Hekima 1:13-15, 2:23-24; Zaburi 30, 2 Cor 8:7.9.13-15; Marko 5:21-43
Kwa Nini Kuamini

Wapendwa, leo ni Jumapili ya 13 ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa. Kabla ya kutafakari kuhusu masomo ya leo, ningependa tujitafakari kuhusu kwa nini tunamwamini Mungu. Wengi wetu tulipokea imani kutoka kwa wazazi wetu na jamii tulizokulia. Baada ya kuwa na akili za kujitambua, baadhi walielewa imani hii waliorithi na sasa wanaweza kusema kama wakazi wa Samaria kwa yule mwanamke Msamaria katika Yohana 4:41-42, kwamba “sasa tunaamini sio kwa sababu ya yale wazazi wetu waliyotufundisha bali kwa sababu tumesikia wenyewe na kuamini kwamba Yesu ni Mwokozi wa maisha yetu”. Hata hivyo, wengine wengi, kwa sababu mablimbali, hawakuweza kuelewa imani waliorithi lakini badala yake waliiacha kwa kuzingizia uhuru kujiamlia na kujitawala.
Leo ulimwengu umevamiwa na itikadi zinazowachanganya vijana wengi. Wengi wamechochewa kufikiria kwamba hawana haja ya kushikamana na yale wazazi wao waliowafundisha au kuwa vile Mungu alichowaumba wawe. Baadhi ya wenzangu wanaofanya kazi katika nchi za Magharibi waliniambia juzi kuwa watoto wanafundishwa kwamba wana haki ya kuchagua jinsia wanayotaka kuwa wanapokua. Unaweza kuamini hilo?
Imani ni kitu ambacho hatuwezi kulazimisha au kunafiki kuwa nacho. Ni aidha tunayo au hatuna. Baada ya hapo, tunaweza kuitunza hadi ikue kiasi cha kutupa matumaini wakati wowote. Hata hivyo, kwa urahisi, wengi hunafiki wanaamini wakati mioyo yao ipo mbali sana na Mungu. Hii haina faida yoyote bali inakuwa mzigo. Imani kwa Mungu inajengwa juu ya mpango wa Mungu mwenyewe anayejifunua kwa wale walio tayari. Hata wale wanaosema kwamba hawaamini Mungu, wanajua vizuri kwamba kuna mambo kuhusu maisha ambayo ni fumbo kwao kama vile kifo.
Kwa upande mmoja, wale wasio na imani kwa Mungu wanapata ugumu kukubali si tu kifo bali pia changamoto za kawaida za maisha yenyewe. Kwa upande mwingine, wale walio na imani wana Mungu wa kumshukuru kwa mafanikio yao na wa kumkimbilia wanapokumbana na changamoto. Tunapopata maumivu makali au kupoteza wapendwa, tunasema ni mapenzi ya Mungu na tunapata sababu ya kuendelea na maisha yetu. Wale ambao hawamwamini Mungu, wanahusisha mafanikio yao na jitihada zao lakini mambo yasipowaendea vizuri hukata tamaa na kukumbwa na msongo wa mawazo. Baadhi yao hujitoa uhai kwa sababu ya kukata tamaa. Imani ni sehemu ya maisha ambayo ikikosekana maisha yanakuwa magumu, yenye maumivu, na mafupi. Sote tunahitaji sababu ya kuishi na imani kwa Mungu inatupa hii kwa wingi si tu kuishi kwa ajili yetu wenyewe bali pia kwa ajili ya wengine.
Kitabu cha Hekima ya Suleimani kinazungumzia asili ya Mungu. Mungu ni muumba, na daima anafanya kazi kudumisha yote aliyoyaumba. Mungu hana mpango mbaya kwa uumbaji wake bali anaujali na kuudumisha. Uovu unakuja kwetu tunapomgeuzia Mungu mgongo. Alituumba tushiriki katika uhai wake na baadaye turudi kwake katika umilele. Mtume Paulo anaongeza kwamba Mungu hakutuumba kuteseka, bali kupitia neema yake katika Kristo tuishi na kusitawi. Kama watoto wa baba mmoja, tunaitwa kushiriki katika furaha na katika huzuni. Vyote tulivyo navyo ni mali ya Mungu. Anatupa tuwasaidie na kuwashirikisha wengine.
Katika Injili Yesu anatuonyesha manufaa ya kuwa na imani kwake. Imani inaleta matumaini pamoja na hivi viwili vinatusaidia kufurahia mazuri ya maisha lakini pia kuvumilia mabaya. Watu wengi walimfuata Yesu lakini ni wachache tu walioamini kuwa yeye ndiye Masihi aliyetarajiwa. Wale waliomwamini walinufaika na msaada wake. Kiongozi wa Sinagogi alipomkaribia Yesu, hakuwa na shaka kuhusu uwezo wa Yesu wa kumponya binti yake. Yesu hakumuhoji kuhusu imani yake kwa sababu ilikuwa imeandikwa usoni mwake. Tunapokuwa na imani, hatuhitaji kupiga ngoma kuionesha kwa sababu itaonekana katika kauli na matendo yetu.
Yesu alienda naye lakini alicheleweshwa njiani na mwanamke ambaye pia aliamini kuwa yeye ndiye ambaye angemuondolea mateso yake ya muda mrefu. “Nikigusa tu vazi lake, nitaponywa.” Binti ya Yairo alikufa kabla Yesu hajafika, hali iliyotoa nafasi kubwa zaidi ya Mungu kutukuzwa. Majirani walimcheka Yesu aliposema kuwa msichana alikuwa amelala tu. Yesu aliwafukuza wale wote wasioamini kabla ya kumfufua msichana huyo. Ikiwa tunataka kufanikiwa maishani, lazima tuondoe mashaka yote moyoni na kujitenga na wale wasioamini ambao daima hutukatisha tamaa.
Mwanamke huyo hakumkabili Yesu ana kwa ana labda kwa sababu kitamaduni alichukuliwa kuwa najisi kutokana na kutokwa na damu. Mwanamke huyu aliteseka kimya kwa miaka yote 12 bila kumweleza yeyote tatizo lake. Alitegemea imani yake kwa Yesu ambaye alitokea kupita karibu. Katika safari yetu ya imani, tunakumbana na matatizo mengi. Wakati mwingine hatuwezi kupata msaada peke yetu na tunategemea wengine wenye imani kutafuta msaada kwa niaba yetu kama vile Yairo alivyofanya kwa binti yake. Wakati mwingine, lazima tujipeleke wenyewe kwa Yesu kwa sababu wale walio karibu nasi sio waaminifu. Tunapowashirikisha matatizo yetu, wao hutusengenya au kutushauri tutafute msaada kutoka kwa nguvu za giza ambazo huishia kutugharimu mali zetu, kuharibu familia zetu, na hatimaye kuharibu maisha yetu.
Imani ni njia ya maisha na siyo vazi ambayo tunaweza kulivaaa tunapohisi inafaa. Siku hizi, wengi wanatafuta miujiza ya papo kwa papo ili kutibu hali walizolimbikiza kwa muda mrefu. Hali kama umaskini inaweza tu kutibiwa kwa bidii ya kazi na uvumilivu na siyo kwa kuwekelewa mikono katika mikutano ya miuzija. Imani kama hiyo haiwezi kudumu. Miujiza ya papo kwa papo ni kama utajiri wa ghafla, haudumu kwa muda mrefu. Miujiza ambayo Yesu alifanya ilitegemea imani ya mtu. Watu wengi huenda kwa manabii wa siku hizi ili waombewe wakati hawana imani. Kusema kwamba nina imani haitoshi, kauli na matendo yetu lazima yaendane na maneno yetu.
Wapendwa, hebu leo tuchunguze imani yetu na kuona kama ni imara kiasi cha kutupitisha nyakati ngumu. Pia tuwe na moyo wa kuwasaidia wale wenye imani ndogo na kuwasilisha mahitaji yao kwa Yesu. Kwa maombezi yetu na msaada wetu, tunaweza kuwaponya wenzetu.
Jumapili njema
Fr. Lawrence Muthee, SVD
