Masomo ya Jumapili kwa Kifupi: Krismasi B
Isaah 52:7-10; Psalms 97(98); Hebrews 1:1-6; John 1:1-18
Krismasi ni wakati wa kuhuisha

Wapendwa, leo ni Siku ya Krismasi, mojawapo ya nyakati mbili muhimu sana katika maisha ya Mkristo. Nyingine ni Kufufuka kwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo siku ya Pasaka. Kama Kristo asingezaliwa leo, hatungeokolewa na bado tungekuwa watumwa wa dhambi na mauti ya milele. Tena, kama Kristo angezaliwa na asingekufa wala kufufuka, basi Mtume Paulo anatuambia imani yetu ingekuwa bure (1 Wakorintho 15:12-14).
Jana usiku tulisherehekea usiku wenye utukufu zaidi wakati Kristo alipozaliwa ulimwenguni. Leo, Siku ya Krismasi, tunapata Habari Njema kwamba wokovu wetu umezaliwa Bethlehemu (ndani ya mioyo yetu). Sote tunapaswa kufanya haraka kwenda kumsujudia kama walivyofanya wachungaji na Maajusi kutoka Mashariki. Krismasi ni siku ambapo Mungu, kwa upendo wake wa dhati kwetu, aliamua kuwa kama sisi katika vyote isipokuwa dhambi, ili tuweze kuwa kama yeye na kurudisha taswira na mfano uliopotea. Tangu uumbaji, Mungu amekuwa akituweka sisi kwanza katika upendo wake ingawa mara nyingine hatumpi hata nafasi kwenye orodha ya vipaumbele vyetu.
Wakati wa semina ya Majilio wiki iliyopita, niliuliza waamini wachache waliohudhuria, wangefanya nini ikiwa rais wa nchi awaambie kwamba atatembelea nyumba zao. Baadhi walisema wangeuza baadhi ya mifugo ili kujenga nyumba nzuri miongoni mwa maandalizi mengine ya gharama kubwa watakayofanya. Nilipo wauliza kwa nini wangefanya hivyo, walisema kwamba ikiwa rais angewatembelea, maisha yao yangebadilika kwa njia nyingi, ikiwa ni pamoja na watu kuwaenzi na kuwaheshimu. Nilipo wauliza ni jinsi gani walivyokuwa wamejiandaa kwa ujio wake Mwana wa Mungu siku ya Krismasi, wengi hawakuwa na uhakika.
Tunaweza kusema kuwa sisi ni Wakristo, lakini ikiwa mambo ambayo Mkristo anapaswa kufanya mara kwa mara si kipaumbele kwetu, basi tunadanganya, na ukweli haumo ndani yetu. Mambo kama vile kuabudu Mungu Jumapili kanisani, kusali nyumbani na katika Jumuiya Ndogo za Kikristo, kusaidia wanyonge, na kuwa waaminifu kwa maadili ya Kikristo kama vile upendo kwa wote na uaminifu kwa wito wetu. Wengi wa Wakristo leo wanachagua kusherehekea Krismasi katika sehemu za burudani badala ya kanisani. Wengi wanashiriki katika shughuli ambazo hata zinapingana moja kwa moja na maana ya Krismasi. Unapanga kusherehekea siku ya leo vipi?
Kwa dhambi zetu, tunashindwa kupata neema ya Mungu na kutengwa naye na jirani yetu. Hata hivyo, Mungu hatuachi bali anaendelea kutuita kutubu na kuimarisha uhusiano wetu naye. Zamani, Mungu alijaribu mara nyingi kuokoa binadamu kupitia manabii kuanzia Musa hadi Yohane Mbatizaji lakini nguvu ya uovu ilionekana kuwa kubwa mno. Binadamu aliyeanguka hakuweza kuchagua Mungu katika hali hiyo ya aibu. Neno la Mungu lililotamkwa na manabii wengi bila mafanikio (soma somo la pili) lililazimika “kuwa mwili na kukaa kwetu” (Injili Yohane 1:14), ili kuleta uhuru wa kweli kwa mwanaume na mwanamke ili waweze kuchagua mema.
Hii ni habari njema ambayo Nabii Isaya anasema, “Jinsi ilivyo vizuri juu ya milima miguu ya wale wanaopeleka habari njema.” Wakati dunia inakabiliana na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na vita vilivyosababishwa na binadamu na majanga ya mabadiliko ya tabia ya nchi, pia yanayosababishwa na shughuli za binadamu, Krismasi inaleta ujumbe huu wa matumaini kwamba Mungu anarejesha uwepo wake katikati yetu. Mzaburi anatukumbusha kwamba “Bwana wetu ni Mfalme” na “Miisho yote ya dunia wameona wokovu wa Mungu wetu.”
Leo na wiki mbili zijazo za Krismasi, tunaitwa kuwa wabashiri wa habari njema kwa wale wanaotuzunguka. Kwa wale wanaohisi njaa, habari njema lazima ijumuishe kitu cha kula. Kwa wale wanaougua na kutelekezwa, uwepo wetu na sala zetu zitakuwa Krismasi kwao. Kwa wale wenye kukata tamaa na kuvunjika moyo, mshikamano wetu utakuwa Krismasi kwao na kadhalika. Kama vile Yohane Mbatizaji, tuna jukumu la kumtambulisha Kristo ulimwenguni na Kuruhusu mwanga wake uangaze kuondoa giza. Kwa kuwa Shetani kamwe aendi likizo na ni mwenye ubunifu daima, changamoto ya kauli iliyojitokeza ndani ya Kanisa kuhusu swala la baraka kwa mashoga hayafai kufunika faida za Krismasi. Tunaitwa kusimama imara zaidi kwa sababu kichwa cha Kanisa ambaye ni Kristo mwenyewe hawezi kamwe kuchanganyikiwa wala kutuchanganya. Masihi anajiandaa kurejesha uwepo wake ndani ya Kanisa, na kile tunachoona sasa kama wingu kubwa la machafuko na tishio kwa umoja wa Kanisa litageuka kuwa wakati wa kurejesha na kukuza imani yetu.
Wapendwa, Krismasi ni zawadi kubwa ya Mungu kwa binadamu. Kuzaliwa kwake kulifanya iwezekane kwetu kuwa kweli huru kutoka utumwa wa dhambi na adhabu ya milele. Mungu ni Baba yetu ambaye hafurahii kuona tunapotea. Leo tunapoadhimisha kuzaliwa kwa Kristo, tuwe macho kuitikia wito wa kurudi kwa Mungu na kusaidia wale waliopotea kuelewa upendo wenye huruma wa Mungu kwao.
Krismasi njema!
Pd. Lawrence Muthee, SVD
