Masomo ya Jumapili kwa kifupi: Maaajili 2 A
Isaya 40:1-5.9-11; Zab 85; 2 Petro 3:8-14; Marko 1:1-8
Umuhimu wa amani

Wapendwa, leo tunaanza wiki ya pili ya Kipindi cha Maajilio na mada ya wiki nzima ni AMANI. Masomo yanaongea kuhusu kuandaa kwa njia kwa ajili ya mfalme wa amani anayekuja kwetu. Hapa kuna maswali ambayo yatatusaidia kutafakari wiki hii. Je, kuna amani ulimwenguni? Je, nchi yako ina amani? Je, kuna amani katika ujirani wako? Je, jamii yako inaishi kwa amani? Je, familia yako ina ina amani? Je, wewe mwenyewe una amani? Kabla hatujajibu maswali haya, tunahitaji kwanza kuelewa maana ya amani. Amani ni nini? Swali kuhusu amani ni pana sana na majibu ni mengi kama ilivyo idadi ya watu duniani. Maana ya amani imekuwa tofauti sana na watu hawaonekani kukubaliana kuhusu jinsi hali ya amani inavyopaswa kuwa. Hata hivyo, swala la amani, kwa maoni yangu, lazima liangazie ngazi ya mtu binafsi. Ikiwa mtu ni mwenye amani, kila kitu kinachomzunguka hakika kitakuwa na amani.
Kamusi ya Kiingereza inatoa maelezo mbalimbali ya neno amani kama vile kutokuwepo kwa vita, uhusiano wa mwema, uhuru kutokana na mizozo, usalama wa maeneo ya umma, kusitisha mapigano, nk. Zaidi ya hayo, maelezo mengi hutokana na hali fulani ya awali ya ukosefu wa amani. Huu tunaweza kuita “maelezo hasi” kuhusu amani. Hii inamaanisha kwamba maana ya amani inatokana na hali hasi inayopingana nayo. Labda ndiyo sababu amani imekuwa ngumu sana kupatikana duniani. Hakuna mtu anayeweza kufanikisha jambo asilolijua. Kuna watu ambao hawajawahi kujua amani maishani mwao kwa sababu walizaliwa katika familia, jamii, jirani na nchi zilizojaa migogoro. Inakuwa ngumu sana kwa mtu kuwa na amani ikiwa hajawahi kujua maana ya amani au jinsi inavyoonekana.
Katika somo la kwanza, Isaya anawafariji watu wa Israeli waliopitia mateso mengi. Nabii anawaambia watu wajiandae kwa ajili ya kumpokea Bwana wa amani. Ili Bwana wa amani apite, maandalizi mengi yanahitajika kufanyika, ikiwa ni pamoja na kujaza mabonde, kunyoosha milima na vilima, kurekebisha yale yaliyopinda na kusawazisha yale yasiyolingana. Hii inatuhusu sisi kama watu binafsi na pia kama jamii. Labda amani imekuwa ikitukwepa kwa sababu hatujajiandaa vizuri ili ikae ndani yetu na katika jamii zetu. Kujiandaa kwa ajili ya amani inamaanisha kutafuta haki. Mwanamuziki mmoja wa nyimbo za reggae anaimba, “Kila mtu analia kwa ajili ya amani lakini hakuna anayelia kwa ajili ya haki.” Haki ni ndugu mkubwa wa amani. Mtu hawezi kuwa na amani ikiwa anajihisi kudhulumiwa na kukosa haki.
Ikiwa ninataka kuwa na amani kama mtu binafsi, lazima nijaze mabonde ya chuki niliyochimba, nifute milima ya kulipa kisasi, nirekebishe njia zile zilizopinda na zilizopotoka na kumtenda jirani yangu kwa haki. Hili pia linatumika ndani ya jamii na kati ya mataifa. Migogoro inasababishwa na machafuko ndani ya mtu binafsi, ambayo yanafurika kwenye mazingira yanayomzunguka. Ni mbaya zaidi ikiwa mtu huyo ni kiongozi kwa sababu mgogoro uliopo ndani yake unawaadhiri wale anaowaongoza. Ndiyo maana wanasiasa na viongozi wa jamii wanapaswa waelewe na wawe na amani wenyewe. Lakini viongozi wanawezaje kuwa na amani ikiwa mara tu wanapochaguliwa, wananza kuchokoza wapinzani au washindani wao?
Mtakatifu Petro anawafariji wale waliosubiri amani kwa muda mrefu na labda wanafikiri kwamba Mungu hawajali. Labda wewe ni mmoja wa wao ambao wamepitia mateso mengi na migogoro isiyokwisha maishani mwako. Kulingana na Petro, Mungu hana mipaka ya wakati wala nafasi. Mungu hafanyi kazi kama binadamu. Hatendi kama tunavyotaka afanye. Nimejifunza hili katika utume wangu. Unapokuwa kiongozi wa watu na jamii kubwa, unapaswa kujifunza uvumilivu ili kuleta amani kwa watu wako. Mara nyingi, waumini huja ofisini kwangu au kunipigia simu kulalamika kuhusu viongozi wao au wanajumuiya wenzao. Mara nyingi, wanataka niwape suluhisho la haraka na hata kunieleza hatua ninazopaswa kuchukua. Baadhi yao wanataka niwafukuze, kuwaadhibu, na hata kuwatenga watuhumiwa kabla hata kuwasikiliza. Wanatarajia nifanye maamuzi kulingana na neno lao na hata kutishia kuwa mambo yatakuwa mabaya zaidi ikiwa sitachukua hatua. Wanachosahau ni kwamba wote ni sehemu ya kundi langu na utume wangu ni kuhakikisha kwamba hakuna hata mmoja wao anapotea. Hawajui kwamba uongozi wa Kikristo haukusudii kuvunja bali kurekebisha kilichovunjika. Wanasahau kwamba wale walio walipotoka ndio wanaohitaji zaidi msaada. Huwa nachukua fursa kama hii kuwafundisha niña hasa maana ya ufalme wa Mungu ulioletwa kwetu katika Kristu.
Mtakatifu Marko anaanza Injili yake kwa kutangaza kwamba Yesu ni Mwana wa kweli wa Mungu na mfalme wa amani. Yohane mbatizaji alikuja kuwaandaa watu kupokea mfalme huyu wa amani kwa kufanya amani na Mungu wao na jirani. Ikiwa sisi pia tunataka mfalme wa amani aje na kutawala mioyo mwetu na jamii zetu, tunahitaji kuandaa njia kwa ajili yake. Amani ni kama mto unaopita karibu. Ikiwa mtu anataka sehemu ya mto huo kunyunyizia shambani lake, basi anapaswa kuchimba mfereji ili kuelekeza ule mto shambani. Kama sivyo, mto unaendelea na njia yake bila kusumbuliwa.
Wapendwa, amani ni kitu cha thamani kubwa sana duniani na haipatikani kwa silaha na au kupiga kelele. Yesu alipofufuka kutoka kwa wafu na kujitokeza kwa wanafunzi wake, zawadi ya kwanza aliyowapa wanafunzi wake ilikuwa amani, “Amani iwe kwenu”. Mungu ni mwenye amani, na sisi kama viumbe vyake tunaalikwa kuishi kwa amani. Labda leo ninapaswa kujiuliza maswali machache zaidi. Nini kinacholeta fujo karibu nami? Je, mimi ndiye chanzo cha migogoro katika familia yangu au jamii yangu? Nini ambacho nahitajika kukifanya ili kuongeza amani katika mazingira yangu? Ni nini ninahitaji kujua au kufanya ili kupata amani ndani yangu? Je, ninaelewa maana ya amani?
Ikiwa unafurahia amani, nakusihi ufanye unakiri vizuri usije ukashau jinsi hali hii. Ikiwa migogoro ndio inayotawala ulimwengu wako, unahitaji kumkaribia Yesu na kumwomba akufundishe jinsi ya kuwa na amani. Nina hakika atakutaka ujinyenyekeze na kusamehe uchungu wote ulio moyoni mwako. Hata hivyo, Mungu ni baba yetu mwenye amani ambaye ametupa amani kwa njia ya Mwanawe. Tumkaribishe mfalme huyu wa amani katika maisha yetu na kumwomba atushirikishe amani yake.
Nikutakie wiki yenye amani.
Pd. Lawrence Muthee, SVD
