Masomo ya Misa kwa kifupi: Jumatano ya Majivu

Joeli 2:12-18; Zaburi 51; 2 Wakorintho 5:20-6:2; Mathayo 6:1-6.16-18

Wapendwa, leo tunaanza kipindi cha Kwaresma, kipindi cha kipekee kwa Wakristo. Jumatano ya Majivu ni mojawapo ya siku za lazima kwa kila Mkatoliki kwenda Kanisani kupokea majivu kichwani kama ishara ya kuanza siku 40 za sala, kufunga, toba, na kutoa sadaka. Pia ni siku ya lazima kufunga kwa wale walio na umri wa zaidi ya miaka 18 na chini ya miaka 60. Kila Ijumaa wakati wa Kwaresma, tunasali Njia ya Msalaba kuwakumbusha mateso aliyoyapitia Yesu kutuokoa. Wakati wa kufunga, ruhusa hutolewa kula mlo mmoja kamili kwa siku na milo mingine miwili midogo ambayo pamoja haifiki mlo kamili. Sheria ya Kanisa inasema, “Funga Jumatano ya Majivu na usile nyama Ijumaa Kuu”. Kufunga ni pamoja na kupunguza ulaji wa chakula, na tunachofunga kinaweza kutolewa kwa wale wasio nacho. Kwaresma pia ni wakati wa kuongeza sala, hasa kwa kuzingatia toba na kutafuta rehema ya Mungu kwa mapungufu yetu yanayotufanya tujitenge naye. Hatimaye, na muhimu zaidi, Kwaresma ni maandalizi ya Pasaka, sherehe muhimu kwa Wakristo wote ambapo Yesu alishinda mauti na kutuletea ukombozi wa milele.

Kufunga, kusali, kujipaka majivu, na kutoa sadaka zote ni ishara na alama za nje za kutubu. Kufunga kimwili pekee haina maana ikiwa hatujajitahidi kuepuka dhambi, kama alivyosema Mt. Basil wa Caesarea. Tunahimizwa kufunga maovu yote wakati  wote wa Kwaresma ili kufikia Pasaka, tutakuwa tumefanya mazoezi ya kutosha kuacha uovu wenyewe.

Kusali haimaanishi kwenda Kanisa tu wakati wa Kwaresma kama watalii. Badala yake, ni jaribio la makusudi na endelevu la kujiunganisha na Mungu ili kuwa na uhusiano mzuri naye. Ni wakati tunapojiombea sisi wenyewe, watu wengine, na ulimwengu wote kwa jumla. Sala mara kwa mara huongeza ufahamu wetu wa uwepo wa Mungu ndani yetu, hivyo kutusaidia kutenda kwa haki. Tukisahau au kufifisha uwepo wa Mungu, tunageukia njia mbaya bila kuhisi kosa. Tuombee  nchi zinazozozana duniani kwani mizozoz hiyo inatuathiri kwa njia moja au nyingine.

Majivu ni ishara ya kutubu na kufanya upatanisho. Kitabu cha Yona sura ya tatu (siyo somo la leo) kinasema watu wa Ninawi walivaa gunia na kuketi kwenye majivu kama ishara ya kutubu baada ya onyo la kuangamizwa kutoka kwa nabii Yona. Mfalme pia alitangaza kufunga kwa watu wote pamoja na wanyama (Yon 3:6-9). Majivu pia utukumbusha kwamba tumetolewa kwenye mavumbi na tutarudi mavumbini lakini roho zetu zitasimama mbele ya hukumu (Mwa 3:19). Tulizaliwa uchi na bila mali yoyote isipokuwa mwili wetu wenyewe. Tunapokufa, miili yetu itazikwa kwenye mavumbi, na baada ya miezi kadhaa, tutageuka tena kuwa mavumbi. Hii pia ni ukumbusho mzuri kwetu katika shughuli zetu za kila siku kutojivuna kwa mafanikio yetu ya kibinadamu wakati tunawakanyaga wale wasio na bahati.

Kutoa msaada ni ishara ya mshikamano tunayojifunza kutoka kwa Yesu mwenyewe. Hatuwasaidii wengine kwa sababu sisi ni matajiri bali kwa sababu inatuhusu kuwaona wanateseka na wanahitaji msaada. Sote tunahitaji msaada wakati fulani katika maisha yetu, hadi kifo. Tunapotoa msaada, tunahimizwa kufanya hivyo kwa heshima. Thamani ya wahitaji haiipunguzwi kwa njia yoyote kwa sababu ya matatizo yao.

Katika somo la kwanza, Nabii Yoeli anatukumbusha kuwa uongofu wa moyo ndio unahitajika kwetu wakati huu na siyo maonyesho ya nje. Pia anatukumbusha kwamba Mungu daima ni mwenye huruma kwa wale wanaojirudi na kutubu. Mungu anataka kuturejesha katika hali asili aliyotuumba na ambayo tunaendelea kuiharibu kwa dhambi zetu. Tunakusanyika kama Kanisa kumuomba Mungu huruma na msamaha kwa ajili ya dunia nzima, tukiomba kusamehewa na kurejeshwa kwake.

Zaburi 51 ni sala iliyotolewa na Daudi baada ya kutenda dhambi. Daudi alimchukua mkewe Uria Mhiti baada ya kumuua vitani. Nabii Nathani aliwasilisha kesi mbele ya mfalme na kumwambia juu ya ghadhabu ya Mungu juu ya kichwa chake kwa kutenda uovu mbele za Mungu. Daudi hakuchelewa kufanya toba na kufunga kwa dhambi zake. Mungu alimwonyesha huruma na kupunguza adhabu yake. Daudi anatukumbusha kwamba hatuwezi kujificha kutokana na dhambi zetu kwa sababu ziko mbele yetu daima. Tunahitaji kukiri dhambi zetu mbele za Mungu na kumwomba atuumbe upya na kuturudishia furaha yetu iliyopotea. Tusihairishe kuungama; itatugharimu sana.

Mtume Paulo anatuita tupatanishwe na Mungu kwa njia ya Yesu Kristo aliyefanywa dhambi ili atuondolee dhambi zetu. Yesu alikuja; kuondoa udhaifu na dhambi zetu. Yesu alimgusa mwanaume mwenye ukoma na kumponya. Hii inamaanisha kwamba kwa hakika alitwaa ukoma kutoka kwake kama alivyochukua dhambi zetu. Kwa kufa msalabani, Yesu alilipa gharama kubwa kwa ajili ya dhambi zetu. Kipindi cha Kwaresma ni wakati mwafaka wa kutengeneza amani ndani ya nafsi zetu, amani na Mungu, na jirani zetu.

Katika Injili ya leo, Yesu anawafundisha wanafunzi wake juu ya njia bora za kufunga, kusali, au kutoa sadaka. Tunapotoa sadaka na kupiga kelele ili watu wote wajue, hatupati tuzo kutoka kwa Mungu kwa sababu wale wanaotusikia wameshatutukuza. Pia, kufanya nyuso zenye huzuni ili wengine wajue kuwa tunafunga haisaidii. Mungu si kiziwi, na hivyo tunapomwomba, hatuhitaji kupiga kelele kana kwamba kufanya watu wajue kuwa tunasali kwa bidii kutafanya sala yetu isikike. Kupiga kelele wakati wa sala imekuwa kawaida katika mikusanyiko mingi ya Kikristo. Mara nyingine unaweza kudhani kuna mashindano ni sauti ya nani itamfikia Mungu kwanza. Mungu anaona yale yaliyofichika na hatuhitaji kufanya sarakasi ili atuone.

Wapendwa, kuna mambo mengi yanayohitaji kukarabitiwa au kurejeshwa katika nafsi zetu, jamii zetu, na Dunia kwa jumla. Tujikite katika toba ya kweli ili Mungu aweze kuturejesha. Familia zilizovunjika, marafiki waliogombana, mahusiano ya kidiplomasia yaliyoharibika, nk. Tuutumie wakati huu kwa busara. Unapanga vipi kuishi kipindi hiki muhimu cha imani yetu?

Uwe na Kwaresma yenye baraka.

Pd. Lawrence Muthee, SVD

Leave a comment