Matendo ya Mitume 1:1-11; Zaburi 47; Waefeso 4:1-13; Marko 16:15-20
Hubiri kwa viumbe vyote!

Wapendwa, leo ni Siku Kuu ya Kupaa kwa Bwana wetu mbinguni. Siku kuu hii husherehekewa siku ya arobaini baada ya ufufuko ambayo uangukia Alhamisi kabla ya Jumapili ya saba ya Pasaka. Katika baadhi ya nchi, siku kuu hii huadhimishwa Alhamisi yenyewe. Hata hivyo, kutokana na umuhimu wa wake, mabaraza mengi ya maaskofu yalihamisha sherehe hii hadi Jumapili inayofuata ili iweze kusherehekewa na waamini wote. Leo Yesu anawaaga wanafunzi wake lakini kwa muda tu kwa sababu aliwaahidi kurudi. Alipowaacha, aliwapa jukumu la kwenda ulimwenguni kote na kuhubiri Habari Njema kwa viumbe vyote. Hata hivyo, kwanza aliwaagiza kukaa Yerusalemu mpaka awashushie Msaidizi – Roho Mtakatifu.
Yesu anawapeleka wanafunzi wake waende kuhubiri Injili kwa viumbe vyote. Hii inatukumbusha Mwanzo 1:28 ambapo Mungu alimpa mwanadamu mamlaka juu ya viumbe vyote. Baada ya kuwaumba kwa mfano wake, Mungu aliwakabidhi uumbaji wote. Hata hivyo, baada ya kuanguka katika dhambi mwanadamu alianza kuharibu uumbaji. Mpaka leo, mwanadamu anaendelea kuharibu uumbaji kwa kwa uongo, udanganyifu, vurugu, dhuluma, ukosefu wa usawa, kutokujibika, ubinafsi, tamaa, siasa za chuki, uharibifu wa mazingira, na maovu mengine ambayo yamemteka. Agizo la kuhubiri Habari Njema liliyotolewa kwa wabatizwa wote kuipeleka Habari Njema ya ukombozi kwa viumbe vyote kwa maneno na matendo. Maisha yetu yanapaswa yaeleleze tunu za ufalme wa Mungu. Miti, wanyama, milima, na binadamu wengine wanahisi nini wanapokutana na mimi? Je, wanahisi amani au kutishiwa na uwepo wangu?
Yesu anawaahidi wanafunzi wake kwamba kwa JINA lake, watafanya ishara zile zile alizofanya yeye. Wataweza kutoa pepo, kusema lugha mpya, kushika nyoka hatari bila madhara, kutodhuriwa na sumu, na kuponya wagonjwa kwa kuwawekea mikono. Aliwapa kinga dhidi ya hatari zote watakazokutana nazo katika kuhubiri Injili. Hii ni muhimu sana kwa sababu dunia inapinga kwa nguvu sana Habari Njema. Injili, ufungua macho ya wale wanaoipokea. Hii inamaanisha mwisho wa biashara kwa wale wanaofaidika kwa kuwadanganya wengine.
Ili wanafunzi wawe na ufanisi katika kuhubiri Injili, Yesu anawaahidi zawadi ya Roho Mtakatifu. Kama Wakristo, tunapobatizwa, tunapokea Roho Mtakatifu ambaye hutuwezesha kufanya mambo ambayo Yesu alifanya. Mtakatifu Paulo katika barua yake kwa Waefeso anaelezea jinsi hii inavyofanya kazi: wengine wanaitwa kuwa mitume, manabii, wainjilisti, wachungaji, na waalimu wa ajili ya kujenga mwili wa Kristo ambao sisi sote ni sehemu yake. Hili ufanyika kwa ushirikiano, kila mmoja akitenda kwa dhati kulingana na kipawa chake.
Ushindani hasi tunaoshuhudia leo kati ya Makanisa ni mkakati wa yule mwovu kupinga roho ya ushirikiano. Huduma ya ufalme imechukuliwa na tamaa na udanganyifu. Ahadi ya utajiri wa haraka bila kufanya kazi kwa bidii ni ya kuvutia sana, hasa kwa vijana. Miujiza ya haraka kwa kila tatizo duniani ni biashara inayokua haraka sana leo. Mkakati wa biashara hii ni kuwachanganya akili wateja ili watake zaidi na zaidi. Ili kuifanya bidhaa iwe ya kuvutia zaidi, wanatumia mbinu zozote ikiwa ni pamoja na maigizo na sarakasi.
Kwa watu ambao hawataki kufuata njia ndefu na ngumu ya kupata “maisha mazuri” kwa kufanya kazi kwa bidii, miujiza ni njia ya mkato. Hata hivyo, njia ya uhakika ya mafanikio ya kweli na ya kudumu ni ile iliyowekwa na Mungu tangu uumbaji na kufanywa upya katika Kristo: “mkaitiishe dunia” (Mwa 1:28). Je, wewe ni mmoja wa wale wanaotafuta utajiri wa haraka?
Wapendwa, Mungu ametupa hekima ili kutusaidia kufaidi mema ya Dunia aliyoyaumba kwa ajili yetu. Tusiharibu dunia ili kupata utajiri wa haraka ambao haudumu. Mafanikio ya haraka yana muda mfupi sana wa matumizi. Jichunguze mwenyewe na uone muda gani miujiza inayofanywa mitaani, nyumbani kwa nabii, na katika vibanda vya miujiza. Je, utadanganyika?
Jumapili yenye Baraka.
Pd. Lawrence Muthee, SVD
