Masomo ya Jumapili kwa kifupi 32 A

Hekima 6:12-16; Zaburi 63; 1 Wathesalonike 4:13-18; Mathayo 25:1-13

“Hekima katika Matumaini”

“Siku moja nilipokuwa nikisafiri kwenda kwenye kituo kimoja hapa parokia, nilimuona kijana mmoja mbele yangu akitembea katika eneo ambalo hamna wakaaji. Kwa jinsi alivyokuwa akitembea, nilijua kwamba mfuko aliyokuwa akibeba ulikuwa mzito. Jua lilikuwa kali sana siku hiyo. Nilipokaribia, alinipungia mkono akiniomba msaada. Safarini, nilimuuliza kwa nini hakusubiri kwenye nyia panda ili apate gari lipitapo. Aliniambia kwamba hakutaka kukaa tu na kusubiri. Aliona ni bora kuendelea kutembea kwa sababu kama gari halingepita, asingekuwa amepoteza muda wake akiwa ameketi hapo. Niliiona wazo lake kuwa la busara sana kuzingatia kwamba magari machache sana hupita njia ile.

Soma la kwanza leo linazungumzia hekima na jinsi ya kuipata. Kitabu cha Hekima kinamwonyesha hekima kama mwanamke mrembo. Hekima katika muktadha huu ni “sanaa ya kuishi vizuri”. Wale walio na hekima wanafaidi mema ya Maisha hapa duniani. Wapumbavu wanakumbana na hali ngumu na maisha yao yamejaa changamoto.

Katika Kitabu cha Hosea 4:6, Mungu anasema kwamba “Watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa”. Ujinga au kutokuwa na maelekezo na malezi sahihi kunaweza kutugharimu rasilimali nyingi, na hata Maisha yenyewe. Kwa mfano, watu wengi hapa kijijini hutumia mchanganyiko wa dawa za jadi (mchanganyiko wa vitu mbalimbali) kama dawa ya kutibu magonjwa yao bila kujali yaliyomo, kipimo, au muda wake. Kumbe wanadhoofisha afya zao kwa madawa haya ambayo hayajapimwa ubora wake.  Wao huita gari la hospitali wakati tu mgonjwa yupo katika hali mbaya sana. Mchanganyiko huu unaweza kusababisha uharibifu mkubwa wa viungo, au upinzani wa dawa mwilini, au kifo.

Ili kusisitiza umuhimu wa kupata na kumiliki hekima, Yesu leo anatuletea mfano wa wanawali kumi, watano kati yao walikuwa wenye hekima na watano walikuwa wapumbavu. Wanawali wenye hekima walifikiria mapema na kutarajia uwezekano wa kuchelewa kwa bwana arusi, jambo ambalo lilikuwa la kawaida sana. Huenda walizingatia mambo mengi ambayo yangesababisha bwana arusi kuchelewa. Hivyo, walichukua tahadhari kwa kubeba mafuta zaidi kwa taa zao. Wanawali wapumbavu hawakujali, walikuwa na furaha tu kwa kuwa walichaguliwa kuwa pamoja na bwana arusi. Labda hawakutaka kujishughulisha na vitu vingine vya ziada.

Kama Wakristo wakubatizwa, tunatumaini katika ufufuo kwa sababu ya ahadi ambayo Mungu alitupa katika Kristo. Tunasadiki kwamba hata kama tutakufa, tutafufuka na kuishi na Mungu milele mbinguni. Hata hivyo, tumaini hili halipaswi kuwa la kusubiri tu. Maisha yetu ya Kikristo ni safari yenye milima na mabonde. Tunahitaji kusubiri kwa hekima sana siku hiyo kwa sababu yule mwovu pia yupo kazini akijaribu kutupoteza njia.”

Maranyingi sisi ni kama wanawali wale wapumbavu. Baada ya ubatizo, tunaingia kwenye upweke wa imani yetu na kusubiri Siku ya Hukumu itushangaze. Tunageukia Mungu tu wakati wa shida. Hekima ya kidunia hutufanya tufikiri kwamba kuishi kwa maadili ya Kikristo ni kupoteza muda. Tumemfanya Mungu kuwa viatu vya matope tunayohitaji wakati wa msimu wa mvua tu na kuiweka mbali wakati wa kiangazi. Kitabu cha Hekima kinaonyesha hekima kwa ujumla kama “ujuzi wa jinsi dunia inavyofanya kazi na jinsi ya kufaidi vizuri.” Ni wale tu walio karibu na Mungu watakaomiliki hekima hii. Tunaweza kugundua uwezo wetu na kuutumia vizuri ikiwa tuko karibu na Mungu. Hata hivyo, kuna wengine wanaoangamia kwa kufikiri kwamba wana hekima kuliko Mungu na kwamba amri zake ni kero maishani mwao. Ni wazi kwamba mafanikio hajatoka kwa Mungu yana muda mfupi sana. Ikiwa una shaka na hilo, chukua muda wako kuchunguza.

Tumaini ni kitu chenye thamani sana na yule asiye na tumaini anajikuta na chaguzi chache sana maishani. Hata hivyo, tumaini la uongo ni mbaya zaidi kuliko kutokuwa na tumaini kabisa. Tumaini la uongo ni kama mtego unaoangukia mawindo yake kwa urahisi. Wafanyabiashara wa matumaini ya uongo ni wengi na kila mahali katika vijiji, miji, majiji yetu. Biashara zao zimeundwa vizuri, na vidhaa zao zinavutia wapumbavu kwa urahisi. Wanajua vizuri wanachokifanya. Ni jambo la kusikitisha kwamba wengi walio batizwa hawafaidi matunda ya imani yao kwa sababu hawatafuti uelewa Zaidi wa mafundisho waliyoipokea walipokuwa watoto.

Katika ubatizo, tunafanyika watoto wa Mungu na hivyo tunaweza kumtafuta kwa mioyo yetu. Yesu ndiye “njia ya kweli” kuelekea katika ufalme wa Mungu. Viongozi wetu kiroho ni wasaidizi tu na sio nywila (password) za baraka za Mungu kama wengine wanavyojifanya. Sisi si wanaharamu wanaohitaji manabii ili kumfikia Baba yetu. Yesu amekufa kwa ajili yetu na kutuchukulia urithi kwa Mungu Baba. Wala hakuna aitwae haki hiyo kutoka kwetu kwa kujifanya kuuza baraka za Mungu kwa bei.

Wapendwa katika Kristu, tumaini la kweli daima lazima liwe hai na tayari. Yesu mwenyewe alituasa kukesha na kuwa tayari kama wanawali watano wenye hekima. Tusisubiri tu mtu atusaidie tunapohitaji, bali tuanza kutafuta suluhu kuhusu hali hiyo. Kuamini Mungu ni jambo jema lakini kuishi kulingana na mahitaji ya imani katika Mungu ni hekima.

Jumapili njema.

Fr. Lawrence Muthee, SVD

Leave a comment