Mwanzo 3:9-15; Zaburi 129(130); 2 Wakorintho 4:13-5:1; Marko 3:20-35
Kuanguka na Ukombozi

Ndugu wapendwa, leo ni Jumapili ya 10 katika Kipindi cha Kawaida. Hata hivyo, katika nchi zingine, leo sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ambayo ilikuwa Ijumaa inaadhimishwa. Kabla ya kutafakari juu ya masomo ya leo, hebu tuseme kidogo kuhusu sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu.
Ibada kwa Moyo Mtakatifu ilianzia katika kipindi cha enzi za kati. Watakatifu kadhaa wanajulikana kuwa walieneza ibada hiyo kama vile Mtakatifu Gertrude, Mtakatifu Margaret Mary Alacoque, Mtakatifu John Eudes, na Mtakatifu Arnold Janssen, miongoni mwa wengine. Ibada kwa Moyo Mtakatifu ina maana ya ibada kwa Yesu katika asili yake ya kibinadamu, hasa ikirejelea moyo kama kitovu cha hisia. Moyo wa Yesu uliwaendea wote waliokuwa na uhitaji, matajiri sawa na maskini. Aliona huruma kwa wagonjwa kama Bartimaeo kipofu (Mk 10:46-52), wenye dhambi kama yule mwanamke aliyeletwa kwake kwa kosa la uzinzi (Yn 8:1-11), na Zakayo mtoza ushuru (Lk 19:1-10), miongoni mwa wengine wengi. Je, moyo wako umuendaa kwa huruma mtu yeyote?
Wakati askari alipomchoma Yesu ubavu, damu na maji vilitoka. Kumwaga damu ina maana ya kutoa uhai, kuacha kuishi, na kujitoa mhanga – kwa kumwaga damu yake Yesu alitoa uhai wake kama fidia kwa dhambi zetu. Kumwaga maji ina maana ya kuhuisha, na kufufua – tunapokuwa na kiu, tunatafuta maji ili kukata kiu chetu. Tunapokuwa na upungufu wa maji mwilini, tunaweza kuzimia au hata kufa. Mimea inapokosa maji, inanyauka na kufa. Kwa kufa msalabani, Yesu alitupa maisha mapya. Moyo ni kiungo Kinachopiga damu kwenda sehemu zote za mwili hivyo kusambaza virutubisho na taarifa muhimu. Moyo ni kitovu cha upendo na imani. Tunawaambia wengine kwamba tunawapenda kutoka moyoni, au tunaamini kwa moyo wetu wote. Je, unamaanisha nini unaposema unapenda kwa moyo wako wote?
Tukirudi kwenye masomo ya leo. Katika somo la kwanza, tunasikia kilichotokea baada ya mwanadamu wa kwanza Adamu, kutomtii Mungu kwa kula tunda alilokatazwa. Macho yake yalifunguka na kuanza kuona uovu, na alijiona uchi akaona na aibu na kujificha. Mambo mengi mabaya hufanyika kwa siri au gizani. Matendo yetu maovu yanapofichuliwa, tunaona aibu na kuepuka kuingiliana na wengine. Adamu alikula tunda lakini Mungu alipomuuliza alimsingizia na kumlaumu mwanamke kwa kosa hilo. Mungu alipomuuliza mwanamke, naye alimsingizia na kumlaumu nyoka kwa kosa hilo. Hivi ndiyo wengi tufanyavyo, kuwalaumu wengine kwa matendo mabaya tunayofanya. Haina maana sana ni nani alimpa nani tunda, lakini ukweli ni kwamba walikula kile walichoambiwa waziwazi wasile, na hata kuonywa kuwa matokeo yake yangekuwa kifo.
Nadhani Adamu na Hawa hawakuelewa maana ya kifo. Sasa wewe na mimi tunajua maana ya kifo – kutengana na Mungu na laana ya milele. Hata hivyo, tunapuuza matokeo hayo na kuchagua uovu. Mchezo wa kulaumiana unaendelea hata leo. Ni watu wachache sana wanachukua jukumu kwa matendo yao. Ni mara ngapi umewalaumu wengine kwa matendo yako?
Hata hivyo, kama mwimbaji wa Zaburi anavyoimba leo, “Bwana amejaa huruma na ukombozi,” Mungu hakuwaacha Adamu na Hawa. Aliwafunika uchi wao na akaanza mchakato mrefu wa ukombozi ambayo ulikamilika katika Kristo Yesu. Tukifanya dhambi, tunaweza kutubu na kuomba huruma na msamaha wa Mungu. Yesu alituachia sakramenti ambazo zinadumisha neema ya Mungu ndani yetu katika safari yetu ya kurudi kwake.
Mtakatifu Paulo katika somo la pili anatuambia kwamba ingawa mwili wetu wa nje unaharibika, mtu wetu wa ndani yaani roho yetu inafanywa upya kila siku. Baada ya Ubatizo, sakramenti zingine zinaendelea kufanya upya roho zetu siku baada ya siku tunapoelekea makao yety ya milele. Sakramenti ya toba ni kurudi kwenye njia ya haki tunapoenda kando. Si muhimu sana kile tunachomwambia padri wakati wa kitubio bali ni mchakato mzima wa kutambua dhambi zetu, ujasiri wa kutubu, kuacha dhambi na kuanza maisha mapya. Kama vipengele hivi havipo, basi kumweleza padri dhambi zetu hakutakuwa na manufaa yoyote katika maisha yetu.
Waandishi katika injili ya leo wamekufuru kwa kusema kwamba Yesu anatenda kwa nguvu za Beelzebuli, mkuu wa pepo waovu. Kukufuru ni kupinga ukweli kwa makusudi na kwa ukaidi. Kwa sababu ya kupigania ukiritimba wa tafsiri ya Torati, ambayo walifanya kwa masilahi yao, waandishi walimchukia Yesu kwa sababu alifungua macho na mioyo ya watu kuelewa torati katika mioyo yao bila waandishi. Leo, aina hii ya tabia inaendelea. Watu wanaopinga ukweli daima watapigana na yeyote anayejitahidi kuutetea. Wengine wangependa watu wabaki gizani kwa sababu ina faida kwao. Je wewe ni mooja wa hao?
Yesu aliwakumbusha waandishi kwamba kosa lao dhidi ya Roho wa Mungu halisameheki. Hii ni kwa sababu ni Roho Mtakatifu anayetekeleza kazi ya ukombozi ndani yetu. Kwa kifo na ufufuo wake, Yesu ametufanya kuwa ndugu zake. Ikiwa tunataka kuwa kweli na uhusiano wa karibu na Yesu, haitoshi kuzaliwa katika familia ya Kikristo, kubatizwa, na kuhudhuria ibada ya Kanisa kama wengine wanavyofikiri. Tunahitaji kusikiliza mafundisho yake na kufanya mapenzi ya Mungu. Je, unajua kama kile unachofanya maishani kinaendana na mapenzi ya Mungu?
Ndugu wapendwa, tunapoingia ndani zaidi katika Kipindi hiki cha Kawaida katika kalenda yetu ya kiliturujia, tusikilize kwa makini mafundisho ya Yesu ili tusije tukapinga Roho wa ukweli.
Jumapili njema.
Fr. Lawrence Muthee, SVD
