Isaya 60:1-6; Zaburi (71)72; Waefeso 3:2-3.5-6; Mathayo 2:1-12
Mungu anajidhihirisha kwa watu wote

Wapendwa, Leo ni sikukuu ya Tokeo la Bwana. Ufunuo maana yake ni kujidhihirisha. Mungu aliamua kujidhihirisha kwetu kupitia Mwana wake Bwana wetu Yesu Kristo ili aturejeshe kwake, kurejesha taswira na mfano wa awali tulioupoteza kwa dhambi. Ufunuo wa kwanza wa Yesu ulikuwa kwa wachungaji maskini wa nyumba ya Israeli. Ufunuo wa pili ni kwa Maajusi kutoka Mashariki wanaowakilisha watu kutoka mataifa yote. Ufunuo wa tatu utakuwa huko Yordani na Yohane Mbaptizaji ambapo Yohane unamtambulisho Yesu kama mwanakondoo wa Mungu na Mungu mwenyewe anamtambulisha kama Mwanae mpendwa (Lk 3:21-22; Yn 1:29-31).
Katika somo la kwanza, Yerusalemu anaitwa kuinuka kwa sababu siku za mateso na uharibifu zitakwisha. Mfalme mpya atakuja na kurejesha utukufu wake uliopotea. Wote waliotawanyika kwa vita na utumwa watakusanyika, na kutakuwa na alfajiri mpya. Kweli ilikuwa habari njema kwa watu wa Yerusalemu na habari njema kwetu leo. Kuna watu wengi wanaoishi kama watumwa wa kisasa. Kuna wengi wamekuwa watumwa wa waajiri wao, serikali zao, wenzi wao wa ndoa, biashara zao, na hata familia zao. Na zaidi, wengi wamekuwa watumwa wa dini zao na viongozi wa dini ambao wanapaswa kuwaweka huru.
Mzaburi anamhimidi Mfalme wa Haki na Amani atakayekuja kutawala juu yetu. Kila mtu atafurahishwa naye na wafalme kutoka pande zote watamletea zawadi. Kila mtu atavutwa na njia yake ya kutawala, ambayo itakuwa tofauti na wafalme wengine duniani. Sote tunatamani mambo mazuri, maisha bora, bila mateso. Njaa yetu ya maisha bora yatapatikana kwa Mfalme huyu aliyezaliwa. Anarudisha uhuru wa kweli wa kuchagua katika ulimwengu ambapo mema na mabaya yanakaa pamoja.
Kuzaliwa kwa Yesu ni zawadi kubwa zaidi ambayo Mungu ameipa dunia. Kupitia Kristo, Mungu amejionyesha kwetu na tunaweza kuthubutu kumkaribia. Amekuja kuunganisha mataifa yote ili tusiwe na ‘sisi’ na ‘wao’ tena. Wote watakuwa kitu kimoja. Maajusi wanawakilisha watu wote duniani ambao wamekuja kumwabudu mfalme mpya. Yeye ndiye nyota itakayoangaza dunia nzima. Zawadi ya Dhahabu inawakilisha ufalme wake, Ubani unawakilisha utendaji wake, na Manemane inawakilisha kifo chake kwa wokovu wa wote.
Kanuni ya kwanza ya Ukristo ni umoja ndani ya Kristo. Katika Kanisa Katoliki, tunaye ‘Vicarius Christi’ au Mwakilishi wa Kristo, yaani, Papa. Papa ni ishara ya umoja wa jamii ya Kikatoliki. Yeye ni mwakilishi wa kibinadamu wa Kristo ambaye ndiye kusudi la Kanisa. Mtu anapowekwa wakfu kuhudumu kama padre katika Kanisa Katoliki, yeye pia anakuwa “in persona Christi” au umwilisho wake Kristo. Anawakilisha Kristo ambaye hufanya kazi ndani yake kubariki watu wake. Yesu aliwapa wanafunzi wake jukumu la kutenda kwa niaba yake ili kuendeleza mafumbo ya wokovu. Kristo, ambaye yupo kimwili pamoja nasi tena, yupo hai kupitia mitume wake waliowekwa wakfu.
Katika Injili, tunasikia kwamba Mfalme Herode aliwaomba Maajusi kutoka Mashariki waende wakachunguze habari zaidi kuhusu mtoto na kumletea taarifa. Kulingana na Herode, yeye pia alitaka kwenda kumsujudia mfalme. Hata hivyo, tunajua kwamba nia yake halisi ilikuwa kumuua mfalme mdogo kwa sababu alimwona kuwa tishio kwa cheo na nafasi yake.
Wakati wengine walipofurahia kuzaliwa kwa mfalme mpya, Herode aliona tishio kwa utawala wake. Aliwekeza muda na nguvu nyingi kujaribu kujua habari za mtoto ambaye hata nyota zilichomoza wakati wa kuzaliwa kwake. Herode anatuwakilisha sisi tunapozidiwa na wivu na chuki kwa watu wengine ambao ni tofauti na sisi au wenye tabia bora kuliko sisi.
Leo tunao wengi kama Herode wanaotafuta habari za wengine ili kuwaangamiza. Mara nyingine wanakuja kwetu wakiwa wamejificha kama watu wema na kwa kwa kutokujua tunawapa habari kuhusu wanafamilia, waajiri wetu, watoto wetu, na marafiki zetu. Baadaye wanatumia taarifa hizi kuwaangamiza. Mara nyingine wanatumia marafiki wetu wa karibu kupata habari zetu ili kutuangamiza. Watu wamefanya uhalifu mwingi kwa sababu ya wivu. Hata hivyo, Mungu anaendelea kutuongoza kupitia Kanisa lake ili tusianguke katika mtego wa Herode wa leo na kusaliti watu wema. Je, nimewasaliti wangapi kwa kusema kuwasema vibaya au kutoa taarifa nyeti kuhusu wao?
Wapendwa, lazima tuwe macho kila wakati kwa sababu si kila mtu anayetaka kujua habari za wengine kutoka kwetu ana nia njema. Baadhi ya watu wanatafuta habari za wengine ili kuwaangamiza kama Herode kwa sababu wanajihisi kutishiwa. Je, mimi ni mmoja wa watu hawa?
Heri ya Mwaka Mpya
Pd. Lawrence Muthee, SVD
