Masomo ya Jumapili kwa Kifupi
Isaya 55:6-9; Zaburi 145; Wafilipi 1:20-24.27; Mathayo 20:1-6
Ukarimu dhidi ya Wivu

Wapendwa, leo ni Jumapili ya 25 ya Kipindi cha Kawaida. Somo la kwanza leo linatuhimiza kumtafuta Bwana wakati angali anapatikana. Swali tunaloweza kujiuliza ni ikiwa itafika wakati ambapo Bwana hatakuwa hatapatikana. “Tafuteni Bwana, angali anapatikana.” Binadamu ni viumbe wadini. “Mwanadamu ni kiumbe mdini sana,” alisema marehemu Profesa John Mbiti. Mtakatifu Augustine pia anatukumbusha kwamba Mungu alituumba kwa ajili yake mwenyewe na mioyo yetu haitapumzika hadi ipumzike Kwake.
Ni uthibitisho wa kiasili kwamba kila kilicho na uhai kitakoma kuishi siku moja. Kama Wakristo, na kwa kweli, dini nyingine nyingi zinaamini siyo tu katika maisha baada ya kifo bali pia kwamba kutakuwa na siku ya hukumu ambapo kila mmoja wetu atalazimika kutoa hesabu ya maisha yake duniani. Yesu anatoa maelezo haya kwa mfano wa siku ya hukumu katika Mathayo 25:31-46.
Katekisimu ya Kanisa Katoliki inafundisha kuhusu Makanisa matatu. La kwanza ni Kanisa la maujaji ambalo ni Kanisa la waamini wanaoishi duniani wakisafiri kuelekea mbinguni. La pili ni Kanisa la toharani, Kanisa la wale waliokufa katika hali ya dhambi na wanatakaswa katika Limbo, na la tatu ni Kanisa la watakatifu, Kanisa la washindi ambao tayari wako mbinguni baada ya kushinda ulimwengu kwa imani na damu ya mwana-kondoo na wanashiriki utukufu wa Mungu milele.
Katika somo la Injili leo, tunasikia hadithi ya wafanyakazi wenye wivu na husuda ambao walikuwa na hasira na mwenye shamba mwenye ukarimu. Hii ni kwa sababu aliamua kulipa wafanyakazi wote waliotumika katika shamba lake mshahara waliokubaliana nao licha ya walifika nyakati tofauti kazini. Kulingana na mmoja wa wale wa kwanza kufika, mmiliki wa shamba hakutenda haki kwao. angepaswa ama kuongeza mshahara wao au kupunguza wa wale waliofika mwisho kwa sababu ingekuwa sio haki kuwasawazisha wote. Hukumu yao ilikuwa kwamba wale wa mwisho hawakustahili mshahara wa siku kamili. Hata hivyo, kutokana na masimulizi katika mfano huu, tunajua kwamba wafanyakazi wale waliofika mwisho walikuwa wamekaa siku nzima bila yeyote kuwapa kazi. Mwenye shamba aliwapa riziki wakati matumaini yote yalikuwa yamepotea. Sina hakika kwamba wafanyakazi hawa wa mwisho walitarajia kupokea mshahara wa siku kamili kama alivyowaahidi mwenye shamba. Lazima walishtuka sana kutokana na ukarimu wake. kimsingi, mwenye shamba alifanya kile kilichokuwa haki kulingana na makubaliano lakini machoni mwa wafanyakazi wa kwanza, na kwa kweli, machoni petu pia, inaonekana kwamba mwenye shamba huyu hakufanya haki kwa wale waliofika kwanza. Hii ni tabia inayojitokeza kwa watu wengi, ikiwa Wakristo.
Hapa hoja sio kuhusu kufika kwanza au mwisho bali makubaliano ambayo mwenye shamba alifanya na kila mfanyakazi. Mungu ameahidi wokovu kwa wote wanaorudi mbali na maovu na kufanya mapenzi yake bila kujali waliamua lini kufanya hivyo. Nina uzoefu kama huo na wafanyakazi wenye wivu katika utume wangu mwenyewe.
Jamii ya Wamaasai (ambapo nafanya kazi kama mmisionari) wanayo mojawapo ya miundo ya utamaduni yenye mfumo hadhi na heshima mkubwa zaidi niliowahi kujua. Heshima, hadhi, na nafasi ya mtu yanalingana na jinsia yake, umri, na utajiri wake. Wanaume wana makundi ya umri takriban 7 yaliyopangwa kwa utaratibu. Wanawake wana takriban 4. Utaratibu wa heshima unaanza na wanaume wazee, wale waliooa na wenye mali, waliioa, wanawake wazee, wanawake walioolewa, vijana mashujaa, na kisha watoto. Hata hivyo, mara nyingine ng’ombe wanakuja kabla ya wanawake na watoto. Daraja la chini halina uwezo wa kuelekeza, kuagiza, au kuamuru wale waliopo juu yao. Hii inasababisha changamoto nyingi linapokuja suala la uongozi wa Kanisa. Wanaume wanahisi kwamba ni haki yao kuwa viongozi wa jumuiya zao za imani, iwe walibatizwa wiki moja iliyopita au bila kujali ikiwa wanishi imani yao au la. Ikiwa wanawake na vijana wanakuwa viongozi, wanapinga kwa njia nyingi, ikiwa ni pamoja na kusitisha kwenda Kanisani, kukataa kuwaruhusu wake na watoto wao kwenda Kanisani, na kwa sababu wao ndio wamiliki wa rasilimali zote, wanakataa kutoa michango yoyote.
Tabia hii si tu katika utamaduni wa Wamaasai, bali pia inadhihirika sana katika makundi mbalimbali ya kikabila, rangi, na matabaka ya kiuchumi. Kuna wale wanaohisi kwamba kwa sababu wanatoka katika jamii, rangi, tabaka la kiuchumi, au nchi fulani, wana haki au ni wenye nafasi bora zaidi kuliko wengine. Tabia hii si nadra hata katika mazingira ya kidini. Kwa watu kama hao, fedheha yao ni kwamba machoni pa Mungu, sisi sote ni sawa. Hakuna anayeweza kudai mastahili mbele za Mungu, bali tunategemea huruma na neema yake. Kifo na fumbo la maisha baada ya kifo ni jambo linalotusawazisha wote licha ya tofauti zetu hapa duniani.
Wapendwa, tunapotafakari masomo ya leo, nawakaribisha kila mmoja wetu atafakari na kuona kama wakati wowote tunajiona wenye kustahili zaidi kuliko wengine. Je! Nafurahi au nachukia na kuona wivu wenzangu wanapofanikiwa? Hata hivyo, kwa kuwa wengi wetu wanapenda kujiona kama waathiriwa, ni vizuri pia kufahamu kwamba ikiwa tunapinga ubaguzi na kudhalilishwa tunapitia kutoka kwa wengine ni vizuri sis tuwatendee tofauti. Tukijibu sawasawa na walivyotutenda hatutakuwa tofauti nao kwa njia yoyote, bali Zaidi ya yote tutakuwa wabaya kuliko wao. Wema wetu unapaswa kupita udhaifu wa wengine. Jinsi tunavyowajibu wengine matendo yao kwetu ndicho ni kipimo halisi cha wema wetu.
Jumapili njema.
Pd. Lawrence Muthee, SVD
