Kwa nini ni lazima Kupenda?

Masomo ya Jumapili kwa kifupi 30 A

Kutoka 22:20-26; Zaburi 17(18); 1 Wathesalonike 1:5-10; Mathayo 22:34-40

Kwa nini ni lazima Kupenda?

Wapendwa, leo ni Jumapili ya 30 ya kipindi wa Kawaida cha mwaka. bado wiki nne zaidi kabla ya kumaliza mwaka huu wa liturujia A. Masomo ya leo yanatukumbusha kuhusu amri za Mungu na kwa nini ni busara kuzitii kikamilifu kadiri tuwezavyo. Kulingana na imani yetu ya Kikristo, Mungu aliumba ulimwengu na binadamu si kwa sababu ilimlazimu bali kwa sababu ya UPENDO. Ndio maana alituumba kwa sura na mfano wake (Mwanzo 1:26-27) na pia akapuliza uhai wake ndani yetu (Mwanzo 2:7), ili tuweze kushiriki katika uhai wake. Wakati mwanamume na mwanamke walipoamini uongo wa shetani na kufanya yale Mungu aliyewakataza kufanya, Mungu hakuwaacha kwa hasira bali alianza mchakato wa kuwarejesha kwake. Hii ni kwa sababu UPENDO ulikuwa ndio msukumo wake. Wakati upendo unapokuwa katika husukani, hakuna jambo baya linaloshindikana kusamehe.

Kwa kuwa dhambi iliharibu uwezo wa mwanadamu wa kuchagua mema badala ya mabaya, Mungu alitupa amri ambazo kama tukizishika kikamilify zitatusaidia kuwa waadilifu. Amri Kumi zinashughulikia vipengele muhimu vya hadhi ya kibinadamu katika uhusiano na Mungu na wanadamu wenzake. Amri tatu za kwanza zinaeleza jinsi tunavyopaswa kuhusiana na Muumbaji wetu, na amri saba zinazingatia jinsi tunavyopaswa kutendeana sisi kwa sisi kama binadamu.

Wakristo wanafahamu tabia ya Mungu kupitia ufunuo wake uliomo katika Maandiko Matakatifu na kuandikwa moyoni mwa kila mmoja kama maarifa ya asili ya mema na mabaya. Agano la Kale ni historia ya watu ambao Mungu aliwachagua kati ya mataifa mengine, ili kutekeleza mpango wake wa wokovu wa binadamu wote dhidi ya kujiangamiza wenyewe.

Kwa sababu ya dhambi, tamaduni zetu, kama ile ya Wayahudi, ziliathiriwa na uovu na ufisadi wa kila aina. Kama tunavyosoma katika Agano la Kale la Wayahudi, desturi zetu za kitamaduni hazina usawa na haki. Katika jamii nyingi, sheria ya mwenye nguvu mpishe inatumika ambapo matajiri, wenye nguvu, na mafisadi wanafanikiwa wakati maskini na wanyonge wanateseka. Katika tamaduni hizi, zinaendesha ukatili wa kijinsia na kuwadhalilisha hasa wanawake na watoto. Mtazamo wa ubaguzi na ukoloni, ambapo baadhi ya watu wanafikiri kuwa kiasili wao ni bora au wana haki zaidi ya wengine, unaendelea kuzua chuki sehemu mbalimbali za dunia. Ukoloni mamboleo na sera zisizo za haki za kibiashara zinaendelea kuwanyima faida nchi masikini, hasa katika ukanda wa kusini wa dunia. Yote haya yanaweza kuonekana kuwa mazuri kwa mdhalimu lakini sio ya kutamaniwa na waathiriwa. Yote haya yanategemea ni upande upi wa historia mtu yupo. Mara nyingi maskini na wajane wanumia Zaidi.

Yote haya yanatokea kwa sababu tunafuata njia zetu wenyewe na sio njia za Mungu. Wakati mmoja Yesu alimkemea Petro na hata kumwita Shetani, kwa sababu alikuwa anafikiri kama binadamu na sio kama Mungu. Ufisadi wote na ukatili tunaoona duniani leo ni matunda tu ya kutumia hekima ya kibinadamu na kutozingatia hekima na amri za Mungu. Matokeo yake ni vita, mateso, ukatili, mabadiliko ya tabia ya nchi, na kifo. Katika somo la kwanza leo, Mungu anatukumbusha kwamba ikiwa tutafanya maskini kulia, atawasikiliza na kuja kuwaokoa. Hii inatuweka moja kwa moja katika vita na Mungu. Wengi wanajiuliza kwa nini, pamoja na utajiri, elimu, nyadhifa, na nguvu walizo nazo, amani na furaha zinaendelea kuwakwepa. Vizuri, jibu linaweza kuwa kwamba wanaweza kuwa wanapigana na Mungu kwa jinsi wanavyoendesha shughuli zao za kila siku.

Yesu alitupa mifano mingi ya upendo wa Mungu kwa watu wake. Akiwa Mungu na Mwanadamu, alikuwa na uwezo wa kutumia hadithi za kidunia ambazo sote tunaelewa, kueleza upendo wa Mungu kwetu. Kwa mfano, mifano ya kondoo aliyepotea, sarafu iliyopotea, na mwana aliyepotea katika Injili ya Luka 15 zinaonyesha jinsi Mungu anavyofanya kila juhudi kuturejesha kutoka katika mateso yetu. Leo anatukumbusha kwamba amri kuu zaidi ni UPENDO. Upendo kwa Mungu na upendo kwa wale walio karibu nasi.

Sayansi inaonyesha kwamba watoto wanazaliwa bila hatia na huwa na tabia ya upendo ya asili. Hii inatufundisha kwamba chuki, ubinafsi, wivu, na ushindani hasi, pamoja na tabia nyingine zinazopingana na sheria ya upendo, ni mambo ambayo tunafundishwa au kujifunza kadri tunavyoendelea kukua. Ili kuendelea kuwa katika upendo wa Mungu, tunahitaji kuwa daima na ufahamu wa hatari ya uovu unaotukondolea macho kila dakika. Mstari uliopo kati ya kuwa mwenye haki na kuwa wakala wa shetani ni mwembamba sana. Hii ni kwa sababu uovu daima huja kinafiki na wakuvutia. Ikiwa hatuna hekima ya kiroho iliyojumuishwa katika amri za Mungu, basi tunaweza kwa urahisi kushawishika na uovu.

Haki haionyeshwi na jinsi tunavyoongea vizuri kuihusu, bali kwa matendo yetu hata yale madogo zaidi ya upendo kwa wengine, bila kujali tunayaelekeza kwa nani. Tunapokubali masilahi binafsi kuteka dhamiri zetu, basi chochote tunachofanya baadaye ni kilema na hakiwezi kufafanuliwa kuwa ni upendo. Kuhusu UPENDO wa Mungu na Jirani, sheria nzima na unabii inafupishwa (Mathayo 22:40).

Tunaweza kwenda kuabudu kila siku, kutoa zaka kubwa, kujenga sehemu za ibada, na hata kutenga maisha yetu yote kwa huduma ya kiroho, lakini ikiwa hatuna UPENDO, vyote hivyo havina thamani. Mtume Paulo analiweka wazi zaidi katika wimbo wake wa Upendo katika 1 Wakorintho 13:1-13.

Mwaliko wangu kwetu sote leo, wapendwa, ni kujitathmini jinsi tunavyoishi na kuona ikiwa kinachotuhamasisha kufanya tunachofanya ni upendo au ni ubinafsi. Hii itatueleza kwa nini maisha yetu yako kama yalivyo. Ikiwa tunafikiri kwamba amri za Mungu ni mzigo mzito kubeba, basi tunawezaje kutarajia kwamba Mungu atuondolee mizigo ya maisha yetu? Kuzishika amri za Mungu ni kumruhusu Mungu kutusaidia.

Iwe na Jumapili yenye upendo.

Pd. Lawrence Muthee, SVD

Leave a comment