Masomo ya Jumapili kwa Kifupi: Mkesha wa Pasaka & Jumapili ya Pasaka

Mkesha

Mwanzo 1:2-2; Mwanzo 22:1-18; Kutoka 14:15-15:1; Isaya 54:5-14; Isaya 55:1-11; Baruku 3:9-15, 32C4:4; Ezekieli 36:16-17, 18-28; Warumi 6:3-11); Mathayo 28:1-10

Upendo wa Mungu Umefunuliwa

Wapendwa, Katika Mkesha wa Pasaka, tunasherehekea usiku muhimu zaidi katika maisha yetu ya Kikristo. Ni usiku ambao hatima ya ulimwengu ilirejeshwa katika njia sahihi baada ya kuanguka kwa binadamu wa kwanza, Adamu. Kwa kufufuka kutoka kwa wafu, Yesu alifungua milango ya uzima wa milele kwa wote wanaotaka kuingia. Wale waliokuwa chini ya mateso na mifumo kandamizi walipata faraja, waliokata tamaa walipata matumaini, waliovunjika moyo wakapona, waliotelekezwa wakapata msaada, walio dhaifu wakapata nguvu, na waliochukiwa wakapata rafiki katika Yesu. Sasa tuna chaguo la mstakabali tunaotaka wenyewe, au tunaweza kuchagua Kristo na kutumainia uzima wa milele au kumkataa na kuwa na uhakika wa adhabu ya milele.

Wakati wa Misa ya mkesha wa Pasaka, Maandiko Matakatifu yanatukumbusha historia ndefu ya wokovu wetu ili kutukumbusha taabu ambayo Mungu alipitia kuwarejesha watu wake kwake. Katika Kumbukumbu la Torati 6, Musa aliwaamuru Waisraeli kusimulia matukio ya Pasaka kwa watoto wao katika vizazi vyote. Hili ndilo tunalopaswa kufanya kwa watoto wetu. Imani lazima ioteshwe na kupaliliwa katika maisha ya watoto na vijana kabla ulimwengu haujawateka akili na ahamu yao ya kujifunza mema. Ikiwa wazazi hawatajengewa uwezo wa kuwafundisha watoto wao imani vizuri, hawatakuwa na kitu cha kuwarithisha na tutaendelea kuwalaumu watoto na vijana kwa makosa ambayo sio yao.

Tunaweza kusema kwamba Mungu alituumba ili atuokoe. Hata hivyo, Mungu hakupanga kwamba mwanadamu apotee baada ya kumuumba ili aweze kuwaokoa baadae. Aliwapa uhuru wa kuchagua kumtii au kutomtii. Hata hivyo, hakuchelewa kuchukua hatua mara moja kuwaokoa walipomsaliti na kutenda dhambi dhidi yake. Yesu ni kilele cha mpango wa Mungu wa kuokoa watu wake. Ni alama ya kudumu ya wokovu uliotolewa kwa wote watakaomkubali yeye kama mwokozi.

Somo la kitabu cha Mwanzo sura ya 1 linasimulia jinsi Mungu alivyoumba kila kitu kwa mpangilio wa kushangaza na kukamilisha uumbaji wake wote kwa kuumba mwanamume na mwanamke. Mungu alitaka kuwashirikisha wanadamu upendo wake hivyo akawaandalia mahali pazuri pa kuishi pamoja naye kule shambani Edeni. Zaburi 104 inaelezea makuu ya uumbaji wa Mungu. Mara ngapi ninaketi na kuhesabu matendo ya ajabu aliyoyafanya Mungu katika maisha yangu? Au najua tu kulalamika kila wakati kwamba Mungu hatendi ninavyotaka?

Kitabu cha Mwanzo sura 22 inaelezea jinsi Mungu alivyoijaribu imani ya Ibrahimu. Baada ya kurejesha matumaini ya uzao kwa mzee huyu, Mungu anajaribu imani yake kwa kumwomba atoe sadaka chanzo pekee cha matumaini yake ya kuwa baba wa taifa kubwa ambacho ni Isaka mwanae wa uzeeni. Wengi wetu tungevunja uhusiano na Mungu na kuamua kubaki na kile tulichonacho mikononi mwetu. Tungesema bora ndege moja mkononi kuliko 100 hewani. Ibrahimu lazima awe alifikiria kwamba Mungu yule yule ambaye alimbariki na mwana katika uzee wake angekuwa na uwezo wa kumpa hata zaidi. Kwa hivyo, hakumzuia mwana wake kutoka kwa Mungu. Baadaye Mungu mwenyewe alimtoa Mwana wake wa pekee Yesu, ili afe kwa ajili ya wokovu wetu. Mara ngapi nimekataa kumtolea Mungu kile ninachokiita “changu” lakini ninajifanya kuwa ninashukuru kwa hicho hicho katika sala yangu. Je! Natoa zaka ya vile vyote ambavyo Mungu amenipa, au ni najigamba kwamba ni matunda ya jasho langu? Zaburi 16 ni wimbo wa imani katika msaada wa Mungu. Tunaitwa kuwa na imani katika mpango wa Mungu kwetu bila mashaka yoyote. Ninajuaje kuwa ni mpango wa Mungu unaoendelea katika maisha yangu sasa? Je! Nina imani katika msaada wa Mungu kama Ibrahimu?

Somo la Kitabu cha Kutoka sura ya 14 linaelezea maumivu ambayo watu wa Israeli walipitia walipovuka Bahari ya Shamu. Walikuwa na hofu kwamba Mungu aliwatoa Misri ili waangamie ufukweni mwa bahari kwa upanga wa Farao. Mungu kamwe hapangi kuhatarisha maisha ya watu wake bali hutumia fursa ya hatari kuonyesha utukufu wake. Siku hiyo, watu wa Israeli waliona nguvu ya Mungu ikifanya kazi kwa ajili yao. Kisha watu walimwimbia Mungu wimbo wa sifa kwa matendo yake ya ajabu. Tusije hata kwa sekunde moja, tukafikiri kwamba Mungu ametuacha kuteseka, badala yake, tutambue kwamba ni sisi tunaomwacha yeye na kuteseka kwa kukosa msaada wake. Mungu daima yuko upande wetu katika changamoto ikiwa tutamtumaini yeye.

Isaya 54 inatukumbusha kwamba mara nyingine Mungu anaweza kuonekana kana kwamba haangalii matatizo yetu lakini daima anatazama na kamwe hapendi tuteseke. Ingawa maumivu yetu yanatokana na chaguzi zetu mbayá n aza kijinga, Mungu haondoi rehema na huruma yake kutoka kwetu. Daima anataka kutuumba upya ikiwa tutampa nafasi. Kama tunavyosoma katika Zaburi 30, ikiwa tunamtumaini Mungu, hatutashindwa kamwe. Maadui wetu hawatashinda juu yetu.

Katika somo la Isaya 55 tunasoma kwamba kuna vinono vingi katika nyumba ya Bwana. Ikiwa tutasikiliza neno la Mungu, hatutasumbuka kwa sababu atafanya mambo yawe mepesi kwetu. Hata hivyo, tunahimizwa kutumia fursa wakati ingali ipo. Tujitie moyo kufanya hima kuokoa kilichosalia katika imani yetu, katika heshima yetu, na katika utu wetu.

Nabii Baruku anaeleza chanzo cha mateso ya Waisraeli utumwani. Kutokuwa na busara na kutotii amri za Mungu hutufanya tupoteze neema na ulinzi wake, hivyo tunatekwa na uovu. Busara na fadhila ndizo siri ya mafanikio na maisha marefu yenye amani. Zaburi 19 tunasoma kwamba amri ya Mungu ni safi na yenye kung’aa. Inaweza tu kutuletea mema kwetu. Usidanganywe kwamba ni upuuzi kuwa muumini. Imani kwa Mungu ndio bima pekee ya mustakabali wetu tunayoweza kuamini. Ahadi na mafanikio ya kidunia ni ya muda mfupi, na hayastahimili mtihani wa wakati. Ni mambo ya pata potea. Hakuna chemichemi ya furaha ya kudumu duniani. Mali za dunianiani haviwezi kutopa furaha naye mwanadamu huchoka haraka kufadhili.

Kutoka kitabu cha Ezekieli, tunaelezwa kwamba mateso ya Waisraeli uhamishoni Babeli yalitokana na dhambi zao. Walikuwa wametia unajisi Jina Takatifu la Bwana kwa kutotii amri zake. Hata hivyo, Mungu asema kwamba atawaokoa kutoka kwa Mataifa kwa ajili ya Jina lake Takatifu na sio kwa sababu ya mastahili yao wenyewe. Wokovu tunao sio leo sio kwa sababu ya mastahili yetu bali kwa sababu Mungu ni mwenye huruma na anatupenda.

Mtume Paulo, katika waraka kwa Warumi, anatukumbusha maana halisi ya kifo na ufufuko wa Kristo. Kwamba katika ubatizo tunakufa katika dhambi zetu na kufufuliwa naye katika maisha mapya. Zaburi 118 ni wimbo wa rehema na wema wa milele wa Bwana. Ukarimu na Wema ni sehemu ya asili ya Mungu, na hawezi kutenda kinyume na asili yake mwenyewe.

Injili inaelezea habari ya kushangaza ya ufufuko. Yule aliyethibitishwa kuwa amekufa na kaburi lake kulindwa na askari amemshinda mauti na kufufuka kama alivyoahidi. Mungu daima hutekeleza ahadi yake. Alimfufua Mwanae kutoka kwa wafu ili sisi pia tuweze kuwa na tumaini la kufufuliwa siku moja pamoja naye. Yesu alijaribiwa sana kukwepa hatma yake kwa sababu ya maumivu aliyoyajua yangempta. Lakini, alijitia moyo katika tumaini la ahadi ambayo Baba yake alimpa. Sisi pia tunaitwa kuwa hodari wakati wa mateso makali na kuchagua lililosahihi kwa kumtumainia Mungu.

Wapendwa, liturujia ya mkesha inatukumbusha historia ya wokovu wetu uliotokana na upendo mkubwa wa Mungu kwetu. Mungu alikusudia kuyaweka maisha yetu katika hali ambayo angeweza kutubariki. Hii ndiyo maana ya Ubatizo katika Kristo Yesu. Kama watu wanavyotapanya utajiri waliourithi au kupewa kwa sababu hawajui maumivu yaliyohusika kuukusanya, vivyo hivyo mtu ambaye haujui jinsi wokovu tulionao leo ulivyokuja hawezi kuuthamini. Kuna wabatizwa wengi ambao hawaendi Kanisani kwa sababu hawakuelezwa vizuri gharama ya wokovu. Wale ambao walikurupushwa katika katekesi bila kuchambua vizuri matendo ya wokovu mwishowe wanaiacha imani yao. Ikiwa wote waliopewa jukumu la kulelea imani imani watatekeleza wajibu wao, tutakuwa na waamini wazuri. Hawa ni wazazi, waalimu wa katekesi, walimu darasani, makasisi na watawa, maaskofu, na watumishi wa Mungu, wafanye kazi yao vizuri. Yesu yuko hai pamoja nasi, na anataka kushiriki maisha yake mapya pamoja nasi.

Jumapili ya Pasaka

Jumapili ya Pasaka: Matendo 10:34a. 37-43; Zaburi 118; Wakorintho wa Pili 3:1-4; Yohana 20:1-19

Mwanzo Mpya

Kila mara ninapotafakari nastaajabu kwamba Yesu alipofufuka, hakwenda katikati ya Mji wa Yerusalemu kujionyesha mwenyewe kwa wale waliomwua kama wengi wetu tungelifanya. Badala yake, alichagua kujidhihirisha kwa wanafunzi wake ambao aliwakabidhi jukumu la kuhubiri Habari njema ya ufufuko wake. Yesu hakupenda kwamba Habari ya ufufuko wake ipotoshwe. Hii ndiyo sababu Yesu alitamani kwamba ufufuko wake usiwe “Habari za hivi punde” kufasiriwa na kwasilishwa vibaya na waandishi wa habari kama ilivyo kawaida yao. Makuhani wakuu wa Kiyahudi walikuwa tayari wamewaonga askari ili washuhudie tofauti kabisa na waliyoyaona. Ni nani ninayemwamini kusimulia maisha yangu?

Yesu alitaka habari za ufufuko wake, zitangazwe na kuhubiriwa na watu ambao walimwamini na kumtumaini. Petro na wanafunzi wengine walitumia nguvu nyingi kuhubiri Habari Njema ya Kristo mfufuka. Waliteswa na kuitwa waongo na kusingiziwa kukufuru. Milenia mbili baadaye, Kanisa la Kristo bado linatumia nguvu nyingi kujaribu kueneza ujumbe huo huo wa wokovu kwa ulimwengu. Je! Unadhani vituo vya habari leo vingesimulia ukweli kuhusu ufufuko wa Yesu?

Petro anaelezea maisha ya Yesu na mambo mengi mazuri aliyoyafanya ili kuleta wokovu kwa wale waliosimkiliza. Yesu alipinga ubaguzi wa aina zote, aliponya magonjwa ya mwili, akili, na roho, alikosoa mamlaka kandamizi za wakati huo, na kuanzisha taasisi mpya ya wokovu katika wanafunzi wake yaani Kanisa. Yesu alipindua utaratibu wa ufisadi, ubaguzi, na udanganyifu uliotawala ulimwengu. Yesu alifichua unafiki na utapeli uliokidhiri katika dini. Hii ilimtengenezea adui wengi. Je! Wewe umewahi kuchukiwa kwa sababu ya kutenda mema?

Ufufuko wake wa ajabu uliweka utaratibu mpya wa wokovu kwa wale watakaokuwa wafuasi wake. Hawangekuwa tena watumwa wa mila za jadi, mifumo ya ufisadi, au nguvu za uovu. Kila mmoja alipata na uhuru wa kuchagua hatima yake mwenyewe.

Paulo anatuhimiza tuishi kama watu ambao wamefufuliwa na Kristo na si kama bandia. Tusitende kana kwamba hatukumjua Yesu kwa sababu huu ni usaliti kama ule wa Yuda. Pamoja naye, tunainuka kutoka makaburi mengi tuliyochimba na kuingia wenyewe. Makaburi ya chuki, wivu, uvivu, ufisadi, tamaa ya mali, n.k., na kuwa hai kwa upendo wa kweli, haki, amani, uchangamfu, na ukarimu, nk.

Tena, Injili inasmulia matukio ya asbuhi ya ufufuko wa Yesu. Maria Magdalene, mwanamke, anakuwa wa kwanza kupokea na kutangaza habari kuu ya ufufuko. Anakuta kaburi wazi, na mwili wa Yesu haupo. Petro na mwanafunzi mwingine bila kumwamini, wanakimbia kwenda kaburini kuthibitisha na wanapata mambo kama alivyowaambia. Bado hawakuwa wametambua kwamba Yesu alikuwa amewaambia kwamba angefufuka baada ya siku tatu. Walikuwa wamejawa na hofu, kukata tamaa, na huzuni. Yule mwovu ameshindwa, na kaburi haliwezi kushikilia uzima. Sisi sio watumwa wa dhambi na mauti tena bali wana wa Mungu kwa sababu Mwana ametuweka huru. Licha ya hii, leo wengi bado wanapendelea kuwa watumwa wa dunia kuliko kuwa huru katika Kristo. Je, wewe ni mtumwa au huru?

Wapendwa, fumbo la wokovu wetu ambalo kilele chake tunakifikia leo linatuletea furaha nyingi. Liturujia ya Kanisa inatupa kipindi hiki maalum cha Pasaka cha siku 50 mpaka Petekoste ili kuhishi upya maisha yetu kwa roho mpya na nia iliyoboreshwa. Tuendelea kuamini, kutumaini, na kupenda, huku tukijua kwamba hatima yetu imehakikishwa ikiwa tutasalia waaminifu kwa mwito wetu.

Heri ya Pasaka

Padre Lawrence Muthee, SVD

Leave a comment