Matendo 3:13-15.17-19; Zaburi 4; 1 Yohana 2:1-5; Luka 24:35-48
Aliwafundua Akili Zao

Wapendwa, leo tunaanza wiki ya tatu ya Pasaka. Kipindi hiki kirefu cha Pasaka ambacho kina wiki 7 kinatusaidia kuelewa maana ya ufufuko wa Yesu na kwa nini ni jambo hili ni la msingi kwetu sisi Wakristo. Masomo katika kila kipindi cha kalenda ya liturujia ya Kanisa yameandaliwa kutuelimisha kuhusu mpango wa Mungu wa wokovu wa binadamu ambao kilele chake kilikuwa kufufuka kwa Yesu kutoka kwa wafu.
Katika Injili leo, Yesu anafungua akili za wanafunzi wake ili waweze kuelewa Maandiko na matukio yaliyotokea. Kisha aliwatuma kuuhubiri ujumbe huu kwa mataifa yote. Wale wanaopokea Injili wanahitajika kutubu dhambi zao na kubatizwa.
Katika somo la kwanza, Petro aliyejawa na Roho Mtakatifu anatoa anahubiri habari njema ya ufufuko kwa ujasiri na shauku ya kipekee. Hana hofu ya kuwaambia Wayahudi kwamba walikosea kumtundika Yesu msalabani Bwana wa uzima mwenyewe. Kwa ujinga wao, Mungu alitimiza mpango wake wa kuleta wokovu wa milele kwa mataifa yote. Sisi pia mara nyingi tunafanana na Wayahudi, tunachochewa kutenda uovu dhidi ya majirani wasio na hatia kwa sababu hatujui ukweli. Hata hivyo, Mungu hugeuza uovu wetu kuwa baraka kwao. Mara ngapi nimechochewa kuwa na chuki, kusema mabaya, au kuumiza mtu au watu wengine?
Katika somo la pili, Mtakatifu Yohana anatukumbusha kwamba Kristo ni mpatanishi wetu wa kudumu mbele za Mungu. Hili linahubiriwa kwetu kila siku ili tuweze kuwa wenye haki na kufikia uzima wa milele. Ikiwa tutatenda dhambi, hatuhitaji kukata tamaa kwa sababu Kristo anatuombea kwa Baba. Tunachohitaji kufanya ni kutubu na kukiri dhambi zetu. Ushahidi pekee unaodhibitisha kwamba tunamjua Mungu ni kuishi kadiri ya mpango na mapenzi yake. Je! Naishi kadiri ya mapenzi na mpango wa Mungu?
Kuelimisha maana yake ni kufungua akili ya mtu na kumfanya aweze kufikiri kwa uangalifu na kuelewa mambo. Yesu alifungua akili za wanafunzi wake kuelewa Maandiko na kisha kuwatuma kuwafungua akili watu wote. Huwezi kufungua akili za wengine ikiwa akili yako mwenyewe haijafunguliwa. Katekisimu sahihi ndiyo njia pekee ya kuhakikisha tunafungua akili zetu kuelewa njia za ufalme wa Mungu. Hata hivyo, leo watu wengi wanataka kubatizwa na kupokea sakramenti zingine lakini hawapo tayari kufuata mafundisho ya katekisimu. Matokeo yake ni kuwa na wabatizwa wengi lakini waumini wachache.
Utume wa misionari ni kufungua akili za watu kuelewa vizuri misingi ya imani na kwa kushawishika waweze kuyabadilisha maisha yao kuendana na mising hiyo. Si kazi rahisi, hasa wakati watu wanaogopa kuacha mila zao. Ili kuacha njia za zamani, lazima mtu awe na uhakika kwamba njia mpya anayoikubali ni sahihi. Kwa imani hii, mtu atakuwa tayari kustahimili matokeo kama vile kutengwa na marafiki au na familia. Kuikumbatia Injili inamaana kuondokana na njia za zamani za kufanya mambo na kushikilia njia mpya. Tunapaswa kuondoa vazi la zamani. Hii inaweza kutufanya tukose amani na kuogopa kwamba uchi wetu utaonekana. Wengine wanakataa kuachilia vazi la zamani ambalo ni mifumo ya maisha, desturi, mila, imani, na tabia. Hii inapelekea kile wanateolojia wanakiita sinokretismu, au mchanganyiko wa imani tofauti, tamaduni, au mafundisho. Utawaona watu walio batizwa wakiwa wakeleketwa mahiri wa maadili yanayopingana moja kwa moja na maadili ya Injili.
Wengine wamejaribu kutengeneza njia za mkato kwa kuhubiri wokovu wa haraka ili kupata utajiri wa haraka. Hata hivyo, kwa yeyote anayejali kuchunguza hili ni wazi kwamba njia hizo hazina mafanikio ya kudumu kwa yeyote. Ikiwa kuna chochote, mafanikio haya ya udanganyifu yanadumu kwa muda mfupi tu. Yesu alimwambia Nikodemo kwamba lazima mtu azaliwe mara ya pili. Hatuwezi kufunika mavazi yetu ya zamani na mapya, lazima yataonekana tu. Yesu alituonya tusiweke divai mpya katika viriba vya zamani au kipande cha nguo mpya kwenye vazi la zamani. Lazima tuache ngozi yetu ya zamani ikiwa tunataka kuzaliwa upya katika Kristo. Si kazi rahisi, lakini ni njia pekee ya uhakika ya kupata matunda ya ukombozi wetu. Je! Natafuta utajiri rahisi na wa haraka bila kulazimika kufanya kazi? Je! Nilipata katekesi sahihi kuhusu mambo ninayoamini? Ni mambo yepi katika imani yangu ambayo nahitaji kujifunza zaidi?
Wapendwa, ujumbe wa leo juu ya mabadiliko ya kweli. Ikiwa hatuachi mavazi yetu ya zamani ambayo ni mambo yanayopingana na mapenzi na mpango wa Mungu, tusijigambe kwamba tuna imani kwa Mungu. Maadili yote, mabaya au mazuri, huwa tunajifunza. Ili kubadilika, lazima tuache yale mabaya na kushikilia yale mema ambayo Yesu anatufundisha. Mtu yeyote asikwambie kuna njia ya mkato ya kupata neema za Mungu. Njia pekee ni kujua na kuishi maadili ya Injili.
Jumapili yenye Baraka
Pd. Lawrence Muthee, SVD
