Utume wangu ni upi?

Masomo ya Jumapili kwa Kifupi: 29 A

Dominika ya Misioni Duniani

Isaya 45:1.4-6; Zaburi 96; 1 Wathesalonike 1:1-5; Mathayo 22:15-21

Utume wangu ni upi?

“Ndugu wapendwa, leo ni Jumapili ya 29 katika kipindi cha kawaida, na ni Dominika ya Misión au Utume ulimwenguni. Kamusi ya Kiingereza inafafanua Misoni au Utume kama ‘kazi maalum inayopewa mtu au kikundi cha watu.’ Kazi ni jukumu ambalo likitekelezwa kwa ufanisi huleta matokeo yanayotarajiwa. Leo ni ni siku ambayo tunakumbushwa juu ya utume wetu kama watu waliobatizwa, yaani, kueneza Kristo kwa watu wote wanaotuzunguka lakini pia utume wa wamisionari wote duniani, lakini pia kuwaombea wamisionari wote duniani. Mimi nikiwa mmoja wa wamisionari, leo ni siku maalum kwangu kutafakari juu ya utume wangu.

Mungu hakumuumba binadamu yeyote kwa bahati mbaya, bila kujali hali za mimba yake au ya mwingine. Wale wote wanaoandaliwa mimba wanapata utume uliotolewa na Mungu wa kutimiza ulimwenguni mara wanapozaaliwa. Hii inathibitishwa na ukweli kwamba sisi sote, hata wale bado hawajaizaliwa, ni wa kipekee. Kadiri tunavyojua, hakuna anayeshiriki vidole sawa na yeyote aliyezaliwa katika ulimwengu huu. Lakini Zaidi, kwa mujibu wa Ubatizo wetu, sisi wakristu tumefanywa washiriki wa utume wa Kristu wa Kuleta wokovu wa watu wote ulimwenguni. Mchungaji marehemu Myles Monroe alisema katika kitabu chake, “Fungua uwezo wako,” kwamba sote tunazaliwa na ufunguo wa kufungua mlango fulani ulimwenguni, na ikiwa tutakufa bila kufungua mlango huo, utaendelea kubaki umefungwa milele na ulimwengu hautaona au kunufaika na kilichomo ndani yake. Kwa maneno mengine, sisi sote tunazaliwa na uwezo wa kuwa kile Mungu alitupanga kuwa.

Hii inamaanisha kwamba bila kujali jinsi tunavyojiona au tunavyowaona wengine, sote tuna utume wa kutimiza. Leo sote tunakaribishwa kutathmini na kuona ikiwa tunatekeleza utume ambao Mungu ametupatia ulimwenguni ipasavyo. Kama mzazi, je, unafanya kile mzazi anapaswa kufanya ili watoto wako waweze kukua kulingana na mapenzi ya Mungu? Ninyi wahudumu wa Neno la Mungu na Sakramenti, je, mnatekeleza utume wenu kwa bidii na kwa uaminifu usioyumba ambao hubadilisha maisha? Walimu, je, mnatoa elimu sahihi kwa wanafunzi ili waweze kubadilisha maisha yao? Watoa huduma zingine zote, je, mnatekeleza majukumu yenu kwa kazi yenu kwa uadilifu na kuheshimu wale mnaowahudumia? Wanasiasa, je, mnajali masilahi ya watu mnaowaongoza na kutumia nafasi yenu kuleta amani, haki, na maendeleo kwa watu wenu?”

Kama jibu la maswali haya kwako ni ndiyo, leo ni siku yako ya kusherehekea kuwa mtume wa kweli. Ikiwa jibu ni la, au nusu nusu, leo pia ni siku yako ya kutubu na kuanza kufanya kile ulichotumwa kufanya ulimwenguni.

Katika somo la kwanza, tunasikia jinsi Mungu alivyotumia mfalme wa kigeni, Koreshi, kuwaachilia huru watu wale wa Israeli aliokuwa amewafunga. Hii inatuambia kwamba Mungu anaweza kutumia yeyote, hata maadui wetu, kutuletea wokovu. Kuna wimbo wa Injili kwa Kiswahili unaosema, “Anayekudharau siku moja atakusalimia kwa heshima.” Mfalme Koreshi labda hakugundua kwamba Mungu alikuwa akimtumia kubariki watu walewale aliokuwa amewasababishia mateso mengi. Watu wanaokuchukia na kusema uongo kukuhusu wanaweza siku moja kujikuta wakiimba sifa zako bila wao kujua. Wale waliofanya ukapoteza matumaini wanaweza wakawa njia yako ya mafanikio siku moja. Mungu atakubariki kupitia wao. Baraka zake zinaweza kuja kwa njia usiofikiria. Watu wanaokurudisha nyuma na kukukatisha tamaa katika utume wako huenda sio waovu mwishowe, kumbe wanakusaidia kufanya bidii na kufanya misuli yako iwe imara. Wale unaodhania wanakuvuta miguu unapopanda ngazi ya maisha huenda wakawa hawakuvuti bali bali wanakutegemea wewe nao kupanda. Ikiwa utakata tamaa na kurudi nyuma, wao pia watadondoka na utakuwa umefeli katika utume wako.

Katika somo la pili, Mtume Paulo anawasifu Kanisa la Thesalonike kwa imani yao thabiti. Paulo anaonyesha heshima kubwa kwao kwa sababu hawakuwa wakusikia tu Neno la Mungu, bali pia walikuwa wakilishika na kuliishi. Paulo anatualika siyo tu kuwa wasikilizaji wa Neno la Mungu bali pia watendaji. Neno la Mungu tunalolisikia kila Jumapili linapaswa kutufanya tuwe watu bora Zaidi – leo kuliko jana. Sisi ndio tunahitaji kuruhusu Neno kubadilisha maisha yetu na kutufanya kuwa bora kila siku. Ikiwa hatutafanya hivyo, tutaendelea kuwa kama mawe katika mto ambayo yako daima machafu na telezi licha ya mto kupita juu yao kila siku kwa miaka mingi.”

Katika Injili ya leo, tunaona jinsi Mafarisayo walivyoshirikiana na maherode, wakoloni na maadui wao, kujaribu kumtega Yesu. Inasemekana kwamba kuwa na lengo moja inaweza kuwaleta pamoja hata maadui. Kwa kutekeleza lengo lao la kumzuia Yesu kutekeleza katika utume wake, maadui hawa walijitahidi kushirikiana. Walipanga mtego madhubuti sana ili kumkamata Yesu. Hawakujua kuwa ujanja wao haungefika mbali. Kwanza, walimmiminia Yesu sifa ili  kumtega. Kwa kumuuliza Yesu ikiwa kulipa kodi kwa Kaisari ilikuwa sawa au si sawa; walidhani wamemfunga na kumdhalilisha katika madai yake ya kuwa Masihi au kumfitini na mamlaka ya Kirumi. Ikiwa angekubaliana na kulipa kodi, Wayahudi wenzake waliokuwa wamelemewa na uzito wa kodi nyingi za Kirumi wasingeridhika naye. Masihi alitarajiwa kuwakomboa watu wake wala sio kusaidia wakoloni wao. Ikiwa angekataa Kaisari asilipwe kodi, wangemshtaki kwa mamlaka kwa kosa la kuvunja sheria na kuchochea vurugu dhidi ya serikali.

Kama vile Yesu, sisi pia mara nyingine tunajikuta tumesongwa katika utume wetu. Watu ambao wameuza nafsi zao kwa shetani daima watajaribu kutuzingira ili kutuzuia kutekeleza utume wetu. Watu hawa si wageni bali ni watu wanaotuzunguka ambao bila kujua wamekuwa mawakala wa shetani. Wao hujipindua kulingana na inavyowafaa wao na utume wao wa kuharibu. Wanaweka mitego katika njia zetu ili kutubana kwa maneno au matendo yetu ili watufitini au kutudhalilisha. Pia, tunaweza kuwa mawakala wa shetani bila kujua. Njia pekee ya kujua hii ni kwa kutathmini mtazamo wetu kwa watu wengine wanaojitahidi kuishi wito wao. Ikiwa utagundua kuwa mafanikio ya wengine yanakuletea huzuni badala ya furaha, na wivu badala ya hamasa, unaweza kuhakikisha kuwa shetani ni bwana wako.

Kwa jibu lake, Yesu anaonyesha kuwa nguvu za binadamu haziwezi kushindana au kulinganishwa na Mungu. “Sanamu hii ni ya nani?” Baada ya yote, kila kitu kilichopo juu ya nchi ni mali ya Mungu. Kaisari alijitengenezea sanamu yake, ambayo haikuwa na uhusiano wowote na Mungu. Kumrudishia kile kinachokuwa chake haikuwa na uhusiano na utume wa Yesu. Kama mmisionari, nemegundua ukweli kwamba hakuna utume unaoweza kuleta matunda isipokuwa mtume awe tayari kupingwa bila kukata tamaa. Mchakato wa kubadilisha maisha ya watu uchukuwa muda mrefu na uchosha. Ni wale tu wanaojitoa wenyewe kama vyombo vya Roho Mtakatifu katika utume ndio uweza kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya watu. Vinginevyo, tunaweza tu kujaza nafasi na kutumia rasilimali ambazo hatukuchangia chochote kutafuta.

Ndugu zangu wapendwa, hatuwezi kuchanganya utume ambayo Mungu ametupa na biashara zetu za kidunia na kutarajia kumpendeza Mungu. Utume wa Mungu unapaswa kuwa utume pekee tunayouwazia katika maisha yetu. Ni lazima kuamini kwamba utume wa Mungu ndiyo pekee ninaohitaji kuwa nayo katika Maisha yangu. Ikiwa tuna utume kutoka kwa mtu mwingine, basi hatuwezi kutarajia msaada wa Mungu kuutekeleza. Utume wa Mungu daima unatambulika kwa upendo na kutafuta mema ya wote tofauti na faida na kutimiza masilahi binafsi. Tunapoadhimisha Dominika hii ya Misioni, tujitathmini wenyewe ni utume upi ambao Mungu amenipa kutekeleza wakati wa maisha yangu mafupi hapa duniani. Tuwe waangalifu kwa sababu shetani daima anatafuta mawakala wa kutekeleza utume wake wa kuharibu, kuchonganisha, kukatisha tamaa, na mengine kama hayo. Je, mimi ni wakala wa Mungu au shetani?

Jumapili ya Utume yenye baraka.”

Pd. Lawrence Muthee, SVD

Leave a comment