Masomo ya Jumapili kwa kifupi 2 B
1 Samweli 3:3-10.19; Zaburi (39)40; 1 Wakorintho 6:13-15.17-20 Yohana 1:35-42
Wito Wangu

Wapendwa, leo ni Jumapili ya pili katika kipindi kifupi cha Wakati wa Kawaida ambacho kitatangulia kipindi cha Kwaresima. Wakati wa Kawaida, masomo ya liturjia yanatuongoza kupitia historia ya wokovu. Leo tunajifunza kuhusu mwanzo wa utume za Samweli na Yesu.
Katika kitabu chake “Kuachilia Uwezo Wako,” marehemu Myles Monroe anasema kwamba wengi huishi na kufa bila kugundua kusudi la kuwepo kwao duniani au kuachilia uwezo ambao Mungu aliweka ndani yao walipoumbwa. Hii inaweza kuwa kutokana na sababu mbalimbali. Baadhi ni ya hizi ni kama vile mazingira walikozaliwa na kukulia, mfano watu waliokulia katika familia zenye matatizo, mitaa duni, kambi za wakimbizi, maeneo ya vita, au wale waliopoteza wazazi wao wakiwa wachanga. Kwa kawaida, watoto wanatarajiwa wazaliwe katika familia yenye wazazi wote wawili wanaowasaidia kukua kimwili, kiakili, kiroho, n.k. Kisha wawpeleke shuleni ambapo walimu huwasaidia kugundua na kukuza uwezo wao kama wataalamu. Hata hivyo, tunajua kwamba hii sivyo hali ilivyo kwa kila mtu kutokana na sababu zilizotajwa hapo juu.
Hata hivyo, tunajua kwamba Mungu daima hujali watu wake na kutuita kutoka katika mazingira tofauti ili kutimiza mpango wake ulimwenguni. Katika somo la kwanza, tunasikia kuhusu wito wa Samweli. Hii ilikuwa wakati Eli kuhani mkuu alikuwa mzee na kipofu. Watoto wake walitarajiwa kumrithi katika huduma huko Hekaluni lakini badala yake, waliasi na kufanya maovu mbele za Mungu. Pia ilikuwa ni “kipindi kavu” kwa taifa la Israeli kwa sababu Mungu hakuwa amesema na watu wake kwa muda mrefu. Kama manabii wengine wengi, wito wa Samweli ulianza na kuzaliwa kwa njia ya muujiza kwa sababu mama yake, Hanna, alikuwa tasa na alikuwa mzee sana wakati Samweli alipozaliwa.
Mungu alimuita Samweli mara 3 kabla ya kugundua, kwa msaada wa Eli, kwamba ni Mungu aliyekuwa akimwita na akaweza kujibu mara ya 4. Tuseme kwamba Samweli alikuwa na bahati ya kuwa mahali sahihi kupata ushauri sahihi. Sote tunahitaji ‘Eli’ katika safari yetu ya kujitambua. Mungu anaweza kutuita mara nyingi lakini kwa sababu ya machafuko na sauti nyingi duniani leo, hatuwezi mara moja kutambua kwamba ni Mungu anatuita. Baadhi pia wamedanganywa wanapojaribu kutamua wito wao kutoka kwa watu na mahali ambao sio sahihi na salama. Kuna watu wengi ambao wapo katika mahusiano ambao wanasema laity wangalijitambua mapema wangeepuka mahusiano hayo kwa mbali kabisa. Kuna manabii wa uongo wengi ambao wanadai kwamba wana majibu ya moja kwa moja kutoka kwa Mungu na wanaweza kutafsiri siri kutoka kwa Mungu kwa kila mtu ikiwa atalipa ada kiwango fulani.
Wengi pia wameiga ‘Eli’. Ni dhahiri kwamba wengi wa hawa ‘Eli’ wameishi kulingana na wito wao na wamesaidia wengi kutambua miito yao na kuachilia uwezo wao. Wengi wetu pia tumenufaika kutokana na hawa Eli na tukawa Eli sisi wenyewe. Hata hivyo, wengine wamegeuka kuwa matapeli ambao badala ya kuwasaidia watu kutambua miito yao, wanawatumia kwa masilahi yao binafsi. Ingawa Eli alijua kwamba wakati wake katika utume wa hekalu ulikuwa umekwisha, na alikuwa ameshindwa katika kuwarudi wanawe, hakumpotosha Samweli bali badala yake alimwelekeza kusema ndiyo kwa Bwana. Wakati mwingine kwa sababu ya hisia uoga, mara nyingine tunawaongoza watu vibaya ili tuweze kulinda nafasi na masilahi yetu.
Wito wa Samweli ulileta habari mpya kwa watu wa Israeli, na ilikuwa wakati wake ndipo ufalme uliporejeshwa kwao kwanza kupitia Mfalme Sauli na zaidi kupitia Mfalme Daudi. Subira ya muda mrefu hatimaye ilileta matunda kama mwimbaji zaburi anavyotuambia: Ikiwa tunamngojea Bwana, hatutavunjika moyo. Mungu hataki chochote kutoka kwetu kama malipo kwa baraka zake bali tu tumsikilize na tuwe na moyo wa kumtii. Mara nyingine tunafikiri tunaweza kumpendeza Mungu kwa zawadi na maneno mengi ya sifa, lakini kama hatutilii maanani neno lake na kujitolea kwa kazi yake, sifa zetu na ibada zetu ni bure.
Mtume Paulo anatukumbusha kwamba miili yetu ni hekalu la Roho Mtakatifu na tunapaswa kuiweka safi na mbali na uovu wote unaomzuia Roho Mtakatifu kuishi ndani yetu. Miili ni chombo cha kutimiza mpango wa Mungu maishani mwetu. Tunahitaji kuziweka safi na nzima kila wakati. Je! Unajua kwamba kuhatarisha afya yako mwenyewe ni dhambi kali?
Kama Eli, Yohane Mbaptizaji alitimiza wito wake kama kungo kati ya watu na Yesu. Yohane hakusita kuwaonyesha wanafunzi wake Masihi wanayepaswa kumfuata. Kama Eli, alijua kwamba utume wake ulikuwa umekamilika na ulikuwa wakati wake kufifia ili Yesu achukue nafasi. Wanafunzi wa Yohane walimfuata Yesu ambaye alipowaona wanamfuata aliwaita waandamane naye ili waweze ‘kuona’ na kujifunza zaidi juu yake. Yesu hakuhakutaka kuwaeleza juu ya makao yake barabarani, lakini badala yake aliwaalika kuwa pamoja naye. Si rahisi kuelewa wito wetu katika mitaa na barabarani. Tunahitaji kukaa muda mrefu na Yesu ili tuweze kujifunza zaidi juu ya utume yake na jinsi ya kushiriki katika utume huo kama wafuasi wake – wakristu.
Baada ya kumjua Yesu, lazima tutafute wengine na kuwaleta kwake kama vile Andrea alivyofanya. Ni wajibu wetu wa Kikristo kushirikisha wengine tunachokiona kutoka kwa Yesu ili nao pia waweze kukaribia zaidi na kujifunza wenyewe. Mwanamke Msamaria pia alifanya hivyo alipokutana na Yesu kwenye kisima. Alienda nyumbani na kuwaambia watu wake kwamba amemwona Masihi. Je! Tunasambaza habari njema na chanya kwa wengine, au sisi ni wataalam wa kusambaza uvumi na umbea kuhusu wengine?
Wapendwa, tujitahidi kutafuta msaada katika maeneo sahihi ili tuweze kugundua wito wetu wa kweli katika ulimwengu huu. Pia tunahitaji kutumia muda wa kutosha na Yesu ili atufundishe kuhusu ufalme wa Mungu, na baada ya kugundua, tuwashirikishe wengine pia.
Muwe Jumapili yenye baraka.
Pd. Lawrence Muthee, SVD
