Ayubu 7:1-4.6-7; Zaburi 147; 2 Wakorintho 9:16-19.22-23; Marko 1:29-39
Utume wangu ni upi?

Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, mataifa mengi duniani yaliamua kuwa na jukwaa la pamoja (Umoja wa Mataifa) kushughulikia si tu mizozo kati ya wanachama wake bali pia kuwa mdhamini wa haki za binadamu. Hata hivyo, miaka karibu 80 tangu tangazo la haki za binadamu, sehemu kubwa ya idadi ya watu duniani hawawezi kufurahia haki hizi. Pamoja na utajiri ulioenea duniani, wengi wanaishi katika umaskini mbaya kwa sababu ya ukosefu wa usawa wa kiuchumi, upendo, na udugu. Kinaya ni kwamba, huku maskini wakitamani siku moja watakuwa matajiri na kuwa na furaha, matajiri wanatamani wangeweza kuwa na furaha kama maskini walivyo.
Siku moja nilitembelea mtaa mmoja wa mabanda maarufu katika jiji kubwa na marafiki kutoka nchi moja ya Magharibi iliyoendelea sana. Ilikuwa mara yao ya kwanza kutembelea eneo kama hilo. Tulipokuwa tunaondoka huko, mmoja wao alikuwa kimya sana na nilipoangalia kwenye kioo cha nyuma cha dereva, niliona machozi yakilengalenga machoni mwake. Nilipomuuliza kwa nini alikuwa analia, alisema ni kwa sababu tofauti na wanavyoona kwenye televisheni, watu katika mtaa huo, ingawa wanavyoonekana kuwa maskini sana na hali ya miundo mbinu yao ni mibaya sana, kila mmoja alionekana kuwa na furaha huku akiendelea na shughuli zake. Watoto walikuwa na furaha kuwaona na waliwafuata kwa kuwapungia na kuwasalimia “how are you” (Habari yako). Aliongeza kwamba kwao, ingawa wengi wana vitu vyote vya kimwili wanavyohitaji, wengi wao hawana furaha kama watu wa mtaa huu wa mabanda. Kwamba huko kwao watu wasio na kazi, hata kama serikali inawapa mahitaji yao ya msingi, wanaishi maisha yenye huzuni sana.
Somo la kwanza kutoka kitabu cha Ayubu linatupa mfano wa kutafakari. Tunajua kwamba Ayubu alikuwa mtu mwadilifu aliyefanyiwa majaribu makali na yule mwovu. Baada ya kupoteza vyote alivyokuwa kumiliki, Ayubu anatafakari juu ya maisha yake na kufikia hitimisho hili: “kwamba maisha ya mwanadamu duniani ni mapambano na siku zake ni kama siku za kibarua.” Hii ni kumbusho zuri kwetu hasa tunapofikiri kwamba tunaweza kupata furaha ya kweli katika vitu vya dunia na tunalegea katika majukumu yetu na ahadi za Kikristo. Nguvu za uovu zinavutia zaidi kuliko hamu ya kutenda mema. Hii ni kwa sababu uovu daima unajitambulisha kwa njia inayovutia na nzuri. Hata Mtume Paulo mwenyewe anasema, “Kwa maana sitendi mema nilitakalo, bali mabaya nisiyotaka hayo ndiyo nayatenda.” (Warumi 7:19). Mapambano yetu leo ni kutofautisha kati ya halisi na bandia. Kamwe tusimhukumu mtu kwa yale anayoyapitia, kwa sababu sisi si bora kuliko wao, ni rehema tu za Mungu zinazotuwezesha kufanikiwa. Sote ni dhaifu na tupo hatarini kwamba leo tunaweza kuwa na afya njema na kesho hali ikabadilika.
Mzaburi anatukumbusha kwamba Mungu wetu ni mwenye huruma, naye anawatunza watu wake. “Huponya waliopondeka moyo, na kuwaponya majeraha yao.” Hata tunapofikiri kwamba hatuhitaji Mungu katika Maisha yetu, bado yeye ana Subira na sisi, na kutuokoa kutokana na changamoto tunazojitia wenyewe ikiwa tutashirikiana na neema yake.
Mtume Paulo anatukumbusha kwamba wito wetu wa Kikristo si kuitwa kujitenga na dunia na kutuweka mahali pa kustarehe tukisubiri kuchukuliwa mbinguni. Badala yake ni mwito wa kushiriki katika utume wa Kristo, ambao daima unavutia upinzani na machungu. Shetani ni anashughulika zaidi kanisani kuliko mitaani. Anajua wapi mtego unavyostahili jitihada. Paulo anaelewa kwamba wito wake ulikuwa wa dharura kwa sababu wengi walipotea katika kukosa kumtambua Yesu kama Masiha. Mwenyewe alilitesa Kanisa kwa sababu alikuwa amepofushwa na imani yake za kitamaduni. Paulo alidhani alikuwa sahihi kusafisha dini yake ya kurithi kutokana na upotovu mpaka Yesu alipokutana naye njiani kwenda kuwatesa Wakristo huko Damasko. Mara ngapi sisi hutenda kama Paulo tukijiamini kwamba tunafanya lililo sahihi?
Katika Injili ya leo, matendo ya Yesu yanamwonyesha kama Masiha asiyejali siasa bali anayejitolea kuokoa watu kutoka maradhi, ujinga, na uovu. Yeye ni kama rafiki anayefika wakati tunahitaji msaada zaidi. Leo, anawatembelea Simon na Andrea hadi nyumbani mwao na kuponya mama yao aliyekuwa na homa. Pia anawaponya majirani wagonjwa waliyosikia na kufika kubisha mlango. Hivi ndivyo itakavyokuwa ikiwa tunamwalika Yesu nyumbani mwetu na kuwakaribisha majirani wetu waponywe naye. Mtaa wetu utakuwa na furaha na salama kwa wote. Kinaya ni kwamba leo ni majirani wanaosali hata pamoja hawaonani uso kwa uso.
Wapendwa, sote tumepewa utume wa kutimiza katika ulimwengu huu. Tunahitaji kutafuta mwanga ili tuweze kutambua wito wetu wa kweli na kuomba Yesu atupe hekima ya kuutekeleza itupasavyo. Utume wangu (yaani maneno yangu, mawazo yangu, na matendo yangu) lazima daima uwe na nia ya kuunganisha kilichovunjika, kuponya kilichoumia, na kurejesha kilichopotea na sio kinyume chake. Je! Umetambua utume wako?
Nawatakia Jumapili yenye baraka.
Pd. Lawrence Muthee, SVD
