Masomo ya jumapili kwa kifupi: Familia Takatifu

Masomo ya jumapili kwa kifupi: Familia Takatifu

Mwanzo 15:1-6,21:1-3; Zaburi 105; Waebrania 11:8,11-12. 17019; Luka 2:22-40

Familia: Msingi wa Jamii

Wapendwa, leo ni sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Hii ni familia ambayo ni mfano bora kwa familia zote za Kikristo. Kila mwanafamilia alitimiza majukumu aliyopewa na Mungu kwa uaminifu ili kufikia wokovu kwa binadamu. Tunawajibika kuwaenzi kwa hili, na njia pekee tunayoweza kuonyesha shukrani yetu kwao ni kujifunza kutoka kwao na kuiga tabia yao katika familia zetu wenyewe. Watu wengi wamebarikiwa kwa sababu ya familia hii. Je, familia yangu ni baraka kwa wengine?

Familia ni taasisi ya kwanza ya binadamu iliyoundwa na Mungu kwa ajili ya ukuaji na maendeleo ya watu wote wanaokuja duniani. Hapo ndipo mambo yote yanapoanzia. Ikiwa familia ni imara na thabiti, jamii na taifa zinanufaika kwa kuwa kutakuwa na viongozi na raia wenye maadili. Ikiwa familia imevunjika, jamii pia itakuwa imevunjika.

Familia huanzia pale ambapo watu wawili, mwanamume na mwanamke, wanapokutana na kuamua kushirikishana kila Maisha yao na vyote walivyonavyo. Katika Kitabu cha Mwanzo 1:26-28, tunasoma kwamba Mungu alimuumba mwanadamu na mwanamke kwa sura na mfano wake mwenyewe, aliwabariki na kuwaamuru wazae na kujaza dunia. Mungu ndiye aliyeongoza ndoa ya kwanza kati ya mwanamume na mwanamke.

Somo la kwanza linasimulia hadithi ya mzee Ibrahimu, aliyekuwa na huzuni kwa sababu alikuwa tayari mzee, mkewe Sara alikuwa amepita umri, na hawakuwa na mrithi. Ingawa alikuwa amezungukwa na watoto wa watumishi wake, alikuwa mtu mwenye huzuni. Hata hivyo, Ibrahimu alikuwa mwaminifu kwa Mungu matokeo yake; Mungu alifuta huzuni yake kwa njia ya ajabu kwa kumpa mwana katika hali isiyokuwa na matumaini na isiyowezekana. Je, uko katika hali inayoonekana haina matumaini sasa? Vema, kila kitu kinawezekana kwa Mungu.

Ni katika familia tunakotarajia kupata upendo na joto tunalohitaji. Familia ni shule ya maadili kwa wanachama wote. Inapaswa kuwa mahali salama zaidi ambapo mtu anaweza kutafuta hifadhi wakati wowote. Familia ni msingi wa jamii. Familia ni taasisi ambayo haiwezi kubadilishwa na kitu kingine chochote.

Hata hivyo, leo kuna changamoto nyingi zinazokabili taasisi hii na ambazo zimeiondolea utakatifu na usalama. Mungu alipoumba ulimwengu na binadamu, aliufanya kwa umakini mwingi na kuweka nidhamu, na utaratibu wa asili. Mwishowe alimuumba mwanamume na mwanamke na kuwapa uhuru juu ya viumbe vingine vyote. Walipaswa kutunza uumbaji wa Mungu kwa faida yao wenyewe. Kama tunavyojua wote, uhuru huu ulisababisha mwanadamu kuharibu kilichokuwa kitakatifu kwa tamaa mbaya. Leo mambo yamekuwa mabaya zaidi. Wengi wanateseka katika ulimwengu huu kwa sababu ama hawana familia au familia zao zimesambaratika. Baadhi hawakuchagua kuwa katika hali hii lakini wengi wanateseka kwa sababu ya maamuzi waliyofanya wao au wanafamilia wao.

Kuna familia nyingi zilizovunjika katika jamii yetu leo kwa sababu upendo na nidhamu inayopaswa kuwaweka pamoja haipo tena. Baadhi zinavunjika kwa sababu ziliundwa kwenye msingi legevu au nia potovu kuanzia mwanzo. Kama Padre, mara nyingi nakutana na kesi nyingi za familia zilizovunjika au zilizopo katika hatari ya kuvunjika. Wengi wao wanajikuta katika hali hii kwa sababu mambo hayakufanyika vizuri tangu mwanzo. Wengi wanapitia mateso makubwa kwa sababu ya machafuko yanayosababishwa na baadhi ya wanafamilia wao. Wengi wa wahanga ni wanawake na watoto. Wanaume pia wanateseka lakini wangependelea kutokuzungumzia hayo.

Wakati mwanaume na mwanamke wanapoamua kuishi pamoja na kuzaa watoto bila kufundishwa maadili yoyote ya kuwaongoza muunganiko huo hauwezi kuwa familia na, mwishowe, uishia kusambaratika. Ingawa binadamu wanashiriki sifa nyingi na wanyama wengine kama uwezo wa kuzaa, wao ni zaidi ya wanyama. Watu wengi huchagua kuishi katika hali ya wanyama na kukataa kupanda hadi kiwango cha binadamu. Mungu aliwaumba mwanamume na mwanamke akawapa akili na utashi ili waweze kuishi kama yeye. Katika tamaduni nyingi za jadi, familia zinathaminiwa lakini kuna mpangilio baguzi wa heshima miongoni mwa wanafamilia. Wanawake kwa kawaida wanachukuliwa kuwa watumishi au watumwa wa waume zao. Ni wazi kuwa jamii inayokandamiza wanawake inabakia nyuma kimaendeleo.

Faida ya familia za Kikristo ni kwamba wanafamilia ufahamu jukumu lao la kujenga jamii imara inayomcha Mungu. Viongozi wa kidini wanapaswa kuwafahamisha na kuimarisha umoja wa familia. Hata hivyo, tunachoshuhudia leo ni manabii, madhehebu, na hata vyama vya kitume visivyothamini umoja wa familia. Jambo la kusikitiza ni kwamba familia nyingi zimevunjika kwa sababu ya mafunisho potovu ya hawa. Yesu hakika si sehemu ya hayo. Hauwezi kuwa na mmoja au baadhi ya wanafamilia “waliookoka” na wengine hawajaokoka na kutarajia pawe na umoja katika familia hiyo. Siku hizi injili ya maendeleo ya mtu binafsi imejichukua nafasi kubwa na wanayoiendeleza wanahidi utajiri wa haraka. Hharama yake familia kusambaratika. Wapendwa, ikiwa utakutana na mtu anayejali tu wokovu wako binafsi na hana haja na familia yako, tafadhali kimbia.

Kila kundi la imani lisilofundisha na kuchochea umoja wa familia linapaswa kuvunjwa na viongozi wake kukamatwa kwa sababu wanaharibu uti wa mgongo wa jamiii ambao ni familia. Tuna ufisadi mwingi katika jamii yetu kwa sababu watu hawajapata maadili ya msingi tangu mwanzo wa maisha yao. Watu wanaokulia katika familia zilizovunjika na sasa wapo katika nafasi kubwa katika utumishi wa umma wanatuchanganya. Wataendelea kuiharibu jamii daima ikiwa hawakupata malezi ya kimaadili.

Wapendwa, tunapoadhimisha sikukuu ya Familia Takatifu, na tuangalie jinsi tunavyojenga familia zetu. Ikiwa tuna matatizo, tunaweza kuchukua hatua kabla hatujachelewa.
Kwa wale ambao familia zao tayari ziko katika matatizo, kuna mengi ambayo mtu binafsi anaweza kufanya kurekebisha mambo. Tafuta msaada kutoka kwa watu na mahali sahihi. Asili ya Shetani ni kuharibu na kugawanya, na kazi yake kuu ni kuvunja kile kilichounganishwa. Tusimpe nafasi.

Siku Kuu njema

Pd. Lawrence Muthee, SVD

Leave a comment