Masomo ya Jumapili kwa kifupi:

Sherehe ya Kristu Mfalme

Ezekiel 34:11-12,15-17; Psalms 22(23); 1 Corinthians 15:20-26,28; Mathew 25: 31-46

Mfalme ni nani?

Wapendwa, leo ni Jumapili ya mwisho ya mwaka A wa liturujia ya Kanisa, na siku hii, tunasherehekea Sikukuu ya Kristo Mfalme. Jumapili ijayo itakuwa Jumapili ya kwanza ya Maajilio na mwanzo wa mwaka B wa liturujia ya Kanisa. Sherehe hiyo iliwekwa rasmi na Papa Pius XI mwaka 1925, katika kumbukumbu ya miaka 1600 ya Mtaguso wa Nisea uliofafanua mafundisho ya kuhusiana kwa Kristo na Baba, kama “Mwenye Umungu Mmoja na Baba”. Yesu alikuja kuleta Ufalme wa Mungu duniani ili dunia iweze kuokolewa kutoka na ufalme wa yule mwovu ambaye alikuwa amewaharibu wanaume na wanawake na kuwapotosha kutoka njia ya kweli, haki, na uadilifu. Katika ubatizo, sisi tunawekwa kuwa warithi wa Mfalme, ambaye ni Mungu Baba yetu.

Hata hivyo, mara nyingi tunaposikia kuhusu mfalme, tunafikiria utukufu, nguvu, utajiri, nyumba nzuri, ushawishi, n.k. Katika jamii yetu, kila mtu anataka kuwa mfalme, ambayo ni mojawapo ya sababu kuu za mizozo kati ya watu. Katika familia, wakati wazazi wanapigana juu ya nani anafanya maamuzi, watoto wanapigana juu ya nani anarithi nini wakati wazazi wao hawapo tena. Katika siasa, watu wako tayari hata kuua ili kupanda kwenye nyadhifa za nguvu kwa sababu ya fursa za kiuchumi zinazokuja na nyadhifa hizo. Katika Kanisa pia, “watu wa Mungu” wanatumia njia hata zisizo takatifu kufikia kilele cha hierakia. Uchaguzi katika Jumuiya Ndogondogo za Kikristo, Parokia, na mashirika ya kidini ni jambo la ushindani. Hata wanafunzi wa Yesu wenyewe walikuwa wakigombania nani angekuwa wa kwanza wakati Yesu alipotangaza kwamba atateswa na kusulubiwa (Luka 22:24-27).

Katika siku zetu kama ilivyokuwa wakati wa Yesu, watu wanatafuta nyadhifa za uongozi si kuhudumia bali kupata nguvu ya kushawishi mifumo ya jamii kwa maslahi yao binafsi na ya jamaa zao. Walei wanataka kuwa viongozi ili waweze kutoa zabuni za Kanisa. Watumishi wa kiroho wanataka kuwa viongozi ili waweze kudhibiti mali za Kanisa. Haya yote ni kwa sababu dunia haijui maana ya kuwa mfalme.

Yesu ndiye mfano wa kweli wa Mfalme na kwa maisha yake; anatufundisha mtazamo sahihi, tabia, na tunu za ufalme wa Mungu. Mungu alijifanya mwanadamu katika Kristo Yesu kutuonyesha kusudio la Mungu alipotuumba. “Yeye, ingawa alikuwa yuna namna ya Mungu, Yesu hakuhesabu kule kuwa sawa na Mungu, kitu cha kushikamana nacho; badala yake, alijinyenyekeza akachukua umbo la mtumwa…” (Wafilipi 2:5-8).

Watu waliomfuata Yesu pia walipata ugumu wa kutenganisha ufalme na utukufu, nguvu, na utajiri. Kwa kweli, hii ni moja ya sababu kuu kwa nini walimkataa kuwa Masihi. Tangu awali, Herode alihisi kitisho kutoka kwa mfalme mchanga. Wayahudi walidhani alikuwa yule atakayerejesha ufalme kwa Wayahudi. Wanafunzi wake walifikiria juu ya nyadhifa Yesu atakapokuwa Mfalme (Marko 10:35-45). Hata leo, wengi hawajaelewa bado dhana ya ufalme na uongozi ambao Yesu alifundisha na kupata katika ubatizo. Hata wale wanaojua, wanapendelea kuipuuza kwa sababu haina maslahi ya kidunia.

Katika somo la kwanza, nabii Ezekiel alitabiri juu ya mfalme atayekusanya kondoo waliotawanyika, kuwalisha, na kuwapumzisha. Yeye ni yule anayetafuta walioopotea na kuinua wale waliotupwa na kuvunjika. Mzaburi anamlinganisha na mchungaji anayetoa uhai wake ili kulinda kondoo zake. Badala yake, katika jamii yetu leo tunao wafalme wanaowanyanyasa wale wanayopaswa kuwaongoza, wachungaji wanaokula kondoo wao wenyewe, na viongozi kandamiza wakosoaji wao na kuwadhalilisha wanaopinga será zao.”

“Mfalme mzuri anapigana hata kutoa maisha yake kwa ajili ya kulinda watu wake kutokana na madhara. Yeye hana ghasia wala kisasi kwa wale wanaompinga. Yesu alitoa maisha yake mwenyewe kama fidia kwa maisha yetu ili atuokoe kutoka utumwa wa dhambi na mauti (Mathayo 20:28). Anatuongoza akiwa mbele, akifungua njia kwetu.

Katika somo la Injili, Yesu anatuambia kuhusu hukumu ya mwisho na vigezo vya kupima mastahili yetu kurithi ufalme wa Mungu. Wengi wanadhani kutoa misaada mikubwa bila upendo na heshima kwa wahitaji, na michango mikubwa kwa makanisa, ndiyo itakayowahakikishia mahali katika ufalme wa Mungu. Badala yake, Yesu anatuambia kwamba ni matendo madogo madogo ya kawaida yaliyojaa upendo na heshima yatakayotupeleka mbinguni. Siyo ziara moja moja kwa vituo yha watoto yatima tunayotangaza kwenye vyombo vya habari inayodhihirisha jinsi tunavyowajali maskini, bali ni vitu ukarimu tunaofanya kwa majirani wetu wa karibu. Tunapofanya mambo haya kwa watu walio karibu nasi kwa upendo na heshima, tunamfanyia Yesu mwenyewe. Ni mara ngapi naligawa chakula changu, nguo, muda, na nguvu zangu kwa wale wanaohitaji? Mara ngapi nawatembelea au hata kusali kwa ajili ya wagonjwa na wanaoteseka? Ninautumiaje wadhifa wangu kuboresha maisha ya wengine?

wapendwa, leo nawakaribisha kuchunguza jinsi tunavyotumia fursa za uongozi tunazopewa. Je, tunazitumia kuwainua wengine au kujiinua sisi wenyewe na jamaa zetu? Ikiwa utajiri tulionao ni matunda ya nafasi zetu na siyo bidii yetu, basi tunaweza kuitwa wezi wa mali ya umma. Aina hii ya utajiri haileti furaha ya kweli, badala yake inaharamisha hata vile tulivyochuma kwa jasho letu. Watu wangapi wanamiliki kila kitu ambacho pesa zinaweza kununua lakini hawana amani na furaha ya kweli katika familia zao? Watu wangapi wenye utajiri waliokufa, na utajiri wao ukageuka chanzo cha mzozo kwa jamaa zao? Utajiri ni wa nini, ikiwa hauwezi kumfanya mtu alale vizuri? Fikiria kuhusu hilo”

“Naamini una sherehe njema.”

Fr. Lawrence Muthee, SVD

Leave a comment