishika, afanye uamuzi wa hiari kubadilisha maisha yake. Leo, wahubiri wanatumia njia zote za kuvutia umati, ikiwemo miujiza ya kuigiza wakidai kuponya na kuwatajirisha watu. Hawajali familia au majirani wa watu. Hawajali kile ambacho umati unafanya baada ya makongamano ya upako na miujiza. Hawa watabaki tu umati bila uongofu wa kweli wa kubadilisha jamii, kama vile umati uliomfuata Yesu kwa sababu ya mikate aliyowapa lakini Ijumaa Kuu walipiga kelele wakimtaka asulubiwe.
Wapendwa, neema ya Mungu haina bei. Tunapaswa kutafuta neema hii kwa dhati ya mioyo yetu na matendo ya imani. Sisi sote tumeitwa, tumechaguliwa, na kutumwa kutimiza utume maalum duniani. Je, umepata utume wako Duniani? Je, unafanya jitihada kutimiza utume huu?
Jumapili njema.
Pd. Lawrence Muthee, SVD
