Masomo ya Jumapili kwa Kifupi: 12 B

Ayubu 38:1.8-11; Zaburi 107; 2 Wakorintho 5:14-17; Marko 4:35-41

Kwa nini unaogopa?

Wapendwa, leo ni Jumapili ya 12 ya Kipindi cha Kawaida mwaka B. Katika somo la leo, Yesu anatufundisha mambo ya ufalme wa Mungu kupitia mafundisho na ishara zake. Kuna hadithi inayosimuliwa kuhusu mkristo mmoja aliyemwalika Yesu aambatane naye katika safari. Hivyo, waliondoka pamoja mapema asubuhi huku yeye akiendesha na Yesu akiwa kwenye kiti cha mbele abiria. Baada ya maili chache, mahali penye njia panda, yule mtu alimuona rafiki yake mmoja mzuri akingojea basi na akasimama kumpa lifti. Alimwambia Yesu arudi kwenye kiti cha nyuma ili yeye na rafiki yake ambaye hajamuona kwa muda waweze kuzungumza. Yesu alitii na kufanya kama alivyoambiwa. Baada ya maili chache zaidi walifika mji mdogo na hapo aliona wanachama wanne wa klabu yake ya mpira wa miguu wakisubiri basi na akasimama kuwapa lifti. Alimwambia Yesu kwamba alitaka kuzungumza na marafiki zake kuhusu mechi yao ijayo na kama hakuwa na shida, aingie kwenye buti. Yesu alitii na kufanya kama alivyoambiwa.

Kisha walifika mji mwingine ulioko juu ya mwa mlima mrefu wenye mwinuko mkali. Waliamua kununua vyakula na vinywaji kwa sababu mbele hakukuwa na miji tena, walikuwa wanaingia kwenye hifadhi ya wanyama. Hivyo, Yesu alirudi kwenye buti na kumwomba Yesu kama angeweza kuachwa kwenye mji huo na kwamba angemchukua katika safari yake ya kurudi. Marafiki wa yule mtu walimcheka Yesu, lakini yeye alitii na kufanya kama alivyoambiwa. Kisha walianza kushuka ule mlima. Katikati ya mlima, yule mtu aligundua kwamba breki za gari zilikuwa hazifanyi kazi na aliwaambia marafiki zake. Kila mtu alianza kuita “Yesu,” “Yesu,”  “Yesu tafadhali tuokoe” lakini hakukuwa na jibu. Walikuwa wamemwacha Yesu juu ya mlima.

Yesu yuko wapi katika maisha yako? Kwenye kiti cha mbele cha abiria? Kwenye kiti cha nyuma? Kwenye buti? Au ulimwacha juu ya mlima? Je, wewe na marafiki zako ambao wamemchukua nafasi ya Yesu katika Maisha yako mnashuka mlima kwa sasa? Je, unaogopa chochote kwa sasa katika maisha yako? Mambo mengi huleta hofu katika maisha yetu kwa mfano, mtu anayesubiri upasuaji muhimu sana anaweza kuwa na hofu kubwa. Mtu anayekaribia kuoa anaweza kuwa na hofu ikiwa ndoa itafanikiwa. Mtu aliyefanya makosa makubwa kazini kwake anaweza kuwa na hofu ya kupoteza kazi. Mtu mgonjwa sana anaweza kuwa na hofu ya kifo. Mtu anayeishi kwa uongo anaweza kuwa na hofu ya kugundulika. Nadhani sisi sote tumepitia nyakati za hofu na wasiwasi katika maisha yetu. Hofu inaweza kutufanya tushindwe kuzingatia majukumu yetu ya kila siku. Hofu inaweza kutufanya vichaa au kutufanya tukimbie huku na huko kutafuta msaada. Hofu ni silaha ambayo shetani upenda sana kutumia. Ukifanikiwa kuingiza hofu kwa mtu au kundi la watu, unaweza kuwatawala na kuwaongoza kufanya lolote. Manabii wa miujiza katika mitaa yetu na vituo vya ibada vya muda wamegundua silaha hii pia. Usidanganywe.

Katika somo la Injili la leo, tunaona jinsi wanafunzi wa Yesu walivyokuwa na hofu kubwa ya dhoruba iliyokuwa karibu kuzamisha mashua yao. Bahari ni maisha yetu na mambo yote yanayotufanya tuogope yanaweza kulinganishwa na dhoruba. Hata hivyo, kinachomvunja moyo Yesu ni kwamba wanafunzi wake wanaogopa sana kuzama wakati wanaye ndani ya mashua, hata baada ya ishara na maajabu yote aliyofanya mbele yao. Anashangazwa sana kwamba bado hawakuamini neno alilowahi kuwaambia awali wala hawakumtambua yeye ni nani.

Kama Wakristo, tunaamini kwamba Mungu ni Emmanueli (Mungu pamoja nasi) na ikiwa ndivyo basi hatupaswi kuogopa chochote mradi tunashika amri zake. Ikiwa tunaye Yesu ndani ya mashua, dhoruba nyingi zinaweza kuipiga mashua yetu kutoka pande zote, lakini itabaki ikielea. Labda uko kwenye njia panda katika maisha yako, ikiwa unaye Yesu ndani endelea kuendesha mashua. Unaweza kuwa umepoteza kazi yako, kuwa na matatizo katika ndoa yako, kutokuwa na furaha katika utume wako kama mtawa, kuteswa na majirani au wenzako kazini, ikiwa unaye Yesu ndani endelea kuendesha mashua rafiki yangu.

Mtakatifu Paulo anatuambia leo “upendo wa Kristo unatusukuma.” Unaweza kuhisi kama kila mtu yuko dhidi yako unapoendeleza wito wako, hii inaweza kuwa jaribio la azma yako kufikia malengo yako. Usikubali kushindwa na dhoruba hata kama zinatoka kwa watu wako wenyewe. Acha upendo wa Kristo ukusukume daima kwa sababu unapokuwa na Yesu ndani ya mashua, dhoruba hazitazamisha mashua yako.

Wengi wetu hatupendi kukosolewa au kupingwa. Tunataka kila mtu akubaliane nasi katika kila jambo. Njia pekee tunavyoweza kupima uvumilivu wetu ni kwa kupita majaribio magumu maishani na kustahimili majaribio mengi. Ikiwa tunapenda mambo yawe rahisi na ya moja kwa moja, huenda tusiwe na nguvu. Yesu aliwafanya wanafunzi wake wapitie majaribio mengi na katika Injili ya Marko; wanaoneshwa kama watu wenye vichwa vigumu waliokuwa wazito sana kumwelewa. Lakini walibaki na Yesu hadi mwisho.

Wapendwa, hebu leo tutafakari mambo yanayotufanya tuogope, na tutafute njia ya kumrudisha Yesu ndani ya mashua ili atusaidie kuvuka dhoruba katika maisha yetu.

Jumapili Njema

Pd. Lawrence Muthee, SVD

Leave a comment