Masomo ya Jumapili kwa Kifupi wiki ya 4 B

Kumbukumbu 18:15-20; Zaburi 94(95); 1 Wakorintho 7: 32-35 Marko 1:21-28

Maksudi ya Mungu

Wapendwa, leo ni Jumapili ya Nne katika Kipindi cha Kawaida Mwaka B. Katika masomo ya leo, mada inayojitokeza ni njia ya Mungu ya kufanya mambo na jibu letu kwa njia hii. Mungu yu karibu na daima anapenda kuingilia kati maishani mwetu, lakini lazima tuwe karibu naye na kumruhusu afanye hivyo. Tunaweza kulinganisha uzuri wa kuwa karibu na Mungu na nini? Ni kama mahali pazuri ambapo tunasikia na labda tumeona hata picha zake. Ili tufurahie uzuri huo kwa kikamilifu, lazima tuwepo pale. Ikiwa tutapatembelea kwa masaa machache au siku chache na kuondoka, uzuri huo utabaki tu kumbukumbu. Wengi wamebatizwa lakini hawapati kabisa uzuri wa uwepo wa Mungu kwa sababu waliondoka mara tu baada ya ubatizo. Kuhudhuria kanisani Jumapili na kutoa sadaka haimaanishi kila wakati kuwepo katika ufalme wa Mungu. Kusikiliza neno la Mungu na kuruhusu liguse na kubadilisha maisha yetu ndiyo kuwepo kikamilifu katika ufalme wa Mungu. Je, wewe upo kikamilifu katika ufalme wa Mungu?

Katika somo la kwanza leo, watu wa Israeli wanahangaika kuhusu mustakabali wao kwani Musa, aliyewaongoza katika safari yao kwa muda mrefu jangwani, alikuwa mzee sana na hawakuwa bado wamevuka kuingia nchi ya ahadi. Musa anawafariji watu kwamba Bwana Mungu atainua nabii mwingine kama yeye atakayewaongoza. Wakati Mungu alipomwita kuwaongoza watu wa Israeli kutoka Misri, hakufikirim kwamba angekuwa na uwezo wa kufanya kazi ambayo Mungu alikuwa anamtuma kuifanya (Kutoka 4:1-18). Lakini Musa aliendelea kuwa katika uwepo wa Mungu na hivyo akafanikiwa katika utume wake. Je, umewahi kushindwa katika maisha yako? Angalia umbali ulioacha kati yako na Mungu labda utapata jibu.

Wapendwa, wakati mwingine tunapopanda ngazi katika jamii na kufika juu, tunashawishika kufikiri kwamba tutadumu huko milele. Tumeona jinsi baadhi ya viongozi wanavyojaribu njia zisizo halali kubaki madarakani. Katika nafasi zetu ndogo au kubwa, uenda ikawa tunang’ang’ania mamlaka na hatupo tayari kuziachia nafasi kwa wengine. Tunasahau kuwa hata kama tutashikilia madaraka, siku itafika wakati miili yetu dhaifu itashindwa. Musa alikuwa tofauti na kuwa alijua kwamba wakati wake uliwadia kwa sababu ya uzee wake, alimjengea Joshua uwezo wa kuchukua uongozi baada yake. Ni upi mtazamo wangu kuhusu nafasi za uongozi?

Nabii ni msemaji wa Mungu. Neno linalotoka kinywani mwake lazima liwe neno la Mungu. Ikiwa nabii atapotoka na kuanza kusema neno lake mwenyewe au la marafiki zake, Mungu anamwambia Musa kuwa huyo hataendelea kubaki katika nafasi yake. Tunajua watu wengi walioanza uongozi wao vizuri lakini katikati wakamsahau Mungu na kuanza kuzingatia maslahi yao binafsi. Hawa mwishowe wanakataliwa na Mungu kama Mfalme Sauli. Mara tu Mungu anapojiondoa kutoka kwetu, kila kitu kinaporomoka. Ni rahisi zaidi kupata nafasi kubwa pamoja na kuwa na nia nzuri ya kutumikia, lakini kubaki mwaminifu kwa lengo ndiyo changamoto ya wengi. Unafikirije?

mzaburi anatukumbusha tuisikiapo sauti ya Mungu tusifanye migumu mioyo yetu. Mungu daima anatujali kwa sababu sisi ni wake. Hata hivyo, mara nyingine tunajitenga naye au kuifanya mioyo yetu kuwa migumu. Tunashawishika haraka na vivutio vya dunia lakini hatuchukui hata muda wa kutambua Mungu anatuomba nini. Tunamtafuta Mungu tu tunapokuwa na matatizo na tumeishiwa maarifa. Mara nyingine, tunatoa visingizio vingi vya kutotimiza majukumu ya imani yetu.

Katika barua yake ya kwanza kwa Wakorintho, Paulo anatusisitiza kudumisha ahadi yetu isiyogawanyika kwa Mungu. Kuna miito miwili mikubwa ambayo  ambayo mwanadamu anaweza kuchagua ili kumtumikia Mungu. Maisha ya ndoa ambayo lengo lake kuu ni kumfurahisha Mungu katika familia, au kama maisha ya useja ambayo lengo lake kuu ni kuwa mjumbe wa upendo wa Mungu kwa wengine. Paulo anatoa maoni yake juu ya miito yote lakini bila shaka, anasisitiza wito aliouchagua mwenyewe. Anasema kwamba wale wanaobaki bila kuoa wanajiweka wakfu wakati wao wote na rasilimali zao binafsi kwa utumishi wa Mungu wakati wale wanaooana wana hamu iliyogawanyika, yaani, kumfurahisha Mungu na mwenzi wao. Jambo muhimu ni kwamba, lolote tunalochagua, ni lazima tuwe tutambue njia inayofaa kulitimiza.

Katika somo la Injili, tunasikia jinsi Yesu alivyokuwa akaponya watu na kuwatoa pepo. Pepo walijua Yesu ni nni na walimwogopa kwa sababu uwepo wake ulimaanisha mwisho kwao. Yesu ana mamlaka ya kuwatoa pepo wote ndani yetu ikiwa tutampa nafasi. Watu walistaajabu kwa sababu mamlaka ya Yesu juu ya pepo yalikuwa wazi. Hakuhitaji kupiga kelele mara elfu moja au kuomba pepo waondoke kama manabii wa kisasa wanavyofanya mitaani na masokoni. Kwa sababu ya hitaji kubwa la kutolewa mapepo na miujiza ya kuigiza imewafanya wengi kuwekeza katika biashara hiyo. Najua watu ambao si wahubiri lakini wamewekeza katika “vituo vya miujiza” na haa radio ambapo wanawalipa wahubiri na watoa pepo. Vituo hivi hukusanya kiasi kikubwa cha pesa kutoka kwa watu wengi waliovunjika na kuchanganyikiwa. Kwa kushangaza, wengi wanaotafuta huduma hizi ni wanawake na wengi wa wanaowatoa pepo ni wanaume.

Wapendwa, kila mmoja ameitwa kuishi wito fulani duniani. Mwandishi maalufu, marehemu Myles Monroe, anasema kwamba kitu kikubwa unachoweza kugundua katika ulimwengu huu ni kusudi lako. Tunaweza kujua hili tu ikiwa tunabaki karibu na Muumba wetu na kumruhusu atuongoze. Je, umegundua kusudi lako katika ulimwengu huu ni lipi?

Muwe na Jumapili yenye Baraka,

Pd. Lawrence Muthee, SVD

Leave a comment