Masomo ya Jumapili kwa ufupi: 11 B

Ezekieli 17:22-24; Zaburi 92; 2 Wakorintho 5:6-10; Marko 4:26-34

Siri ya Ufalme wa Mungu

Wapendwa, leo ni Jumapili ya 11 katika Kipindi cha Kawaida cha Mwaka B. Kipindi cha Kawaida ni wakati wa kujifunza kutoka kwa Bwana wetu Yesu kuhusu tunu za Ufalme wa Mungu. Kwa takriban miaka mitatu, Yesu alihubiri ufalme wa Mungu duniani kwa kutumia mifano mbalimbali ili watu waweze kuelewa vizuri. Leo anatupa mifano miwili inayozungumza juu ya maajabu na usiri wa jinsi ufalme wa Mungu uchipuka na kukua.

Wengi wetu tumewahi kuotesha mbegu au tumeona zikiwa zinaoteshwa. Baada ya hapo, ukuaji wake hadi wakati wa mavuno ni siri kubwa sana. Hata kamera za kisasa zaidi haziwezi kurekodi ukuaji wa mmea. Itakuwa jambo ngumu sana mtu kuchukua kamera na kuanza kurekodi ukuaji wa mimea. Ukuaji wa mimea unnaweza kuonekana mchakato wa taratibu sana lakini tunapolala na kuamka, tunastaajabia kuona miche imechipua, na gafla baadae tayari ni wakati wa mavuno. Ukuaji wa mimea uenda ikawa ni kitu cha kawaida kwetu kiasi kwamba hatuoni ajabu kwake. Sayansi inatueleza jinsi mimea ukua na hata tarakirishi za kisasa zinaweza hata kuiga jinsi inavyotokea. Hata hivyo, kinachotokea kinabaki kuwa siri iliyofichika. Ni furaha kila wakati kuona mimea ikikua, ikiongezeka kwa urefu kila siku, ikichanua maua, na kisha matunda.

Yesu anatumia mfano huu kuelezea jinsi ufalme wa Mungu unavyokua miongoni mwetu. Kazi ya uinjilishaji inafananishwa na kupanda mbegu. Jinsi Kanisa lilivyokua kutoka kwa wanafunzi wachache waliokuwa wamejifunguia kwa hofu ya Wayahudi hadi ilivyo sasa ni siri ya kutafakari. Wito wetu ni kuhubiri Neno la Mungu na kuendelea na kwenda zetu. Jinsi inavyochukua mizizi na kuchipua katika mioyo ya watu binafsi na jumuiya hatujui. Roho wa Mungu anafanya kazi kwa njia yake ya siri na kwa wakati wake mwenyewe ili kufanya Kanisa linawiri. Wakati mwingine mmisionari anaweza asikae katika misioni kwa muda wa kutosha kuona matunda ya kuhubiri kwake, lakini miaka kadhaa baadae nafurahi anaporudi na kuona kile kilichotokana na juhudi zake.

Kwa mfano huu, Yesu anatuhimiza tusikate tamaa wakati utume unaonekana kwenda taratibu na kwa ugumu. Tunaitwa kupanda mbegu za Injili katika mioyo ya wale ambao bado hawajamjua Kristo na mafundisho yake na kumwachia Roho Mtakatifu kuwabadilisha. Mtakatifu Paulo anatueleza kwamba si kwa macho yetu ya kimwili tunaona ukuaji wa ufalme wa Mungu bali kwa imani. Imani hapa ina maana tumaini letu kwa mambo yajayo. Hatupaswi kutafuta matunda ya papo kwa hapo kwa sababu Roho wa Mungu hafanyi kazi hivyo. Wengi wanadanganywa kufikiri kuna njia za kuharakisha kazi ya Roho wa Mungu. Manabii wa kujitangaza wenyewe, ambao wanaahidi mafanikio ya haraka kwa jina la Yesu, wamewaibia matajiri na maskini pesa zao. Roho wa Mungu hawezi kuharakishwa au kupigiwa kelele ili kutenda jinsi manabii wa siku hizi wanavyowadanganya watu.

Mfano wa pili ni kuhusu mbegu ya haradali, ambayo ni ndogo sana kiasi kwamba mtu anaweza asiamini kuwa inaweza kukua na kuwa mmea mkubwa wa kutosha ndege kujenga viota vyao kwenye matawi yake. Haijalishi mbegu ni ndogo kiasi gani, ndani yake kuna uwezo wa kuwa mti. Ikipewa hali nzuri, huota na kuwa mmea. Yesu anatuhimiza kutokata tamaa wakati mambo yanaonekana kuwa madogo sana taratibu kukua. Mwanzo kila wakati ni mgumu na dhaifu. Juhudi za kuhubiri ukweli zinaweza kuonekana dhaifu sana kuweza kushindana na uwongo maarufu katika jamii. Hata hivyo, uvumilivu kila wakati huzaa matunda ya ajabu.

Katika utume wetu, kuna nyakati nyingi za mwanzo, ambazo kwa pamoja huleta ukuaji mkubwa. Wakati mwingine tunakatishwa tamaa tunapoona jinsi hali ilivyo ndogo na dhaifu. Katika parokia yangu, bado tunafungua Jumuiya ndogondogo za Kikristu mpya na wakati mwingine zinaonekana kana kwamba hazitakuwa. Hata hivyo, nimeshuhudia kwamba katika kila moja yao, daima kuna mtu mmoja au wawili ambao wanaendelea kushikilia imani hata wakati wengine wote wanakata tamaa. Mwanzoni, ilikuwa vigumu sana kuona ukuaji Jumuiya hizo hizo. Wengi wao walianza kuadhimisha ibada chini ya mti wakiwa wanakalia magogo makavu na ni mimi na katekista tu tungepokea Ekaristi. Sasa Jumuiya nyingi nyingi kati ya hizo zimejenga makanisa ya muda ya udongo, nyingine zinajenga makanisa ya kudumu. Iadi ya waliobatizwa na wanaopokea Komunyo Takatifu pia imeongezeka sana.

Nimeshuhudia kwamba mara tu mbegu ya imani inapopandwa, inaweza kuchukua hata miaka kadhaa kuota lakini kamwe haiwezi kufa. Je, unaogopa kuanza mambo mapya? Labda katika maeneo yetu kuna baadhi ya miti ya matunda ya kienyeji kama vile maembe, maparachichi, zabibu, maapulo, na mingineyo. Mara nyingi, wale waliopanda hawakukaa muda wa kutosha kula matunda yake. Huenda walihamia maeneo mengine au walikufa kabla. Wale ambao wana bahati ya kula matunda ya miti waliyopanda wenyewe hupata hisia nzuri zaidi ambayo mtu anaweza kutamani. Hivyo, ukuaji polepole wa mambo haupaswi kutukatisha tamaa kupanda miti ya matunda ingawa tunajua kwa hakika huenda hatutakula matunda yake. Ubinafsi unaweza kutufanya tukatae kujaribu au kuwekeza katika mambo mapya.

Wapendwa, ukuaji wa kitu chochote, hata ukuaji wetu ni siri iliyofichika sana. Mungu aliifanya hivyo kwa maksudi. Tusikatishwe tamaa wakati mambo yanaonekana magumu sana, taratibu, na dhaifu. Lazima tubaki waaminifu kwa wito wetu na tumaini katika Bwana anayefanya mambo yakue kwa njia za siri na ajabu.

Uwe na Jumapili njema.

Padre Lawrence Muthee, SVD

Leave a comment