Jeremia 31:31-34; Zaburi 51; Hebrania 5:7-9; Yohana 12:20-33

Kuvunjika na kufunguka
Wapendwa, leo ni Jumapili ya tano katika kipindi hiki cha Kwaresima. Jumapili ijayo itakuwa Jumapili ya Matawi na mwanzo wa Wiki Takatifu. Tunakaribia kilele cha mfungo wetu Kwaresima. Tumefika mbali katika safari yetu ya kuandamana na Yesu katika njia yake kuelekea msalabani. Tunatamani kwenda Golgotha pamoja naye ambapo yote yatakamilika na zaidi ya hayo tunatamani kusherehekea kufufuka kwake tuimbe aleluya na utukufu juu kwa Mungu tena.
Katika maisha yetu, tunafanya maazimio na mapendekezo ya kukabiliana na matatizo na changamoto zinazotukabili. Hata hivyo, sote tunajua kwamba changamoto kubwa zaidi huja wakati wa kutekeleza maazimio na mapendekezo hayo. Changamoto ni kwamba hatuko tayari kutoa sadaka inayohitajika kuyatekeleza. Je, una kumbuka baadhi ya maazimio uliyofanya muda fulani uliopita ambayo hujayaanza hata kutekeleza, kama vile kupunguza uzito, kuhudhuria sala za jumuiya, kufunga, kuwai kanisani, kuacha pombe, nk?
Mungu ni tofauti na mwanadamu. Yeye daima hutekeleza ahadi zake kwa wakati sahihi bila kujali gharama zake. Kupitia nabii Yeremia, Mungu aliwaahidi watu wa Israeli kuanzisha agano jipya nao baada ya kuharibu agano la kwanza kwa kutokutii kwao. Hata hivyo, agano hili jipya litakuwa tofauti na la kwanza. Agano la kwanza lilikuwa la pamoja ambapo mafanikio ya mtu binafsi yalitegemea utii wa pamoja wa jumuiya yote. Hapa watu wasio na hatia hasa maskini waliteseka kwa sababu ya maamuzi mabaya yaliyofanywa na matajiri na wenye nguvu. Katika agano jipya, kila mtu atamjua Mungu na amri zake zitakuwa moyoni mwake. Kwa hivyo kila mtu pia atatoa hesabu ya matendo yake mwenyewe. Agano hili lilifanikiwa katika Kristo Yesu na katika ubatizo wetu, tumelikubali.
Tulipobatizwa, wazazi wetu au sisi wenyewe tulifanya ahadi za ubatizo. Hizi ni ahadi ambazo zitahusika katika wokovu wetu wa sasa na wa mwisho. Hata hivyo, Jumuiya ni muhimu kwa sababu ni kama mlezi wa maadili na wanajumuiya wenzetu hutuweka bidii na motisha ya kuyafuata. Lakini jukumu ni la kila mtu kutimiza ahadi zake kwa Mungu. Ikiwa tunaahidi kuishi ahadi zetu za ubatizo kisha kuzipuuza baadaye, tutawajibika kwa hilo kama binafsi SAA ya mwisho itakapofika.
Kufanya ahadi ni rahisi lakini kuishi ni kazi ngumu. Tunapokuwa na furaha tunaweza kuahidi mambo mengi lakini kuyatekeleza inakuwa ngumu. Tunapoingia katika changamoto tunaweza kuahidi mambo mengi ili kupata msaada, lakini baadae inakuwa changamoto kutimiza ile ahadi. Katika somo la pili, tunasikia kwamba ilikuwa vigumu kwa Yesu pia alipokabiliwa na mateso yanayotarajiwa na kifo. Yesu aliomba Baba ili kikombe hicho cha mateso kipite kwake lakini alikuwa tayari kufanya mapenzi ya Baba yake kwa ajili ya lile alilolitarajia, yaani utukufu wa milele. Kuwa na shida katika kutekeleza ahadi tunazoweka ni jambo la kawaida, lakini Yesu anatufundisha tusikate tamaa bali tumtumainie Mungu ambaye anatupa nguvu.
Tunaweza kuwa na ari sana tunapochagua kutekeleza kazi fulani ngumu lakini wakati SAA inapofika, ujasiri wote unaonekana kupotea kama moshi hewani. Yesu anazungumzia “Saa Yake” kwa shauku kubwa. Anajua kwamba ingawa saa hiyo ingekuwa ngumu, ilikuwa njia pekee ya kupata utukufu alioahidiwa na baba. Alijua kwamba kama nafaka ilibidi aanguke chini, azikwe, na kuvunjika ili atoe miche na kuzaa matunda. Sote tunapenda maisha yetu na tungependa kuyahifadhi kadiri tuwezavyo, hata hivyo, Yesu anatufundisha kwamba kuna wito mkubwa zaidi kuliko kuhifadhi maisha yetu duniani. Ufalme wa Mungu unatokana na sadaka ya mwisho ya maisha yetu.
Yesu anatuhakikishia kwamba ikiwa tunamwiga na kumfuata, mahali alipo sisi pia tutakuwepo siku moja. Hatimaye, Yesu anafanya sala ya mwisho kwa Baba yake ili kumtukuza. Kutoka wakati huo, Yesu alipata ujasiri wa kushangaza wa kukabiliana na msalaba wake. Mungu alimfunulia na kumhakikishia utukufu mwishoni mwa sadaka yake. Sadaka hii ilikuwa kwa ajili ya kuharibu giza la yule muovu. Huyu hakuwa akikubali kushindwa bila mapigano. Sisi pia tunahitaji hakika kama hiyo ya Yesu ili kutekeleza jukumu letu licha ya changamoto tunazokumbana nazo. Mkuu wa giza yupo na hai na mwenye bidii katika utume wetu kila siku. Anakuja akiwa amejificha katika nyuso nyingi. Mapambano yetu lazima yatolewe kwa Mungu ambaye utupa nguvu na ujasiri wa kupigana hadi mwisho.
Mungu ameumba kila mmoja wetu akiwa na uwezo fulani ndani yake. Ili kuchipua uwezo huu, tunahitaji kukubali kuvunjika kwanza kama vile mbegu yoyote. Lakini, wengi hufa bila kutumia uwezo wao kwa sababu wanahofia kuvunjika na kuchipua. Wengi huishi maisha ya wafungwa kwa sababu wanahisi kwamba ikiwa watajitokeza, wanaweza kupoteza usalama wao na kuwa hatarini. Yesu alihofia kuvunjika, lakini alipata ujasiri kupitia sala kwa Baba ambaye alimtia nguvu. Watu wengi sana hujitoa uhai kwa sababu hawana mtu wa kuwatia moyo ili wakubali kuvunjika na kuchipua. Wengine wanaishia kufanya maamuzi mabaya kwa sababu hawana mtu wa kuwashauri, au wanadanganywa na wale ambao hata hawajali uwezo wao. Je, unahofia kuvunjika na kuchipua kwa sababu hauamini mtu yeyote katika maisha yako?
Wapendwa, nawakaribisha leo tuchunguze maisha yetu na tuone kwanza ikiwa tunatimiza ahadi zetu kwa Mungu na wenzetu. Pili ikiwa tunaujasili wa kutaka kuvunjika na kuchipua vipaji na uwezo ulioko ndani yetu. Hakuna kitu kizuri kinachokuja bila changamoto.
Uwe na Jumapili Njema
Pd. Lawrence Muthee, SVD
