Masomo ya Jumapili kwa Kifupi: 4 Pasaka B

Matendo 4:8-12; Zaburi 118; 1 Yohana:1-2; Yohana 10:11-18

oppo_0

Mchungaji Mwema

Wapendwa, leo ni Jumapili ya nne ya Pasaka, ambayo pia inajulikana kama Jumapili ya Mchungaji Mwema au Miito. Kanisa leo linasherehekea miito ya upadri, maisha ya Kitawa, na maisha ya Ndoa. Leo msisitizo upo katika kuhamasisha miito ya upadri na maisha ya kitawa kwa sababu mavuno yanazidi kuongezeka lakini wafanyakazi wanazidi kupungua. Hata hivyo, bila familia imara katika imani hatuwezi kupata miito ya upadri na maisha ya kitawa. Ni muhimu sana kusisitiza pia umuhimu wa maisha ya ndoa.

Katika Injili ya leo, Yesu anajitambulisha kama mchungaji mwema ambaye ana anawajali sana kondoo wake. Analinganisha mchungaji mwema na mfanyakazi wa kulipwa ambaye masilahi yake mkuu si usalama wa kondoo bali mshahara. Yesu ni mchungaji ambaye hakuogopa kutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo zake. Huyu ndiye jiwe lililokataliwa na Wayahudi lakini, kama Petro anavyowaambia, amekuwa jiwe kuu la pembeni. Wazazi pamoja na viongozi wa kidini wana jukumu sawa la kuwaongoza watoto wa Mungu. Wazazi wanatakiwa kuhakikisha kuwa watoto wao wanapata lishe bora ya mwili, roho, na akili. Viongozi wa kidini wanatakiwa kutoa lishe bora ya kiroho kwa watu.

Katika Yesu, upendo wa ajabu wa Mungu unadhihirishwa kwa ulimwengu mzima. Ametufanya watoto wake kupitia mateso, kifo na ufufuko wa mwanawe mpendwa. Hatimaye, wale wanaomwamini na kuishi kulingana na mapenzi yake watakuwa kama yeye. Upendo huu wa Mungu unatakiwa kuonekana pia kwa wazazi, makuhani, na watawa.

Kanisa ni la kimisionari ndani na nje. Wakristo wote waliobatizwa wametumwa kuwa wamisionari kwa wengine kwa kuhubiri Habari Njema ya Ufalme kwa maneno na matendo. Makuhani na watawa wamisionari haswa wametumwa kuwaleta watoto kwa ufalme wa Mungu. Wazazi wametumwa kuleta watoto duniani kwa kushirikiana na Mungu. Maandalizi mazuri ni muhimu sana ili wale wanaokubali miito hii waweze kushinda changamoto nyingi zinazohusika. Leo tunaona watu wengi wakiacha ndoa, upadri, na maisha ya kitawa. Watu wanaopenda miito yao wanaacha kwa sababu hawana vitendea kazi au mafunzo ya kutosha ya kupambana. Shetani na mawakala wake anatusukuma tuanguke chini ya uzito wetu wenyewe kwa sababu hana uwezo wa kutuondoa kutoka kwa miito yetu. Anatuudhi na kutufanya tuwe na mashaka ili tuache. Rafiki, simama imara na utaona kwamba shetani na mawakala zake hana nguvu juu yako?

Kuhani mwema, mtawa, au mzazi anajali kweli kundi lake na yuko tayari kutoa hata uhai wake kwa ajili yao. Mchungaji mwema haogopi mbwa mwitu wanaotishia maisha ya kondoo. Mbwa mwitu hawa wanakuja wamejificha au kama sehemu ya kundi au kama wachungaji wakitafuta wakati mwafaka wa kula kondoo. Mchungaji mwema daima husema ukweli kwa kondoo wake, anawapa fursa za kujifunza kutokana na makosa yao ili waweze kukua. Nimeona viongozi wa Jumuiya za kitawa na wanandoa wengine ambao wana tabia kama marefa kwenye mechi ya mpira wa miguu. Mara zote wanakimbia uwanjani kote wakitafuta makosa na wanapoona moja, wanapiga filimbi, kuadhibu, na hata kuwafukuza wachezaji kutoka uwanjani. Mchungaji mwema ni yule anayetibu wagonjwa na kuwarudisha kundini kondoo waliopotea.

Watu uingia katika maisha ya ndoa ili wawe wachungaji wa watoto wanaowaleta ulimwenguni. Wazazi wanaitwa kuwa wachungaji wanaolisha familia zao kimwili na kiroho na kuhakikisha usalama wao. Hata hivyo, kuna baadhi ya wazazi ambao wamegeuka kuwa wakatili kwa watoto wao. Hii inaonyesha upungufu mkubwa wa maandalizi na mafunzo kabla ya ndoa na malezi katika safari ya ndoa. Watu wengi wanateseka bure katika ndoa kwa sababu hawakujipanga vizuri au hawana mahali pa kujipatia malezi na makuzi ya kindoa. Lakini, Kanisani kuna fursa na vyanzo za kutosha kurekebisha hali zozote kupitia Sakramenti, Neno, vyama vya Kitume, na Jumuiya Ndogondogo za Kikristu. Ikiwa tutajitenga na chemchemi ya neema, hivi karibuni itatupungukia na changamoto zitatuzidi nguvu. Usiogope kutafuta msaada.

Tunaposherehekea na kuhamasisha miito Kanisani, tuzingatie kwa karibu kinachoendelea kila siku katika utume na familia zetu na kukarabati mahali pana mapungufu mapema. Katika nafsi zetu, tujitazame na kujiuliza iwapo tunajali na kupigania miito yetu au tunaishia  kuacha kwa sababu ya kukatishwa tamaa au kusukumwa na watu au hali.

Jumapili njema.

Pd. Lawrence Muthee, SVD

Leave a comment