Masomo ya Jumapili kwa Kifupi: Dominika ya 2 ya Pasaka B
Matendo 4:32-35; Zaburi 117(118); 1 Yohana 5:1-6; Yohana 20:19-31
Ushahidi wa ufufuko wa Yesu

Wapendwa, leo ni Jumapili ya pili ya Pasaka. Kalenda ya liturujia hutupa siku 50 za kusherehekea fumbo la Pasaka ambalo hufikia kilele chake katika sherehe ya Pentekoste. Ni muhimu kutafakari matukio ya wiki iliyopita kwa makini ikiwa tunataka kuelewa maana ya imani yetu ya Kikristo. Yesu alikuja duniani kutuletea habari njema kuhusu ufalme wa mbinguni na jinsi ya kufika huko. Tunaweza kumlinganisha Yesu na mchungaji mwenye ukarimu ambaye baada ya kupata mahali penye malisho mengi wakati wa kiangazi, anarudi na kuwaambia wenzake kijijini kuyahusu na kuwapeleka. Wengi wetu tusingependa kushirikisha wengine habari hizo lakini badala yake tungepeleka mifugo yetu kule usiku wa manane ili wengine wasigundue malisho hayo. Wengi wetu tunafikiri kwamba tunaposhirikisha wengine, tunapoteza, lakini kinyume chake, kushirikishana kunazidisha kile tunachoshirikishana.
Somo la kwanza leo kutoka kitabu cha Matendo ya Mitume linaangazia sifa za jumuiya ya kwanza ya Kikristo. Ni jumuiya ambapo wanachama wake walikuwa na moyo mmoja na roho moja. Waamini wote walitoa mali zao kwa ajili ya wote. Uwepo wa neema ya Mungu unaonekana kwa kila mwanajumuiya. Kuna mithali kadha wa kadha katika tamaduni tofauti inayohamasisha roho ya umoja na kushirikiana. Kwa Kiswahili, msemo unasema, “Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu.” Je! ni mara ngapi mimi utumia muda, mali, maarifa, na vipaji vyangu, kwa faida ya wengine?
Wimbo wa Katikati kutoka kitabu cha Zaburi unakumbusha kwamba Mungu ametupa mfano wa kuiga. Kwa rehema yake isiyo na mwisho, Mungu alitupa Mwana wake pekee kutuokoa kutoka utumwa wa dhambi. Anaendelea kututia moyo katika mapambano yetu ya kila siku. Anaweza kubadilisha hali zetu ngumu na kuyafanya ziwe fursa za furaha na mafanikio. Wale waliokataliwa anawafanya kuwa watawala na wanyonge anawainua juu. Mungu anaweza kugeuza udhaifu wetu kuwa nguvu ikiwa tutamwomba. Hata hivyo, ushirikiano wetu ni muhimu kwa sababu Mungu si mchawi wala mwanasarakasi. Wengi wanataka Mungu awafanyie miujiza bila wao kushughulika kufanikisha lile wanalotaka. Je, wewe ni mtu kama huyo?
Yohana katika barua yake ya kwanza anatuambia kwamba hatuwezi kudanganya kwamba tunampenda Mungu. Njia pekee ya kuonyesha kwamba tunampenda Mungu na Mwana wake Yesu ni kwa kufuata amri zake tu. Amri za Mungu si mizigo ya kutuadhibu bali ni silaha ya kushinda dunia. Kushinda dunia si rahisi bila msaada wa Mungu. Tunahitaji mara kwa mara msaada wa Mungu katika hali zetu zote. Hata hivyo, wengi wanadanganywa kupeleka pesa zao kwa manabii wa siku hizi ambao wanadai wana suluhisho kwa matatizo yote.
Katika Injili, hata hivyo, Yesu anaonekana kuficha ushahidi wa ufufuko wake kwa wote isipokuwa kwa wanafunzi wake wa karibu tu. Hii ni ngumu kuelewa. Kazi ya kuhubiri Kristo aliyefufuka kwa ulimwengu imekuwa ngumu sana kutokana na jinsi Yesu alivyochagua kujifunua mwenyewe. Kwa nini hakwenda katikati ya mji wa Yerusalemu na kuonyesha wote waliomuua kwamba alikuwa hai? Ikiwa ingekuwa leo, Je, Yesu angerusha ufufuko wake kwenye mitandao ya kijamii au kutangazwa katika vyombo vya habari vya dunia kama habari ya hivi punde?
Yesu alikataa kujionesha kwa kila mtu isipokuwa kwa wale waliomwamini tu. Alihitaji habari ya kufufuka kwake iwe inasimuliwa na watu wenye uaminifu na siyo vyombo vya habari ambavyo mara nyingi hupotosha ukweli ili kuendana na masilahi ya kibiashara au kisiasa. Ni muhimu sana kuchagua ni nani tunayeruhusu kusimulia habari zetu. Tunaelezwa kwamba Wayahudi walilipa fedha nyingi kwa maaskari waliolilinda kaburi ili washuhudie uongo kuhusu kilichotokea siku ya ufufuko. Ilikuwa kazi ngumu na hatari kwa wanafunzi kumuuhubiri Bwana mfufuka kwa watu wale wale waliomuua. Hakuna mtu angewaamini. Uongo wa askari ulikuwa na uaminifu zaidi kuliko maneno maneno ya wanafunzi. Hata hivyo, kwa nguvu ya Roho Mtakatifu waliyopewa, walifanikiwa kuwabadilisha wengi. Labda kuna watu waliolipwa pesa nyingi kuharibu sifa yako au kushinikiza upoteze ajira yako, usikate tamaa, mwamini Roho Mtakatifu, hawatafanikiwa. Yule mwovu na mawakala zake hawana uwezo wa kutuangamiza, wanatufanya tutumie uzito wetu wenyewe kujiangamiza. Wanataka tukate tamaa na kujiondoa sisi wenyewe kwa sababu hawana nguvu juu yetu. Simama imara kwa imani uone jinsi watakavyotokomea maishani mwako.
Yesu aliendelea kujidhihirisha kwa wanafunzi wake kuwaimarisha walipokuwa wanakata tamaa. Ni Yesu pekee anayeweza kujidhihirisha kwa wale ambao amechagua mwenyewe. Tusingemtambua kama yeye mwenyewe asingetaka. Mwanzoni Maria Magdalene alipoona Yesu bustanini, alidhani ni mtunza bustani. Ni Yesu aliyejifunua kwake kwa kumwita kwa jina lake. Yesu alipojitokeza kwa wanafunzi wawili waliokuwa wakirejea kijijini mwao kwa huzuni na kukata tamaa, walimtambua tu katika kuumega mkate. Yesu aliporudi kwa Petro na marafiki zake waliporudia kazi yao ya zamani ya kuvua samaki wakidhani kwamba yote yalikuwa yamekwisha, ajijidhihirisha yeye mwenyewe kwa muujiza wa kiasi kikubwa cha samaki. Leo tunasoma jinsi alivyoonekana kwao na kuwapa zawadi ya amani ili kuushinda uoga uliowakumba.
Yesu alirudi baada ya wiki moja kujidhihirisha kwa Tomaso ambaye hakuwepo alipojitokeza mara ya kwanza. Aliondoa mashaka yake na kumtia nguvu. Hii inaonesha jinsi Yesu alivyomjali Tomaso na sisi sote. Hakutaka mashaka yake yamzidi nguvu. Yesu atarudi mara nyingi kutusaidia kwa sababu anatupenda na kutujali kila mmoja wetu tunaomwamini. Katika safari yetu ya imani, ni lazima tupate mashaka mengi. Tusikate tamaa kwa sababu Yesu hataruhusu wale wake wazindiwe na mashaka.
Leo wapendwa, nawakaribisheni tuchunguze maisha yetu kwa kina na kuona kama kuna ushahidi wa kutosha kwamba sisi ni wafuasi wa kweli wa Kristo. Je! Tunampenda kweli Yesu kwa kuwa, au tunamtaka tu atatue matatizo yetu? Tunaweza kujionyesha kwamba sisi ni wafuasi wa Kristo, lakini hatuwezi kuidanganya dhamiri yetu wenyewe. Imani katika Bwana aliyefufuka ni silaha ya kweli ya kushinda changamoto za ulimwengu huu.
Jumapili njema
Fr. Lawrence Muthee, SVD
