Masomo ya Jumapili kwa Ufupi: 26 A
Ezekieli 18:25-28; Zaburi 25; Wafilipi 2:1-11; Mathayo 21:28-32
Unyenyekevu wa kweli na Uongofu.

Wapendwa, leo ni Jumapili ya 26 ya Wakati wa Kawaida. Kuna msemo unasema, “Usihukumu kitabu kwa jalada lake.” Mara ngapi tunawatizama watu na kuwahukumu, kisha baadaye, tunapowajua vizuri, tuelewa kwamba hatukuwa sahihi kuwahusu? Yesu pia aliwaonya wanafunzi wake, “Si kila mtu asemaye Bwana, Bwana atatakayeingia katika ufalme wa mbinguni, bali ni yule afanyaye mapenzi ya Baba yangu” (Mt. 7:21-23).
Masomo ya leo yanahusiana na kauli ya unyenyekevu na kuongoka. Katika somo la kwanza, Ezekieli anatuambia kwamba ikiwa mtu mwovu atanyenyekea, atambue njia zake mbaya na kuongoka, Bwana atamsamehe dhambi zake. Hata hivyo, ikiwa mtu mwema anageuka kuwa mwovu, historia yake nzuri itafutika kwa matendo yake mabaya. Nimesikia watu wakisema kwamba wakati mwingine Mungu si mwenye haki wanapoona watu wanaodhaniwa kuwa waovu kiwakifanikiwa na wale wanaodhaniwa kuwa wema wakiteseka. Kwa kutumia uamuzi na viwango vyetu binafsi tunawahukumu watu kuwa wema au wabaya. Walakini, hukumu ya Mungu haitegemei sura au mwonekano bali kilichopo ndani ya mtu: nia, motisha, mapambano, na kadhalika. Sisi huangalia nje lakini Mungu huangalia ndani.
Mara nyingi tunajiona kuwa wema au hata wakamilifu kwa kutumia vigezo na mtazamo wetu wenyewe. Walakini, tukizingatia vigezo vya nje tunaweza kuwa wakosefu sana. Kipimo bora cha wema daima ni kipimo cha Yesu. Ikiwa matendo yetu yote, maneno na mawazo kuhusu wengine yangetawaliwa na mfano wa Kristo, basi tunaweza kusema kwamba tunajitahidi kuwa wema.
Mtakatifu Paulo anatuhimiza kumwiga Kristo, ambaye, ingawa alikuwa Mungu, hakuona kuwa ni sababu ya majivuno. Alijinyima na kuwa mnyenyekevu. Unyenyekevu wa Yesu ulikuwa na bado ni jambo unaovutia mioyo mingi kuongoka. Katika nyakati zetu, kuhubiri Injili imegeuka kuwa njia ya kupata umaarufu na utajiri binafsi wa mhubiri. Ukiangalia hatua wanazofikia katika maandalizi na vifaa vilivyotumiwa katika ibada na makongamano ya imani leo havionyeshi unyenyekevu wowote bali nguvu na tamaa ya utajiri. Ibada ya Kikristo imegeuka kuwa biashara ya kuuza na kununua miujiza. Unyenyekevu wa Kristo uko wapi katika haya yote?
Ndugu zangu, mara nyingine au mara nyingi tunawaahidi watu vitu ambavyo hatujapanga hata kutoa. Tunaahidi tu kuonekana wazuri na kupendwa na watu. Katika Parokia yetu Simanjiro, tuliamua kutokubali ahadi yoyote katika harambee kwa sababu tulitambua kwamba watu wengi wanatoa ahadi bila nia ya kuzitekeleza hata kidogo. Wanaahidi michango mikubwa ili kuonekana wazuri na kutumia jukwaa hilo kukuza malengo yao ya kisiasa na ya binafsi. Baada ya tukio, hawapatikani tena. Watu wanarudi nyumbani na fikra kwamba fecha nyingi zilizopatikana akilini mwao. Baada ya kufahamu msimamo huu, wanasiasa wengi hawahudhurii matukio yetu tena. Hii pia imesaidia watu wetu kujifunza umuhimu wa kujitegemea zaidi na kutotarajia watu wenye ushawishi mkubwa kuwapa ahadi za uongo.
Katika somo la Injili leo, Yesu anatoa mfano wa wana wawili ambao baba yao aliwaagiza kwenda kufanya kazi katika shamba lake na mizabibu. Wa kwanza alikataa waziwazi lakini, baada ya kujitafakari aligundua kwamba alikuwa amekosea kwa kutomtii baba yake na hivyo akaenda kufanya kile kilichohitajika kufanya. Mwana wa pili alikubali mara moja na kuahidi kufanya kazi, lakini hakufanya. Baba lazima alimpenda na labda alikuwa amepanga kumletea zawadi akirudi. Mara nyingine kufanana na mwana wa pili ili kuonekana wazuri mbele za watu.
Yesu hamtukuza mwana wa kwanza kwa kutokubali kufanya mapenzi ya baba yake, bali kwa kubadili mawazo yake na kufanya kile alichpagizwa. Toba pekee haikutoshi. Tunapaswa kwenda hatua Zaidi na kutekeleza kile kinachotarajiwa kutoka kwetu. Kuonekana kuwa wema na kufanya tofauti ni jambo ambalo Yesu alimea sana kwa mafarisayo.
Watu ambao tunaweza kuwachukulia kuwa waovu kwa sababu tunawahukumu kutoka nje, wanaweza kuwa bora zaidi kuliko sisi kwa ndani. Unafiki ni kitu ambacho Yesu alikemea kwa nguvu. Mungu anatazama mioyo yetu na siyo tunavyotaka watu waamini.
Wapendwa wangu, haijalizi ni kiasi gani cha vipodozi tunavyojipaka ili watu waamini kwamba sisi ni wazuri. Jambo muhimu ni jinsi tulivyo kwa kweli. Tunapokuwa pekee yetu katika vyumba vyetu, na tujitazame kwa kioo na kujiuliza ikiwa sisi ni wema au tunatumia nguvu na rasilimali nyingi kujifanya tuonekane wema. Tunaweza kuwa tunapoteza muda mwingi wa raslimali kujipendekeza lakini mwishoni vipondozi ufutika na ukweli unafunuliwa. Tumwombe Mungu atusaidie kukumbatia kweli na kuongoka kwa kweli.
Uwe na Jumapili yenye baraka.
Pd. Lawrence Muthee, SVD
