Majukumu ya Kikristo: Jumapili ya 27 A

Masomo ya Jumapili kwa kifupi 27 A

Isaya 5:1-7; Zaburi 79(80); Wafilipi 4:6-9; Mathayo 21:33-43

Majukumu ya Kikristo: Kile kinachotarajiwa kutoka kwa Mkristo.

Wapendwa, Ukristo ni njia ya maisha, mwongozo wa tabia, njia ya fadhila. Kwa hivyo, Wakristo wanatarajiwa kuendesha maisha yao kwa njia fulani, wakijitofautisha na ulimwengu. Njia hii ya maisha siyo ideolojia bali ni kumuiga Yesu wa Nazareti, Kristo wa Mungu. Kila kitu ambacho Mungu alitaka wanadamu wajue na waishi, amekifunua kupitia Yesu Kristo (Waebrania 1). Kila Mkristo anahitaji kufanya ili kuwa kwenye njia hiyo ni kumuiga Kristo.

Sasa, ili kumuiga mtu, tunahitaji kumfaham vizuri huyo mtu. Wakristo wanapaswa kukua katika kumfahamu Kristo kila siku kwa kusikiliza mafundisho yake. Maandiko Matakatifu ni mlango wa kuelewa Kristo na ufunuo wake kuhusu Ufalme wa Mungu.

Ukristo si mtindo wa maisha wa kubweteka tu bali ni mtindo wa maisha wa vitendo na wenye majukumu mengi kwa nafsi na ulimwengu unaomzunguka Mkristo. Mkristo anatarajiwa kuzaa matunda mema (Yohane 15:16). Katika somo la kwanza, Isaya analinganisha Israeli na shamba la mizabibu na Mungu kama mmiliki wa shamba lenyewe. Mkulima mzuri anajiandaa vizuri kabla ya kupanda mbegu, na anatarajia akirudi baada ya muda Fulani shamba hilo liwe na matunda. Anaweka uuzioa kuilinda dhidi ya Wanyama. Anaondoa vikwazo vyote na kulisafisha magugu yote. Mungu aliwaandaa watu wa Israeli ili wazae matunda katika mpango wake wa wokovu kwa binadamu wote. Hata hivyo, watu wa Israeli walizaa matunda pori ya uovu badala ya haki.

Katika ubatizo, Mungu anaandaa mzabibu wa maisha yetu kwa kututakasa na dhambi zote tulizorithi kutoka kwa wazazi wetu (dhambi ya asili). Anatuokoa kwa damu ya Mwanae iliyomwagika msalabani. Anatuzunguka kwa neema yake na kutulinda na yule mwovu. Kwa hivyo, Mungu anatarajia kutoka kwetu matunda mema ya upendo, haki, na amani. Badala yake, watu waliobatizwa ndio wanaochukia zaidi, kutenda dhuluma zaidi, na kuvuruga amani kuliko wengine wote. Kuanzia ngazi ya familia, tunashuhudia jinsi watu waliobatizwa wanavyotenda ukatili mbaya. Watu wanaobeba majina ya Kikristo ndio watumishi wa umma wasio na nidhamu, wafisadi na waporaji wakubwa wa rasilimali za umma ambazo zinapaswa kuboresha Maisha ya raia.

Wakati tunafanya haya yote, wanadamu tunasahau kwamba Mungu anatutazama. Tunapokamatwa na hatua inachukuliwa dhidi yetu, tunalalamika na kuleta siasa mbaya. Tunalia mambo yanapotugeukia na tunapoteza kila kitu. Hatufahamu kwamba Mungu ameondoa uzio wake aliotuzunguka nao tayari. Hakuna mtu anayeweza kuelewa hili zaidi ya wakulima wanaoishi na wafugaji au wanyama wa porini. Ili kuvuna, wakulima wanatumia gharama kubwa kulinda mashamba yao kuanzia siku ya kupanda mbegu hadi kuvuna. Nimeona jinsi wanyama wanavyoweza kusafisha shamba lote kwa dakika chache. Hatungependa Mungu aondoe uzio wake na ulinzi kutoka kwetu. Ni bora kukabiliana na changamoto zinazotuzunguka katika neema ya Mungu kuliko kuwa matajiri bila uwepo wake.

Katika Injili ya leo, Yesu anasimulia mfano unaolenga kuwakemea wazee wa Israeli ambao walikuwa na jukumu la kuwaongoza watu kwa Mungu. Badala yake, walijishughulisha na biashara zao binafsi na wakati manabii walipowaonya, waliwaua. Mwishowe, Mungu alimtuma Mwanawe lakini wakamwua kwa kumtundika msalabani. Walichokuwa hawajui ni kwamba wakati ulikuwa umefika ambapo upinzani wao haukuvumilika tena. Ukristo ulizaliwa katika mazingira haya. Pamoja na kuja kwake Kristo, jukumu la wokovu liliondolewa kutoka kwa viongozi hadi kwa mtu binafsi. Sheria ya haki ilipaswa kuandikwa moyoni mwa kila mwanaume na mwanamke ili kila mmoja aweze kutoa mahesabu ya matendo yake mwenyewe. Hata hivyo, bado tuna watu ambao wamepewa jukumu kubwa la kuwaleta watu karibu na Yesu na kuwafundisha jinsi ya kuwa kama yeye.

Viongozi wa Kanisa ni wakulima katika shamba la Bwana. Wanatarajiwa kuwatunza vizuri watu wa Mungu na kuzaa matunda. Wamisionari, kwa mfano, ni watu waliotumwa na Kanisa kuwaletea watu ambao au hawajafikiwa kabisa na neno la Mungu au hawajamwelewa vizuri Kristo. Wao ni nuru kwao. Wanapaswa kuwasaidia kuona nuru na kubadilisha mtindo wao wa maisha. Wanapaswa kuwa karibu nao na kwa maneno ya Papa Francis “kunukia kama wao”. Hata hivyo, hawatarajiwi kuwa kama wao lakini kuwasaidia kuwa kama Kristo.

Mwanzoni mwa uinjilishaji barani Afrika, wamisionari walifanya bidi kuwavuta watu kumwamini Mungu. Walichangia kwa kiasi kikubwa kuanzisha Kanisa la mahalia. Baadhi walitoa pumzi yao ya mwisho kwa ajili ya utume na matunda yao ndiyo yamekuwa Kanisa mahalia lililo hai. Hata hivyo, baadhi ya wamisionari walifanya kosa kubwa ambalo matokeo yake yanaliandama kanisa hata leo. Walidhani kwamba kuzama katika tamaduni za watu waliowahubiria, hata kuvaa kama wao, ilikuwa njia bora zaidi ya kuhubiri. Walishindwa kuwafundisha ukweli na maadili ya Kikristo ya msingi na badala yake kusisitiza ubatizo wa watu wengi katika Kanisa. Walitumia mali nyingi kuwavutia watu Kwenda kanisani kwa kuwapatia nguo, chakula, na vitu vingine. Walichukua jukumu la kuelimisha watoto kutoka kwa wazazi. Sasa siku hizo za kutoa misaada zimepita, watu wanahisi kwamba wametelekezwa na Kanisa linawasaliti. Ilikuwa kama kuwakuta watu wakioga katika maji machafu, na kujitosha mwenyewe Pamoja nao. Miaka mingi baadaye, watu wa wengi bado hawajakubali kabisa Injili. Wamisionari wanapaswa kuwaonyesha watu njia sahihi ya kumuiga Kristo. Kuwasaidia watu kuwa kama Yesu na sio kumfanya Yesu afanane na watu na kumfanya afuate mila zao za jadi.

Ikiwa watu watatembea katika njia ambayo hawajaielewa vizuri au hawajaridhika nayo, mara nyingi wanarudi kwenye njia zao za zamani. Mikutano ya umati inayotafuta uongofu wa haraka, ubatizo wa umati na ibada zenye msisimko wa kihisia haziongezi imani bali zinaridhisha mtu kisikolojia kwa muda mfupi. Haipiti muda kabla ya wale ambao walionekana kuwa katika kilele cha furaha ya kiroho kurudi katika tamaduni na tabia zao za awali.

Kuwa Mkristo ni safari yenye changamoto na sio mahali pa kujificha au kuepuka majukumu. Shetani haendi likizo, tukilegea kidogo anapata nafasi ya kutupepeta. Inahitaji majitoleo, ibada, na bidii kubwa sana kuendeleza maisha ya Kikristo. Mkristo anapaswa kuwa nuru na chumvi ya ulimwengu. Mtumishi wa umma Mkristo anapaswa kutimiza majukumu yake kwa uaminifu kwa watu anaowahudumia na vivyo hivyo kwa watoa huduma wengine, wa binafsi au wa umma. Manabii wengi wamejitokeza wakihubiri mafanikio ya haraka na miujiza ya kuvutia watu wasio na uelewa. Wanahubiri mafanikio bila kufanya kazi na utajiri bila kutoa jasho. Tunaweza kuita hii “udanganyifu” kwa jina la Yesu. Watu wanapaswa kuhimizwa kukaa mbali na manabii kama hawa. Mungu mwenyewe alifanya kazi na aliwaamuru mwanamume na mwanamke kufanya kazi (Mwanzo 1:1-28).

Wapendwa, leo tuna chaguzi la kufanya. Lazima tufikirie ikiwa tutamuiga Yesu wa Nazareti aliyekuwa mfanyikazi hodari, mwenye huruma kwa maskini lakini mwenye msimamo thabiti juu ya maadili ya ufalme wa Mungu, au ikiwa tutamfuata Yesu wa mitaani na katika makongamano kuanzia Jumapili hadi Jumapili. Yesu ambaye anapaswa atufanyie kila kitu bila sisi kufanya chochote.

Nikutakie Jumapili yenye baraka tele.

Pd. Lawrence Muthee, SVD

Leave a comment