Kuzaliwa: Novemba 5, 1837, Goch, Ujerumani
Kuanzisha Shirika: Shirika la Neno wa Mungu,
Masomo: Chuo cha Bonn
Kufa: Januari15, 1909, Steyl, Uholanzi
Kufanyika Mwenye Heri: 19 Oktoba 1975, na Papa Paulo VI
Kufanyika Mtakatifu: 05 Novemba 2003 Roma na Papa Yohana Paulo II
Siku Kuu: 15 January

Arnold Janssen alizaliwa Novemba 5, 1837 huko Goch, mji mdogo katika eneo la Rhineland Chini (Ujerumani). Akiwa wa pili kati ya watoto kumi, wazazi wake walimjengea upendo mkubwa wa imani Katoliki. Alipata daraja la upadre tarehe 15 Agosti, 1861 katika jimbo la Muenster na akapewa jukumu la kufundisha Sayansi Asilia na Hisabati katika shule ya sekondari huko Bocholt. Huko alijulikana kwa kuwa mwalimu mwenye nidhamu lakini mpenda haki. Kwa sababu ya kujitolea kwake kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Jimbo wa Utume wa Sala. Utume huu ulimtia moyo Arnold kufungua moyo wake kwa Wakristo wa madhehebu mengine.
Pole pole alianza kutambua mahitaji ya kiroho ya watu zaidi ya mipaka ya jimbo lake mwenyewe, na kuwa na shauku kubwa la utume wa ulimwengu mzima wa Kanisa. Aliamua kujitolea kuamsha jukumu la kimisionari la Kanisa la Ujerumani. Akiwa na lengo hili, mwaka 1873 aliacha kazi yake ya kufundisha na muda mfupi baadaye akaanzisha, Gazeti la Utume Mdogo wa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Gazeti hili maarufu la kila mwezi lilikuwa likiangazia habari na shughuli za utume na kuhamasisha Wakatoliki wa Ujerumani kufanya zaidi kusaidia misioni.
Hizi zilikuwa nyakati ngumu kwa Kanisa Katoliki nchini Ujerumani. Bismark alizindua “Kulturkampf” na sheria kadhaa za kupinga Kanisa Katoliki, ambazo zilisababisha kufurushwa kwa mapadre na watawa na kufungwa kwa maaskofu wengi. Katika hali hii ya machafuko, Arnold Janssen aliwasilisha wazo kwamba baadhi ya mapadre waliofurushwa wangeweza kwenda kwenye misioni za nje au angalau kusaidia katika maandalizi ya wamisionari. Pole pole lakini kwa hakika, na kwa ushawishi kidogo kutoka kwa Askofu Vikari wa Hong Kong, Arnold aligundua kwamba Mungu alikuwa akimwita kutekeleza kazi hii ngumu. Wengi walidai kwamba hakuwa mtu sahihi kwa kazi hiyo, au kwamba wakati haukuwa sahihi kwa mradi kama huo. Jibu la Arnold lilikuwa, “Bwana anatupa changamoto ya imani yetu kufanya kitu kipya, hasa wakati mambo mengi yanaporomoka katika Kanisa.”
Kwa msaada wa maaskofu kadhaa, Arnold alifungua nyumba ya kwanza ya misioni tarehe 8 Septemba 1875 huko Steyl, Uholanzi, na hivyo akaanzisha Shirika la Wamisionari wa Neno wa Mungu. Tarehe 2 Machi 1879, wamisionari wawili wa kwanza waliondoka kwenda China. Hao walikuwa Mt. Joseph Freinademetz, Pd. John Baptist Anzer.
Akitambua umuhimu wa machapisho katika kuvutia wito wa kimisionari na ufadhili, Arnold alianzisha mtambo wa kuchapisha miezi minne tu baada ya kufunguliwa kwa nyumba ya misioni. Maelfu ya watu waamini walei walichangia muda wao na juhudi kusaidia katika kusambaza magazeti kutoka Steyl. Tangu mwanzo, shirika jipya lilijitokeza kama jumuiya ya mapadre na mabruda.
Wanaume na wanawake wengi walijitolea kufanya kazi katika nyumba mpya ya misioni. Tangu mwanzo kabisa, kundi la wanawake kadhaa, ikiwa ni pamoja na Mwenyeheri Maria Helena Stollenwerk, walitumikia jumuiya. Lakini walitamani kutumikia misioni kama watawa. Huduma ya wanawake hao ya kujitolea isiyo na ubinafsi, na ufahamu wa jukumu muhimu la wanawake katika kufikia malengo ya utume, vilimchochea Arnold kuunda shirika la kimisionari la “Watumishi wa Roho Mtakatifu,” SSpS, tarehe 8 Desemba 1889. Masista wa kwanza waliondoka kwenda Argentina mwaka 1895.
Mwaka 1896, Padre Arnold alichagua baadhi ya masista ili kuunda tawi la kusali kwa kujitenga, lililofahamika kama “Watumishi wa Roho Mtakatifu wa Ibada ya milele (Kuabudu ya Muda Wote),” SSpSAP. Huduma yao kwa misioni ilikuwa kudumisha Ibada kuabudu ya Ekaristi Takatifu muda wote, kusali mchana na usiku kwa ajili ya kanisa na hasa kwa ajili ya jumuiya hizo nyingine mbili za wamisionari.
Arnold alifariki tarehe 15 Januari 1909. Alitawazwa Mwenye Heri 19 Oktoba 1975, na Papa Paulo VI, na kutawazwa kuwa Mtakatifu 05 Novemba 2003 Roma na Papa Yohana Paulo II. Maisha yake yalijaa na shauku ya kutafuta mapenzi ya Mungu, imani kubwa katika upendo wa Mungu, na kazi kwa bidii. Kwamba kazi yake imebarikiwa inaonekana katika ukuaji uliofuata wa mashirika aliyoanzisha: zaidi ya Wamisionari wa Neno la Mungu 6,000 wanafanya kazi katika nchi 80, zaidi ya Masista wa Roho Mtakatifu3,800, na zaidi ya Masista wa Roho Mtakatifu wa Ibada ya Milele 400.
Shirika la Neno wa Mungu lilifika kanda ya Africa Mashairiki 1984 katika Jimbo la Meru Nchini Kenya na baadae Tanzania mwaka 2000 katika Jimbo Kuu la Arusha. Mapadre na Mabruda wa Shirika wanahudumu katika Parokia za Tokeo la Bwana Burka (2000), Yesu Mchungaji Mwema Simanjiro (2002), Mt. Agustino Orkesumet (2010) na Mt. Yosefu Mfanyakazi Olasiti, (2013).
SALA YA MTAKATIFU ARNOLD JANSSEN
Mungu Kweli ya milele – Tunakuamini
Mungu nguvu yetu na wokovu wetu – Tunakutumainia
Mungu Mwema kabisa – Tunakupenda kwa mioyo yetu wote
Umemtuma Neno kama Mkombozi wa ulimwengu – Tafanye tuwe kitu kimoja kwake
Tujaze na Roho wa Mwanao – Ili tutukuze Jina lako, Amina
Giza la dhambi na usiku wa kutokuamini vitokomee mbele ya mwanga wa Neno na Roho ya neema, Na Moyo wa Yesu uishi ndani ya mioyo ya watu wote. Amina
